Monday, May 29, 2017

WANACHAMA 681 KUTOKA UMOJA WA VIJANA WA CCM VYUO NA VYUO VIKUU MKOA WA DAR ES SALAAM WATUNUKIWA VYETI VYA KUHITIMU MASOMO YAO
“Ujana ni rika, ujana ni wakati na wakati haurudi nyuma” haya yalizungumzwa na  mgeni rasmi Ndg. Rodrick Mpogoro Naibu katibu Mkuu CCM Bara kwenye mahafali ya Vijana Chama Cha mapinduzi kutoka Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar es Salaam yaliyofanyika leo 28/05/2017 katika ukumbi wa King Solomoni Kinondoni.

Ndg. Rodrick Mpogoro alisema, Siri pekee ya kufanikiwa kwa mtu yeyote inategemea namna anavyotazama na kutathmini mambo. Ni mtazamo chanya pekee ndiyo humvusha mtu kwenye mafanikio, hivyo ipo haja kwenu vijana kujikita kutazama fursa zinazowazunguka na kuwa wabunifu ili kujitengenezea vipato vyenu wenyewe kuliko kusubiria ajira, alisema.

"Sura ya Chama Cha Mapinduzi inajengwa na wanachama wenyewe kwa vitendo, jengeni uadilifu, zungumzeni habari ya uzalendo wa nchi yenu, jengeni maslahi kwa wanyonge, jifunzeni historia ya Chama, someni katiba na kanuni zake, fanyeni kazi kwa bidii na jengeni moyo wa kujitolea mkifanya hayo mtafanikiwa. Alisema.

Akiendelea kuhutubia hadhara, Ndg. Mgeni rasmi alisema, ni vyema kwa  wanachama, wananchi na kila mpenda amani, umoja na maendeleo ya Taifa kuendelea kumuunga mkono Rais wetu Mhe Dr. John Pombe Magufuli katika juhudi anazozifanya za kupambana na ubadhilifu wa mali za umma kwani anaiishi misingi ya Chama Cha mapinduzi kama ilivyoainishwa kwenye madhumuni yake kupitia katiba Ibara ya 5. "Simameni imara katika kumuunga mkono Rais wetu kwani anaiishi misingi ya Chama Cha Mapinduzi katika kujenga uzalendo wa nchi".

Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama akiwemo Ndg. Shaka Hamdu Shaka K/Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Ndg. Daniel Zenda K/Katibu wa Vyuo na Vyuo vikuu UVCCM, Uongozi wa Senate Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar es Salaam na makada kutoka vyuo mbalimbali vya mkoa wa Dar es Salaam.

Sherehe hii ilihudhuriwa  na wanachama takribani 1,100 kutoka matawi ya vyuo mbalimbali vikiwemo DUCE, UDSM, DIT, ST. JOSEPH, ST.JOHN, MWL NYERERE, TAASISI YA WATU WAZIMA, IMTU, DMI, TIA, DIPLOMASIA, BAGAMOYO, CBE, DIT, KIU, MABIBO HOSTEL, CHUO CHA MAJI, IFM, USTAWI n.k ambao miongoni mwao walikuwemo wanachama waliotunukiwa vyeti vya kuhitimu masomo yao.
 

No comments: