Tuesday, June 3, 2008

Hatukuumbwa ili tuuguwe - 4

You Are what You Eat!
Wiki iliyopita niliahidi kuilezea kwa kirefu makala ya hewa ambayo ni muhimu katika suala zima la afya bora. Pasipo na hewa safi na ya kutosha, hata kama kuna lishe bora na yenye virubisho vya hali ya juu, maisha hayawezi kuwepo.

Hivyo hewa, maji na lishe bora ni vitu vinavyotegemeana. Kwa kuwa hewa ni kitu tunachokipata ‘automatic’, wengi hatujui kama inaathari yoyote katika afya na muonekano wa mtu.

JE, UNAHAKIKISHAJE UNAPATA HEWA YA KUTOSHA?
Inaelezwa kuwa mapafu yaweza kutanuka vizuri na kuingiza hewa mwilini iwapo mtu atasimama au kukaa akiwa amenyooka, vinginevyo kiwango cha hewa unachovuta hugandamizwa njiani na kushindwa kufika kwenye mapafu kwa kiwango kilichotakiwa.

Iwapo mapafu yatakosa hewa ya kutosha, damu nayo haiwezi kupata okseji ya kutosha na matokeo yake kila kitu mwilini hakiwezi kufanya kazi yake ipasavyo, hivyo ni muhimu sana kujifunza jinsi ya kukaa au kusimama huku umenyooka ili kuwezesha mzunguruko sahihi wa hewa mwilini.

Kwa juujuu, unaweza kuona kama ni jambo rahisi kuwa unapovuta hewa ndani inaingia na unapopumua inatoka hivyo kila kitu kiko sawa. Lakini inaelezwa kuwa ni 1/7 tu ya hewa tunayoivuta inafika kwenye seli zinazohusika. Katika mazingira hayo, ni muhimu sana kufanya mazoezi ya kupumua (deep breathing) angalau mara tatu kila siku ili kuyapa mapafu yako hewa ya kutosha.

Fanya zoezi la kupumua kwa kuvuta hewa nyingi ndani na kuizuia kwa muda kabla ya kupumua taratibu hadi mwisho na kisha kujizuia kwa muda kuvuta hewa nyingine. Rudia zoezi hili kama mara 20 hivi. Zoezi hili huboresha mzunguruko wa hewa mwilini na huondoa sumu (toxins) mwilini.

Wakati mzuri wa kufanya zoezi hili ni asubuhi kabla hujashuka kitandani na kabla hujafungua kinywa. Njia bora ya kujifunza zoezi hili ni kulala chali huku viganja vya mikono yako miwili vikiwa juu ya tumbo lako. Wakati unapandisha na kushusha pumzi mikono yako nayo itakuwa ikipanda na kushuka, zoezi hili liendelee hadi misuli ya tumbo itakapozoea kupanda na kushuka yenyewe kila unapopumua wakati wote.

Upumuaji wa namna hiyo unaonesha kuwa mapafu yote yanatanuka ipasavyo huku ikitilia mkazo sehemu ya chini ya mapafu na tumbo na kufanya damu ipate oksijeni ya kutosha na kwa upande mwingine viungo vingine vya mwili kufanyakazi zake vizuri na hivyo kumuondolea mtu uchovu usio wa lazima.

Pendelea kukaa nje kwa kadri iwezekanavyo, hata unapofanya mazoezi ya viungo, pendelea kufanya mazoezi hayo nje badala ya ndani. Hakikisha nyumba unayoishi ina mzunguruko wa hewa wa kutosha na mwanga wa jua na vivyo hivyo kwa sehemu yako ya kazi. Wakati wote kuwe na mzunguruko wa hewa wa kutosha na kusiwe na sumu.

Usiku unapolala, hakikisha unavuta hewa safi kutoka nje. Inashauriwa kuacha madirisha wazi ili hewa ya nje iweze kuingia ndani na ya ndani iweze kutoka nje (air circulation). Lakini katika mazingira haya, itategemea na hali ya usalama ya nyumba na eneo unaloishi, vinginevyo vibaka watakuliza.

Mtu anayelala kwenye chumba ambacho hakina mzunguruko wa hewa wa kutosha, aamkapo asubuhi hujisikia homa na mwenye uchovu, kwa sababu ya mwiwli kukosa hewa ya kutosha na hivyo kuubughudhi mfumo mzima wa mwili.

Kama inavyosisitizwa kila siku, usivute sigara wala usivute hewa yenye moshi wa sigara. Vile vile hatuna budi kuelewa kuwa ngozi yetu ya mwili nayo hupumua, hivyo ili ipate nafasi ya kupumua vizuri, unashauriwa kupendelea kuvaa nguo zilizotengenezwa kwa pamba asilimia 100, lineni, hariri au wool ambazo zinapitisha hewa mwilini.

Hewa bora kabisa hupatikana ufukweni mwa bahari (beach), kwenye maporomoko ya maji, msituni na penye mwanga wa jua. Sehemu hizi za asili zinauwezo wa kuhuishi seli za miili yetu pale inapopata hewa. Hata hivyo hewa itokanayo na kiyoyozi inaelezwa kuwa siyo bora sana.

UNAPOSIKI BARIDI UFANYAJE?
Inashauriwa kwamba unaposikia baridi usivae nguo nyingi badala yake fanya mazoezi kuupa mwili joto au kwa kutumia njia nyingine unayoona inafaa, lakini mara baada ya mwili kupata joto ondoa nguo za ziada ulizo vaa.

MADHARA GANI HUYAPATA MTU ASIYEPATA HEWA YA KUTOSHA?
Panapokuwa na upungufu wa oksijeni mwilini kunakosababishwa na kutokuvuta hewa ya kutosha, damu hutembea mwilini kwa shida. Uchafu na sumu sumu za mwili, ambazo zilipaswa kutoka mwilini kwa njia ya mapafu, hubaki mwilini na kuganda, hivyo kuichafua damu.

Viungo vingine vinavyoathirika kutokana na ukosefu wa hewa safi, si mapafu peke yake, bali tumbo, ini na ubongo. Ngozi hubadilika rangi na mfumo wa usagaji chakula huathirika. Vile vile inaelezwa kuwa ukosefu wa hewa ya oksijeni kwenye seli husababisha kansa. Majaribio yanaonesha kuwa ‘kansa’ haiwezi kuishi kwenye damu yenye hewa ya oksjeni ya kutosha.

Hivyo hewa ni miongoni mwa vitu muhimu anavyotakiwa binadamu avipate ili aweze kuwa na afya bora, pasipo na hewa safi, hapawezi kuwa na afya bora. Kama unavyoweza kuchagua maji ya kunywa na chakula gani ule, hewa unayovuta nayo unapaswa kuichagua.

Mwisho.

No comments: