Sunday, December 6, 2015

Tukumbushane: "Kwenye Maji Bwelele Mpumbavu Ndiye Hushinda Na Kiu..!"

Ndugu zangu,
NCHI yetu imo sasa mwanzoni kabisa mwa vita vya kweli kweli vya kupambana na panya ( Mafisadi) waliokuwa wakiitafuna hazina yetu.
Fikiri mwandishi wetu mahiri wa riwaya za upepelezi angelikuwa hai leo. Bila shaka, angemwona Willy Gamba katika Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, na kwa maelekezo ya Mkuu wake wa operesheni anavyovichua ' Njama' za maadui kuiangamiza nchi kupitia bandari zote; Majini Na Nchi Kavu. Kisha, Willy Gamba anavyochukua jukumu la kuongoza ' Kikosi Cha Kisasi' kupambana na waliotujeruhi kama taifa, kuhakikisha nao wanakiona cha mtema kuni.

Elvis Musiba, alipata kuandika riwaya za kusisimua zikiwamo ' Njama' na ' Kikosi Cha Kisasi'. Sterling katika riwaya hizo alikuwa mpelelezi mahiri na jasiri katika mapambano; Willy Gamba.
Ndugu zangu,
Ukiacha ya panya wa bandarini, nchi yetu iko sasa kwenye hatari ya kukumbwa na laana ya rasilimali. ( Resource Curse). Mabepari wanazinyemelea rasilimali zetu, tena kwa hila. Tumeanza sasa kugombanishwa kwa urithi tulioachiwa na wahenga wetu. Ni rasilimali zetu; gesi, mafuta, madini na wanyamapori wetu. Kwa mfano, tumeshaambiwa na imethibitishwa, kuwa tuna hazina ya gesi bwelele.
Kuacha rasilimali zetu ziwafaidishe matajiri na watu wetu wabaki kuambulia makombo si ujinga, bali ni upumbavu anaouzungumzia Msanii Bob Marley, kwamba kwenye maji bwelele ni mpumbavu ndiye anayeshinda na kiu.
Ona kwenye eneo la nishati. Tuna ugomvi mkubwa. Makampuni ya kigeni yanakuja na yanashindana hata kwa hila ya kutugombanisha ili yapate udhibiti wa kupitisha mirija ya kutunyonya. Tunakusanyaje kodi kutoka kwenye makampuni hayo?
Tunataka sasa viongozi wazalendo wa kweli watakaosimama kidete kutetea yale yaliyo na maslahi kwa wengi. Na wala wasijifanye watetezi wa wanyonge ili hali nao wanatanguliza tamaa ya kujikwapulia vitalu kwa kisingizio cha uwekezaji, kumbe wanataka kuhodhi ili nao waje kuongeza mitaji yao. Kwamba nao ni mabepari wenye kujali mitaji yao. Katika dunia hii hakuna tofauti ya unyonyaji. Kwa Mtanzania kunyonywa na Mzungu au Mtanzania mwenzake matokeo ni yale yale. Kunyonywa ni kunyoywa tu, haijalishi ni mrija mweupe au mweusi.
Ndugu zangu,
Tujiadhari pia na wakubwa kutuwekea viongozi wanaowataka wao ili wawatumikie. Kutuwekea vibaraka wao.
Ona kwenye hili la Tanesco; Ilianza na Baffour Beatty, Net Group Solutions, IPTL, Mechmar, Agreko, Songas, Richmond, Dowans na hata Symbion. Ni kama mbio za panya zenye kuishia ukutani. Kwamba hatusongi mbele.
Ni wakati sasa kuwa na kampuni yetu ya kizalendo ya kuzalisha umeme. Tuachane na hayo ya kigeni yenye kutuchanganya.
Na hakika, Bob Marley hakukosea alipoimba wimbo huu: Rat Race, mbio za panya.
http://www.youtube.com/watch?v=dCE3Ge4bCLk
"Political violence fill ya city, ye-ah!
Don't involve Rasta in your say say;
Rasta don't work for no C.I.A.
Rat race, rat race, rat race! Rat race, I'm sayin':
When you think is peace and safety:
A sudden destruction.
Collective security for surety, ye-ah!
Don't forget your history;
Know your destiny:
In the abundance of water,
The fool is thirsty.
Rat race, rat race, rat race!"- Bob Marley
Maggid ,
Iringa.

No comments: