Tuesday, September 11, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT


Madhara na jinsi ya kukabiliana na ukosefu wa choo!

Pengine naweza kusema kwamba matatizo mengi ya kiafya anayoyapata binadamu huanzia tumboni, hasa pale vitu vinapokuwa haviendi sawa humo. Chakula tunachokula kila siku, kinatakiwa kuingia tumboni na kusagwa, kuchujwa na masalia kutolewa nje kwa njia ya kinyesi.

Mchakato huo unaposhindwa kufanyakazi ipasavyo, masalia yanayobaki tumboni hugeuka na kuwa chanzo cha maradhi. Kwa kawaida mtu hutakiwa kupata choo sawa na anavyokula. Kama unakula mara tatu kwa siku, basi na choo hivyo hivyo, chini ya hapo ni mara mbili.

Kwa ujumla suala la ukosefu wa choo liko mikononi mwa mtu husika, kutokana na jinsi anavyokula na staili yake ya maisha anayoishi. Baadhi ya vitu vinavyosababisha mtu kupatwa na ukosefu wa choo ni kupenda kula chakula haraka bila kutafuna ipasavyo, ulaji wa kupindukia, unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji sigara.

Sababu nyingine ni kuwa na vidonda vya tumbo, msongo wa mawazo, kuwa na ugonjwa kwenye mfumo wa usagaji chakula na kutokunywa maji ya kutosha kwa siku kama inavyopendekezwa, lita moja mpaka mbili kwa siku.

TIBA MBADALA YA UKOSEFU WA CHOO

Ili kuepuka tatizo la kutokupata choo, kabla ya kula mlo wako kunywa glasi moja ya juisi ya limao ili kuondoa gesi tumboni na kuweka mazingira mazuri ya kusagwa kwa chakula utakachokila. kama tatizo la kutokupata choo limekuwa ni la muda mrefu, kunywa juisi ya ukwaju pamoja na papai bivu (angalau nusu) asubuhi kabla hujala kitu chochote.

Juisi ya ukwaju (glasi moja au mbili) na tunda la papai, vimeoanekana kuwa njia ya uhakika ya kulainisha choo, njia hii inaweza kutumika kama tiba mbadala kwa wale wenye tatizo hili kwa muda mrefu.

Kwa kawaida juisi na papai hutoa matokeo mara moja na iwapo hutapata choo kikubwa kwa siku ya kwanza, basi endelea kwa siku mbili au tatu zaidi na utaona mabadiliko makubwa tumboni mwako.

Tiba nyingine mbadala ni kunywa maji ya kutosha kwa siku na unaweza kuyanywa kila baada ya saa 2 au 3 huku ukichangaya kidogo na matone ya limau. Kwa wale wenye tatizo kubwa zaidi, wanaweza kujichua tumboni kwa mafuta ya kitunguu swaumu au mafuta ya soya.

LISHE YA MWENYE MATATIZO YA UKOSEFU WA CHOO

Ili kujiepuesha kabisa na tatizo la kukosa choo, epuka kupenda kula na kushiba mpaka unashindwa kupumua vizuri, kula chakula kiasi kama ilivyo kawaida mara tatu kwa siku. Ongeza kiwango cha kunywa maji kwa siku na usipendelee kunywa chai au kahawa, badala yake kunywa tangawizi, abdalasini (herbal tea), n.k.

Aidha katika mlo wako wa kila siku, jiepushe kula vyakula vyenye mafuta au vilivyopikwa kwa kukaanga. Epuka matumizi ya sigara na pombe za kupindukia. Zingatia kanuni ya ulaji matunda, milo mitatu kwa siku na ukishindwa basi angalau kula tunda moja, laweza kuwa papai, ndizi, embe, tufaha, chungwa, n.k. Utakavyokula matunda kwa wingi ndivyo utakavyojiepusha na matatizo ya tumbo na matatizo mengine mengi ya kiafya.

USHAURI MWINGINE

Epuka kuvaa nguo zinazobana. Tembea kwa miguu, angalau kwa dakika 30 kwa siku kama njia mojawapo ya kufanya mazoezi. Punguza msongo wa mawazo kwa kupumzika na kujiliwaza. Usifanye mchezo wowote mgumu mara baada ya kula. Fanya mazoezi ya mara kwa mara, kwani ni mazuri kwa mfumo mzima wa usagaji chakula.

Kama una tatizo la kumaliza siku moja au zaidi bila kupata choo, jua una matatizo, usikae kimya, chukua hatua sasa ili kujiepusha na matatizo makubwa ya kiafya siku zijazo!

Tuonane tena kwa makala nyingine wiki ijayo.

2 comments:

Anonymous said...

Naomba unisaidie kunielewesha kuhusu grape fruit(tunda la daranzi), huku niliko yanauzwa bei kubwa sana .

Anonymous said...

Kaka Mrisho mbona nilikuuliza swali hukunijibu? Nilikuuliza kuhusu mbegu za papai kama ni kweli zinatibu minyoo na amoeba lakini mapa lep kimya hukunijibu.Au blog yako hujibu maswali ya wadau?