Tuesday, January 6, 2009

UYOGA: KINGA BORA DHIDI YA SARATANI


Virutubisho maalum vinavyopatikana kwenye uyoga, vimevuta hisia za watafiti wa kimataifa kwa zaidi ya miaka 20 sasa, ili kupata uhakika kwamba mboga hii ina uwezo mkubwa wa kutoa kinga kwa mwili wa mwanadamu dhidi ya ugonjwa wa saratani, ikiwemo ya matiti.

Uyoga una vitamini na aina nyingi za madini. Virutubisho vilivyothibitishwa kuwemo kwenye uyoga ni pamoja na: Vitamin B2, B3, B5, B6, B Complex pamoja na madini ya ‘Potasiamu’ na ‘Phosphorus’. Virutubisho hivyo ni muhimu katika mwili wa binadamu katika kutoa na kuimarisha kinga ya mwili kupambana na ‘wavamizi’ maradhi.

Aidha, inaelezwa kuwa uyoga ni chanzo kingine kizuri sana cha madini ya chuma (iron) na kopa ambayo yanahusika kwa kiasi kikubwa na usambazaji wa hewa ya oksijeni mwilini. Kupatikana kwa madini ya chuma na kopa kwenye uyago, ni jambo la kipekee ambalo linafanya mmea huu kuwa tofauti na muhimu.

Zikifafanuliwa zaidi faida za uyoga (Mushrooms), inaelezwa kuwa Vitamin B2 inayopatikana kwenye uyoga ni tiba tosha kwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kichwa unaojulikana kama ‘Kipanda uso’. Kiasi kidogo cha uyoga utakachokula kitapunguza kasi ya kuumwa kichwa hicho.

Vile vile Vitamin B inasifika kwa uwezo wake wa kuzuia uchovu wa mwili (Fatique) na akili hasa wakati wa kazi nyingi. Vitamin B3 husaidia kupunguza kiwango cha mafuta mabaya ya Kolestro mwilini, wakati Vitamin B6 yenyewe huondoa hatari ya mtu kupatwa na Kiharusi au moyo kusimama ghafla (Heart Attack).

Kama faida zote za kiafya zilizoorodheshwa hapo juu zinazopatikana kwenye uyoga hazitoshi, basi kuna faida nyingine ambayo inatokana na madini aina ya Zinc inayopatikana kwa wingi kwenye mboga hii. Zinc ina faida nyingi mwilini na miongoni mwa faida hizo ni pamoja na uimarishaji wa kinga ya mwili (Body Immune System).

Zinc si muhimu tu kwa kuimarisha kinga mwilini, bali pia kwa kuponya haraka vidonda mwilini. Vile vile mboga hii inasaidia sana ukuaji mzuri wa seli za mwili, huimarisha kiwango cha sukari mwilini na kukufanya kusikia ladha na harufu ya vyakula na vitu vingine ipasavyo.

Kwa ujumla, Uyoga ni mboga muhimu na inapaswa kuliwa na kila mtu anayejali afya yake kutokana na faida zinazopatikana humo. Kuanzia leo, jaribu kuweka Uyoga katika orodha ya mboga unazonunua kila wiki kwa ajili ya familia yako.

Bila shaka kwa wakazi wa miji midogo na vijijini, mboga hii hupatikana kwa wingi wakati wa mvua mvua na kwa miji mikubwa kama Dar es salaam, Uyoga unaweza kupatikana kwenye masoko maalum kama, Kariakoo, Kisutu na ‘Super Markets mbalimbali’.

No comments: