Friday, January 2, 2009

Kalapina: 2009 ni mwaka wa kukomaa na hakimiliki, mafisadi wa redio

Ikiwa ni siku ya pili tangu tulipoukaribisha mwaka mpya wa 2009, ShowBiz ilipata chansi ya kupiga stori na kiongozi wa familia ya Kikosi cha Mizinga, Kalama Masoud a.k.a Kalapina au Nabii Koko ili kujua ni kitu gani kipya wanatarajia kukifanya mwaka huu.

Akiongea kwa kujiamini, Kalapina alisema kwamba, inawezekana mwaka huu ukawa ni wao kwasababu wamejipanga kuleta mapinduzi mengine kunako game ya muziki ya muziki wao ikiwemo kuanzisha bendi waliyoipa jina la ‘Kikosi’ ambayo itakuwa inagonga Hip Hop ‘live’.

“Vilevile tumerudisha studio yetu ambayo haikuwa hewani kwa muda ambayo hivi sasa tumeipa jina letu, ‘Kikosi Records’ badala ya House Of Music ambalo tulikuwa tukilitumia siku za nyuma na kugundua kwamba jina hilo lilikuwa gumu sana kwa baadhi ya watu, kwa kifupi mwaka huu tuko full,” alisema Kalapina.

Aidha, msanii huyo alisema kwamba, bado wataendelea na mapambano dhidi ya ufisadi, kitu ambacho walikianzisha na kufuatiwa na baadhi ya wasanii wa muziki wa Hip Hop Bongo ambao hivi sasa wanachana ‘live’ tofauti na mwanzo ambapo walikuwa wanaogopa kusema ukweli kuhusu ufisadi unaoendelea kufanywa na baadhi ya vigogo nchini.

“Mwaka huu pia tunataka kuwafumbua macho mashabiki ili wafahamu kwamba, ufisadi haupo kwa baadhi ya vigogo wa serikali tu, upo sehemu nyingine nyingi ikiwemo katika baadhi ya vituo vya redio na sehemu za huduma za ‘intaneti’ ambao wengi wao wamekuwa wakikopi kazi za wasanii bila idhini yao na kuziuza. Yaani hatutaficha kitu kwasababu tunataka kuwakomboa wasanii ambao kila siku wamekuwa wakiburuzwa na kunyonywa,” alisema Kalapina.

Kitu kingine alichokiongelea kiongozi huyo wa Kikosi cha Mizinga ni hakimiliki. “Mwaka huu pia tutakomaa mpaka sheria ya hakimiliki ambayo inalinda haki za msanii ipewe meno, vinginevyo tutaendelea kupiga kelele bila mafanikio au kuwakamata wezi wa kazi zetu, tukiwafikisha katika vyombo vya sheria wanaachiwa. Pia mwaka huu tunatarajia kuzindua documentary yetu ya ‘Hip Hop bila madawa’ ambayo imeshakamilika,” alisema.

No comments: