Saturday, December 5, 2015

SHINDA NYUMBA YA GLOBAL KUZINDULIWA WIKI IYAYO JIJINI DAR

file-page2
Bango la Shinda Nyumba ya Global Publishers (katikati) likiwa eneo la Karume Jijini Dar.
  file-page4
Bango likiwa eneo la Ubungo.

file-page6
Bango likiwa eneo la Tegeta.
BAADA ya kujihusisha na misaada mbalimbali ya kijamii na kiutu, Kampuni ya Global Publishers Ltd, wachapishaji wa magazeti pendwa na lile bora la michezo nchini Tanzania, imekuwa ya kwanza ya habari kutoa zawadi ya nyumba kwa wasomaji wake katika promosheni inayotarajiwa kuanza Desemba 11, 2015. Kumbukumbu zinaonesha kwamba, michezo ya kubahatisha imekuwa ikichezeshwa na kampuni mbalimbali za habari, lakini zawadi kubwa zaidi kutolewa ni magari. Meneja Mkuu wa Global, Abdallah Mrisho amesema wameamua kutoa zawadi hiyo ya nyumba ikiwa ni shukrani kwa wasomaji wao huku wakiamini shindano hilo litaongeza imani ya wasomaji kwa magazeti ya Global na litabadili maisha yao, hasa kwa atakayebahatika kushinda nyumba hiyo. “Tunaamini maisha bora ni pamoja na kuwa na nyumba bora, sasa promosheni hii ni changamoto kwa wasomaji wetu lakini lengo kubwa ni kuwarudishia shukrani kwa sababu tunaamini nao ni sehemu ya mafanikio yetu,” alisema. Global Publishers inayochapisha Magazeti ya Championi, Amani, Uwazi, Ijumaa Wikienda, Risasi, Ijumaa na Uwazi Mizengwe ambalo ni gazeti makini la siasa na uchunguzi, imekuwa ikijihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa misaada ya kiutu na zawadi kupitia mashindano na promosheni. Miongoni mwa misaada ambayo kampuni hiyo imekuwa ikitoa ni pamoja na kuwasaidia wanajamii kukabiliana na magonjwa mbalimbali huku wakiwa hawana misaada ya kumudu gharama za matibabu kwa kuwapeleka India na hospitali za hapa nchini. Misaada mingi ya matibabu imekuwa ikiwalenga watoto wenye vichwa vikubwa na uti wa mgongo ulio wazi, wenye vimbe mbalimbali ambazo zimeshindwa kufanyiwa upasuaji hapa nchini pamoja na wanajamii walioshindwa kumudu gharama za matibabu. Global Publishers Ltd pia imekuwa ikiunga mkono juhudi za serikali katika masuala ya maendeleo, ambapo imepata kutoa gari la wagonjwa (ambulance) huko Buchosa mkoani Mwanza. Aidha, kampuni hiyo imekuwa ikitoa misaada kwa jamii maskini nchini kwa kuziwezesha mitaji baadhi ya familia na kugharamia elimu kwa watoto wenye uwezo kielimu na nia ya kujiendeleza lakini wanashindwa kutokana na kukosa ada. “Sisi siyo matajiri na hatuna fedha za kutosha lakini tunaguswa na maisha ya Watanzania wenzetu ndiyo maana tuko tayari kugawana hata kile kidogo tunachopata,” anasema Eric Shigongo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global. Shigongo ambaye licha ya kufahamika kwa utunzi mahiri wa hadithi zinazogusa jamii, amefanikiwa pia kuwatia moyo na kuwafundisha wanajamii wengi kuhusu ujasiriamali huku akihimiza kujiamini na kuthubutu katika maisha. “Lengo letu kubwa ni kuona maisha ya mtu mmojammoja yanabadilika, kwa sababu kadiri jamii inavyokuwa na hali nzuri kimaisha, ndivyo maendeleo yanavyopatikana...hatuko kwa ajili ya kufanya biashara na kukusanya fedha, tuko kwa ajili ya kuibadili jamii iishi maisha bora na tunapoona mmoja anabadilika, kwetu ndiyo furaha,” anaongeza. Mbali na kutoa misaada kwa jamii, lakini pia kampuni hiyo imekuwa ikienzi mchango wa wasomaji wake kwa kutoa zawadi mbalimbali kupitia mashindano kama hayo. Tangu mwaka 2000 hadi sasa, Global Publishers imekuwa ikifanya Bahati Nasibu na kutoa zawadi mbalimbali kwa ajili ya wasomaji wake. Jumla ya magari matano, pikipiki kadhaa na safari ya kwenda China kwa msomaji wa Gazeti la Ijumaa Wikienda na pesa taslimu shilingi milioni kumi, zimetolewa kwa wasomaji wake hadi sasa. Magari yaliyowahi kutolewa kama zawadi za juu ni pamoja na Toyota Starlet, Toyota Vitz, Mitsubishi Pajero, Mercedes Benz, Toyota Noah na Toyota March. Zawadi ya nyumba inakuwa ya kwanza na ya aina yake nchini kutolewa na Global Publishers Ltd, hivyo wasomaji wanahimizwa kuichangamkia mchezo utakapoanza.

No comments: