Sunday, November 29, 2015

Tukumbushane; Utumishi Wa Umma Na Swali La ' Nani Atauzima Mshumaa Wa Serikali?'

Ndugu zangu,
Kuna wakati Mama Maria Nyerere alipata kuulizwa swali la kukera kutoka kwa mwandishi kijana.
Mwandishi huyo alimuuliza Mama Maria Nyerere: “Hivi, inakuwaje Mwalimu ameondoka na kuacha familia yake ikiishi katika hali ya kawaida sana bila kuwa na mali nyingi wakati tunaona watendaji wa siku hizi wana mali na wengine wanasomesha watoto wao nje ya nchi?”
Mama Maria Nyerere alimjibu mwandishi yule: “Naona wewe bado ni kijana sana, hukuwepo wakati
ule wa Azimio la Arusha, lakini hiyo si sababu ya wewe kushindwa kufahamu ya nyuma, maana ulitakiwa kusoma.
Wakati wa Mwalimu kulikuwa na Azimio la Arusha na miiko ya viongozi. Na Mwalimu kama kiongozi, asingeweza kufanya tofauti na yale ambayo aliyasimamia na aliwataka wenzake katika uongozi wayafuate.”
Ndiyo, katika utaratibu wa sasa, na hasa baada ya kuondokana na kanuni, miiko na maadili ya uongozi ya enzi za Mwalimu, ni kawaida kukuta Watendaji wenye miradi ya biashara, mashamba na hata viwanda ambavyo wao wenyewe ndio wasimamiaji.
Hivi, Waheshimiwa hawa watapata wapi muda wa kusimamia biashara, mashamba na viwanda vyao kama si kuiba muda wa kuwatumikia wananchi na hata kutumia rasilimali za umma?
Inahusu swali hili; Ni nani atauzima mshumaa wa Serikali? Hapa kuna kisa nilichopata kusimulia.
Naam, miongoni mwa viongozi waliopata kuongoza dola ya Kiislam, hususan baada ya Mtume Muhammad (SAW) na baada ya masahaba, ni Amir muumini na Khalifa Umar bin Abdulaziz.
Wanazuoni wa Kiislamu wanatwambia, kwa utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ulijaa uadilifu. Si kwa viongozi tu, hata kwa raia wake.
Inasemwa kwamba moja ya mafanikio makubwa ya utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz, ni kukusanya zakka. Katika Uislamu, zakka ni ibada ya lazima kwa mwenye nacho kuwapa masikini, yatima, wajane, wasafiri, raia na wengineo wenye kuhitaji.
Watu walijengewa imani kubwa, kiasi hakuna aliyethubutu kukwepa kutoa zakka. Hata wale waliopokea zakka walikuwa waadilifu, hawakupokea zakka mara mbili kama walishapokea kabla. Wote waliostahili kupata zakka , walipata zakka. Hakika, zakka zilitolewa zikajaa mabohari.
Siku moja raia mmoja alikwenda kwenye ofisi ya Khalifa Umar bin Abdulaziz. Wakati wa maongezi yao, Khalifa Umar alikuwa akihangaika kuupuliza na kuuzima mshumaa mmoja na kuwasha mwingine.
Alikuwa na mishumaa miwili mezani. Kadri mazungumzo yalivyoendelea, Umar aliendelea kufanya hivyo. Alipuliza mshumaa mmoja ukazimika, kisha akawasha mwingine.
Jambo hilo lilimstaajabisha sana mgeni wa Khalifa Umar bin Abdulaziz. Akauliza: "Je; ni kwanini unazima mshumaa huu na kuwasha mwingine, kisha huo nao unauzima na kuwasha ule wa kwanza?
Khalifa Umar bin Abdulaziz akamjibu: "Mshumaa huu ni wa Serikali, wewe unaponiuliza habari za Serikali, nauwasha. Lakini naona mara unauliza habari za familia yangu, ndiyo maana nauzima wa Serikali na kuuwasha mshumaa wangu mwingine nilioununua kwa pesa za mfukoni mwangu. Nachelea nisije fanya dhuluma kwa mali ya nchi."
Ndugu zangu,
Bila shaka, hicho ni kisa chenye kutupa mafundisho muhimu
juu ya dhana nzima ya maadili katika utumishi wa umma. Tafakari!
Maggid,
Iringa.

No comments: