Monday, June 8, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!

Bambo

Kingwendu
Kingwendu, Bambo uso kwa uso
Wasanii wawili waliopata kutamba kupitia fani ya uchekeshaji, Rashidi Mwinshehe Said a.k.a Kingwendu na Dickson Makwaya ‘Bambo’ wanatarajia kupambana kupitia shoo moja kali itakayopigwa ndani ya Ukumbi wa Dar West, uliopo Tabata, Dar es Salaam.

Akipiga stori na safu hii, msanii Cool Braton wa Backyard Records ambao ndiyo waandaaji wa mpambano huo alisema kwamba, baada ya Dar West, siku itakayofuatia yaani Juni 20 mpambano huo utaendelea katika Ukumbi wa Kontena, Kihaba, mkoani Pwani. “Mshindi kunako ishu hiyo ataibuka na zawadi ya gari na atakayefuatia atalamba zawadi ya baiskeli,”.

Kwa upande wa Kingwendu ambaye tayari amekamilisha albamu yake mpya yenye jina la Sofi, alisema kuwa kuhusu mpambano huo yuko fiti na anachosubiri ni siku ya kumtoa nishai Bambo. Vile vile kwa upande wake Bambo alitamba kwamba, Kingwendu ni mtoto mdogo sana kwake ukizingatia yeye ndiye alimkaribisha kunako sanaa hiyo.
***********************************
Jumamosi iliyopita wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya walikuwa na shoo maalum katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, lengo likiwa kuchangia waathirika wa mabomu mbagala. Shoo ilidhaminiwa na Tigo na ilikuwa ya mafanikio kutokana na watu wengi kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo....

Kundi la Mabaga Fresh lilipiga shoo ya nguvu, kama anavyoonekana mmoja wa wasanii wa kundi hilo, JB.

Maunda Zorro naye aliwakilisha

Baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wakiinua mikono juu kuonesha ishara ya umoja baada ya kuungana na kupiga shoo ndani ya Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi kwa ajili ya kuwachangia waathirika wa mabomu Mbagala (Picha na Christopher Lissa)
*************************************************

Fake Smile ya Kanumba wiki ijayo
Muvi ya Fake Smile iliyochezwa na mastaa kadhaa waliopo kunako fani hiyo, akiwemo Steven Kanumba inatarajiwa kudondoka kitaani mapema wiki ijayo na kukata kiu ya wapenzi wa filamu za Kibongo ambao wanaisubiri kwa hamu.

Akipiga stori na safu hii juzi Kanumba alisema kwamba, filamu hiyo ilikuwa itoke Jumatatu ya leo lakini kutokana na kuiboresha zaidi itatoka rasmi Jumatatu ya wiki ijayo.

“Unajua baada ya kukamilisha zoezi la kupiga picha hapa Bongo tuliituma nchini Malaysia kwa ajili ya kuifanyia ‘editi’ katika kiwango cha kimataifa, kitu ambacho kitaifanya iwe katika kiwango cha juu kitakachoipeleka mbali zaidi,” alisema Kanumba.

Wasanii wengine waliofanya mambo makubwa ndani ya filamu hiyo ni pamoja na Richard Bezuidenhout, Aunt Ezekiel na wengine kibao.

***********************************

Prof. Jay, Dj Choka wazinguana!
Wakati Abby Cool & MC George Over The Weekend inaelekea mtamboni ilidondoshewa ishu kwamba msanii Joseph Haule a.k.a Prof Jizze na Dj wake, maarufu kama DJ Choka wametemana na hawatosimama jukwaani pamoja kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Akipiga stori na kipindi cha Bongo Fleva kilichorushwa hewani na Kituo cha Radio Clouds FM siku ya Jumamosi, Dj Choka alisema kwamba sababu iliyomfanya aondoke kwa Jay hata yeye bado haifahamu vizuri na amewataka mashabiki wake na wa Profesa waelewe kwamba hakuna bifu kati yao.

“Ishu yenyewe ni kwamba, hivi karibuni nilirudi home asubuhi (kwa Profesa Jay), kwa sababu usiku wa kuamkia siku hiyo nililala kwa washikaji ambao tulikuwa tunapiga nao kazi usiku, nilipoingia ndani ‘bro’ (Jay) akaniambia nirudi nyumbani (kwa wazazi wake Sinza), sikutaka kubishana nae kwakuwa alionekana yupo kwenye mudi mbaya.

“Niliamua kuondoka, nilipofika home moyo wangu ukaamua kutorudi tena kwa Jay wala kufanya naye kazi, najishangaa kufikia maamuzi hayo lakini imeshatokea sina jinsi, kwa sasa niko bize na blog yangu (bofya hapa) ambayo nina mpango wa kuifanya iwe tovuti,” alisema Dj Choka. Safu hii itacheki na Profesa Jay ili kujua ishu zaidi kuhusiana na hilo.
************************************
Steve White: P-Square wa Bongo waongo
Kama tulivyoahidi wiki iliyopita kwamba, wiki hii tutamtafuta mtayarishaji muziki, Steven Mayunga a.k.a Steve White na kupiga naye stori ili aweke wazi juu ya ishu iliyosemwa na wasanii Jonson na Jackson Mwomboke wanaofahamika zaidi kama P-Square wa Bongo ambao hivi sasa wako juu na ngoma yao yenye jina la ‘Usife Moyo’.

Ukiwa ni mmoja wa wasomaji ambao hukufanikiwa kuicheki safu hii wiki iliyopita, kupitia stori iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘P-Square wa Bongo wamburuza Steve White Studio’, wasanii hao walitamka kwamba, wakati wanarekodi ngoma hiyo walimuweka pembeni prodyuza Steve White aliyekuwa akiwarekodia kazi hiyo na kufanya sehemu kubwa ya traki hiyo wao wenyewe, kitu ambacho prodyuza huyo amekiita ni cha uongo.

“Kwanza naomba niseme kuwa sikufurahishwa na kauli ya uongo waliyoitoa wasanii hao mapacha ambao mimi nimewasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha albamu yao, halafu leo wanasimama na kusema waliniweka pembeni studio na kufanya kazi yao, kitu ambacho mtayarishaji muziki yeyote hawezi kukubaliana nacho.

“Kama walikuwa wanataka kujipaisha zaidi kupitia ishu hiyo wamechemka au wangenitafuta mimi kabla ya kwenda kuongea kwenye vyombo vya habari. Nakumbuka siku moja nikiwa nao kwenye intavyuu kupitia kituo cha Star TV, waliiwambia mashabiki wao kuwa mimi ni mtu ambaye wataendelea kuniheshimu kwa kuwa nimewasaidia mambo mengi, iweje leo waseme wao waliniburuza studio? Naomba niishie hapo,” alisema Steve White. Je, ni nani mkweli? Jibu unalo wewe msomaji.
*******************************************

Ebwana Dah!’ hii hapa tena, leo inamcheki staa wa kike kupitia muziki wa R&B, Christina Milian ambaye ana mvuto unaowadatisha wanaume wengi wakiwemo wale wenye majina makubwa, yakiwa ni maombi ya wasomaji wengi ambao walitamani kufahamu juu ya uhusiano wa kimapenzi wa mrembo huyo.

Kama ulikuwa haufahamu, Christina amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Nick Cannon ambaye ni mume wa mwanamuziki Mariah Carey, kabla hajaendelea kuwa na uhusiano na mastaa wengine wa kiume, hiyo ni kwa mujibu wa mtandao unaodili na mastaa wa nje kuhusiana na ishu hizo.

Mtandao huo uliendelea kuangusha ishu kwamba, baada ya kutemana na Nick mwaka 2005, Christina aliendelea kujiachia na mastaa wengine wa kiume kama mwanasoka Sol Campbell aliyefuatiwa na Andre Benjamin wa kundi la Out Cast. Baada ya kutoka kwa mchizi huyo Millian alitua kwa Eric West aliyedumu naye kwa mwaka mmoja.

Mcheza filamu maarufu, Jamie Foxx pia alipata chansi ya kula maisha na mrembo huyo kwa kipindi kadhaa kabla hawajatosana na kumuacha Christina akidondokea kwa Dre aliyedumu naye kwa miaka mitatu mfululizo, yaani mwaka 2006 hadi 2009.

Baada ya kuachana na Dre mkali huyo wa R&B alidondokea kwa Dream mchizi ambaye yuko naye hadi hii leo. Staa huyo wa kike ambaye ana umri wa miaka 27 na urefu wa futi 5 na nchi 2 sasa, alizaliwa Septemba 26, 1981 huko New Jersey, Marekani na kupewa jina la Christine Flores.
***************************************
Compiled by mc george

No comments: