Bw.Materego akiwaongoza wasanii kupima virusi vya UKIMWI katika zoezi lililoshirikisha zaidi ya wasanii na wadau wa sanaa 79.
Bi.Sidney Msamba akiwasilisha mada Kuhusu Mchango wa Wasanii katika Mapambano dhidi ya UKIMWI kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii.Kushoto ni Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia program yake ya kila wiki ya Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii limeendesha zoezi la kupima kwa hiari virusi vinavyosababisha UKIMWI kwa wasanii na wadau wa sanaa.Zoezi hilo lililoenda sambamba na mada ya ‘Mchango wa Wasanii Katika Kupambana na Virusi vya Ukimwi na Wao Kujikinga’ iliyowasilishwa na Mwanaharakati Kutoka Programu ya Monitoring and Evaluation Bi. Sidney P.Msamba liliendeshwa na shirikika la kimataifa la kupambana na virusi vya UKIMWI la AMREF na kuvuta idadi kubwa ya wasanii na wadau wa sanaa ambao walitaka kujua afya zao.
Awali akiongea kwenye Jukwa la Sanaa,Bi.Msamba alisema kwamba, wasanii ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya UKWIMWI hivyo hawana budi kuwa mstari we mbele katika kutambua afya zao na kuandaa kazi za sanaa zenye ujumbe wa kumaliza janga hili ambalo limekuwa likimaliza nguvu kazi ya taifa na kuacha familia nyingi zikihanganika.
Alisema kwamba, kazi za Sanaa hasa filamu na muziki zina uwezo wa kusafiri mbali na kupenya maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kuwa chanzo kikubwa cha elimu dhidi ya UKIMWI na kushusha kiwango cha maambukizi ambacho kwa sasa kimefikia asilimia 5 ya watanzania wote yaani zaidi ya watanzania milioni mbili.
“Kazi zetu za Sanaa tunazozifanya zitumike kueneza elimu dhidi ya UKIMWI.Ieleweke kwamba hili ni janga la taifa ambalo lazima wasanii tulitambue na tushiriki walau kwa asilimia 10 itasaidia sana.Tukishindwa kusaidia mapambano haya hata wateja wetu wa kazi za sanaa wataisha” alisisitiza.
Alimalizia kwa kuwakumbusha wasanii kwamba, wana kazi kubwa ya kuhakikisha hawawi wachochezi wa virusi vya UKIMWI kupitia matendo na kazi zao za sanaa kwani wanapaswa kuwa kioo na kuhakikisha muda wote wanakuwa mstari wa mbele katika kujenga jamii yenye maadili na iliyoelimika juu ya virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga (UKIMWI).
“Sisi wasanii ni sehemu kubwa ya mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI,hatutakiwi kuwa mabalozi wa kusambaza habari za kuiharibu jamii na kuiingiza kwenye majanga ksms hili la UKIMWI bali mabalozi wema wa kuhakikisha vita hii dhidi ya UKIMWI inapiganwa kila kona” alimalizia.
Akiahirisha program ya wiki hii, Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema kwamba, wasanii hawana budi kuwa mstari wa mbele kupambana na majanga mballimbali katika jamii kwani kazi zao zimekuwa zikiifikia jamii na kufikisha ujumbe kwa urahisi.
Hata hivyo alionya juu ya maadili mabovu yanayooneshwa na wasanii hasa uvaaji wa nusu uchi kwa kisingizio cha kutafuta masoko ya kazi zao na kusisitiza kwamba huko ni kupalilia janga la UKWIMWI na kwa kuendelea hivyo hakutakuwa na hatua itakayopigwa kwenye mapambano hayo.
Katika zoezi hilo la kupima virusi vya UKIMWI jumla ya wasanii na wadau wa Sanaa 79 walitambua afya zao ambapo wanaume walikuwa 39 na wanaume 79.
No comments:
Post a Comment