MADA: MAHUSIANO
Kama
ilivyozoeleka,blogu hii inaelemea zaidi katika masuala ya siasa.Lakini
kuna nyakati ninajaribu kuangalia nyanja nyingine za maisha katika
jamii.Na kwa bahati nzuri kabla ya kuzamia kwenye Siasa kitaaluma
nilikuwa mwanafunzi wa Sosholojia (ndio mchepuo niliosoma katika Shahada
ya Kwanza hapo Mlimani).
Ninajaribu
kuanzisha utaratibu ambapo angalau mara moja kwa wiki nitajadili mada
ya kijamii,hususan masuala ambayo ni ya kibinafsi zaidi kama vile
mahusiano,mapenzi,nk.Nakaribisha michango na maoni kutoka kwa wasomaji.
Leo ninaanza na jinsi mwanaume anavyoweza kukabiliana na kuvunjika kwa uhusiano kati yake na mwanamke.Karibu sana.
JINSI YA MWANAUME KUDILI NA KUVUNJIKA KWA UHUSIANO NA MWANAMKE
Pointi tatu muhimu za kuzingatia:
- Kwanza unapaswa kufuta kumbukumbu zote za uhusiano uliovunjika
- Jaribu kutumia muda mwingi kuwa karibu na watu 'uliowapuuza' wakati ukiwa 'bize' na mwandani wako.Watu hao wanaweza kuwa familia yako,ndugu zako au marafiki zako
- Kisasi kikubwa dhidi ya aliyekubwaga ni mafanikio.Kwahiyo hamasika kupata mafaniko ili 'ulipe kisasi.'
Hakuna
anayeweza kubisha kwamba moja ya mambo magumu kwa manaume yoyote yule
(na kwa wanawake pia) ni pale uhusiano na mwenza wako unapovunjika.Mara
nyingi wanaume wengi wanapokumbwa na tatizo hilo hujipa matumaini potofu
kwamba maisha yataendelea kama kawaida licha ya ukweli kwamba mioyoni
mwao wanaumia vya kutosha.Wengi huendelea kujifariji na matumaini 'feki'
kuwa wenza waliowabwaga watarejea.
Matokeo
ya matumaini hayo 'feki' ni mithili ya mkuki wa kukataliwa wenye makali
pande zote (double edged sword of rejection).Kwanza ni maumivu
yanayotokana na ukweli kwamba umebwagwa,na kisha ukweli mwingine
unaofuatia baadaye kuwa matarajio feki kuwa mwenza
atarejea,well,yalikuwa feki.Mwenza wako ndio ameondoka moja kwa moja,na
hatorejea (hapa tunazungumzia kubwagana ambako hakuna dalili wala
uwezekano wa suluhu).
Lakini
maumivu haya yanaweza kufupishwa kwa aliyebwagwa kutambua kuwa hali
ndio hiyo-ameshabwagwa na hakuna uwezekano wa kurejea katika hali
ilivyokuwa awali.Kuendelea kusubiri na kutarajia miujiza ni sawa na
kujifungia kwenye mzunguko wa mateso usio na mwisho (endless circle of
turture).
Kwahiyo ili kumudu kuendelea na maisha yako ya kawaida baada ya kubwagwa (au hata kubwagana) jaribu kufuata njia zifuatazo:
ACHA KUJILAUMU
Mara
nyingi sie wanaume tumejenga tabia ya kuwa mithili ya watoto wakubwa
(big babies) ambapo hatuachi kujilaumu.Kubwagwa ni kama kunaongeza
ukubwa wa tabia hii.Kuna wanaochukulia kubwagwa kama mwisho wa
dunia,yaani kana kwamba kuondoka kwa mwenza wako maishani mwako ni kama
ameondoka na sababu ya wewe kuendelea kuishi.
Lakini
ukijaribu kidogo tu kujiuliza "Niliishije kabla sijakutana na huyu
aliyenibwaga?" utagundua kuwa ulikuwa ukiishi kama kawaida,na kama
binadamu wengine.Kwahiyo,huu ni ushaidi tosha kuwa kama uliwahi kuweza
kuishi bila mwenza aliyekubwaga ni dhahiri unaweza kuishi pia baada ya
mwenza huyo kuondoka maishani mwako.Acha kujilaumu,jipange upya,na
endelea kuishi.
FUTA KUMBUKUMBU
Kama
nilivyoandika hapo juu,wengi wa wanaume wanaobwagwa huendelea kuwa na
matumaini 'feki' kuwa mwenza aliyeamua kuondoka atarejea.Kwamba labda ni
tisha toto tu,au anatikisha kiberiti tu.Mara nyingi wanaume
tunapobwagwa hatupendi kukiri hadharani kuwa inatuuma.Wengi wetu
hujifanya jasiri mbele ya 'washkaji' zetu tukijigamba kuwa 'ahh yule
demu anadhani mimi nitababaika kwa vile tumeachana' (actually huwa
tunakwepa kutumia neno 'kanibwaga').
Kiasili,katika
mahusiano wanaume wengi wanapenda kuwa ndio walioshika usukani.Kwahiyo
hata wanapobwagwa bado watajaribu kudanganya umma kuwa wao ndio
waliokuwa wa kwanza kubwaga.Lakini kimsingi huko ni kujidanganya kwa
sababu hao unaojaribu kuwaaminisha ujasiri wao hawajali sana (na pengine
nao wana ishu zao binafsi zinazowanyima nafasi ya kujihangaisha na ishu
zako).
Penigne
una picha za mwenza aliyekubwaga,au zawadi mbalimbali alizokupatia
wakati wa uhusiano wenu.Licha ya kubwagwa,unaweza kuogopa kuzitupa kwa
hofu kuwa labda atarejea na akikuta azawadi alizokupatia hazipo
atakasirika na kuondoka tena.Tumia akili yako vizuri.Ameondoka
jumla,hatorudi.Usijaze bure nafasi kwenye albamu yako au kwenye sehemu
unapoweka zawadi/kumbukumbu zako kwa matarajio hewa.
Uwepo
wa kumbukumbu hizo (picha, zawadi,nk) ni sawa na uwepo wa mwenza
aliyekubwaga kiroho japo si kimwili.Kila utakapoziona utaendelea
kumkumbuka na kutamani awepo au arejee maishani mwako.Ukweli ni kwamba
hatorejea.Cha kufanya basi ni kuteketeza kila kumbukumbu ya huyo
aliyekubwaga.Hufanyi hivyo kwa ajili ya hasira bali ni kujipa nafasi ya
kuendelea na maisha yako kama yalivyokuwa kabla hujakutana
naye.Kumbuka,utakapopata mwenza mwingine hutazihitaji kumbukumbu
hizo,sio tu kwa vile tayari una mwingine lakini pia itamsaidia mwenza
wako mpya kupata uhakika kuwa wewe ni wake peke yake.
JIREJESHE KWA ULIOWATELEKEZA
Wengi
wetu tunafahamu jinsi mapenzi motomoto yanavyoweza kutuweka mbali na
watu wetu wengine wa karibu.Si kwamba tukiwa kwenye mapenzi tunawasahau
watu hao lakini mara nyingi ni maotkeo ya kuweka akili na nguvu zaidi
kwenye mahusiano yetu na wenza wetu,na hivyo kupata fursa finyu ya kuwa
karibu na watu wetu wa karibu (kwa mfano wanafamilia wenzetu,ndugu,jamaa
na marafiki).
Kufanya
kosa si kosa bali kurejea kosa.Na alimradi wakati uko na mwenza wako
hukuwafanyia dharau watu wako wa karibu basi ni dhahiri utakaporejea
kwao (na pengine kuwafahamisha bayana kuwa umebwagwa) watakuwa radhi
kukupokea.Kuwa karibu na watu wako wa karibu kutakusaidia sana
kukarabati maisha yako,hasa kwa vile walikuwa nawe hata kabla hujakutana
na huyo aliyekubwaga.
Kumbuka,mara
nyingi hawa ni watu wanaokupenda kwa dhati- aidha kwa vile ninyi ni
damu moja au ni watu uliopitia nao kwenye milima na mabonde.Kwa
wanafamailia na ndugu,hawa kiasili ni watu ambao tunapaswa kuwa nao kwa
vile tofauti na uchaguzi tunaokuwa nao kudeti mtu fulani au la,sheria za
kibinadamu hazitupi fursa ya kuchagua nani tuzaliwe naye au
atuzae.Ukaribu na watu wako wa karibu utasaidia kukukumbusha nani mwenye
umuhimu wa kweli katika maisha yako.
USIKURUPUKE
Hapa
unaonywa usikurupuke kutaka kuanzisha uhusiano mwingine kuziba pengo la
yule aliyekubwaga.Uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi jitihada za haraka
haraka kutaka kuziba pengo hilo huishi kwenye maumivu/majonzi zaidi
kuliko mafanikio.Tatizo kubwa hapa ni kwamba katika papara ya kutaka
kuziba pengo hilo,unaweza kukosa muda wa kumwelewa vyema huyo
'unayemfukuzia.' Mara nyingi jitihada hizo huelemea zaidi kwenye kupata
'demu bomba zaidi ya yule aliyenizingua.' Lakini kama wasemavyo
waswahili,usione vyaelea vimeundwa.Huyo 'demu bomba' anaweza kuwa na
mwenza wake au ana 'pozi nyiiingi' ambazo sana sana zitaishi kukuumiza
tu.
Suluhisho
ni 'kutuliza boli.' Vuta pumzi.Angalia sababu zilizopelekea ukabwagwa
au mkabwagana na mwenza aliyetangulia.Ukishaelewa chanzo/sababu
itakupatia nafasi nzuri ya sio tu kuepuka kurejea makosa ya awali bali
pia kujenga uwezekano wa kupata mtu aliye bora zaidi ya aliyetangulia.
JIHAMASISHE
Wengi
wetu tunapobwagwa tunakuwa mateka wa hasira.Na katika hasira hizo
baadhi yetu hujikuta tukifanya vitu vya kitoto,kijinga na visivyo na
maana kabisa.Si ajabu kuona mtu akibwagwa akakimbilia kwenye waal ya
Facebook profile ya aliyembwaga na kutundika 'madudu' yenye lengo la
aidha kumuumiza mhusika au kujaribu kumshawishi arejee.Unaweza kukidhi
mahitaji yako kwa dakika au siku chahe lakini mara nyngi matokeo ya
'upuuzi' wa aina hiyo huwa sio mazuri hasa pale utakapobaini kuwa
'kujigonga' kwako hakujafanikiwa kubadili msimamo wake.
Kumbuka,aliyekubwaga
anaweza kuwa anafuatilia kwa karibu namna unavyodili na uamuzi
wake.Matarajio ya wengi wanaobwaga wenza wao ni kuwa aliyebwagwa
ataumia,atakonda,atateseka au,kwa hakika,ataaanza kubembeleza.Hiyo ni
attention seeking.Na hakuna dawa mwafaka kwa attention seekers kama
kuwapuuza.Kuendelea na maisha yako kana kwamba hakuna lililotokea sio tu
itakuwa kama kumwadhibu attention seeker aliyekubwaga (ie kuvunja
matumaini yake kuwa amekuumiza na labda utambembeleza) bali pia utakuwa
unajisaidia wewe mwenyewe kuendelea na maisha yako kama kawaida.
Kisasi
kikubwa kabisa kwa aliyekubwaga ni kwa wewe kupata mafanikio.Yaani
badala ya wewe kuonekana umekondeana kwa mawazo ya kubwagwa,siku ya siku
unakutana na aliyekubwaga na kukuona ukiwa mwenye furaha na
mafanikio.Na kwa vile 'what goes around always comes around' si ajabu
aliyekubwaga kwa wakati ho atakuwa anajutia kwanini alichukua uamuzi
huo-lakini hawezi kukubembeleza mrejeane kwa sababu yeye ndiye aliyeamua
bila kulazimishwa kuwa mwachane.
Pata
picha,baada ya kubwaga unaelekeza nguvu zako kwenye kujiendeleza
kimaisha (kitaaluma au kikazi),unatumia muda wako kujenga mwili wako kwa
mazoezi, na kwa vile Mungu humjalia kila anayejituma,unafikia mafanikio
yanayoweza kugeuza shingo za watu (ya kutamanisha).Mafanikio ni sawa na
sumaku,lazima yatakusaidia kuongeza nafasi zako za kupata mwenza
bora,pengine bora zaidi ya yule aliyekubwaga.Sasa siki ua siku,mwenyewe
umenawiri vyema kutokana na kazi inayolipa vyema,na pembeni una mwenza
bora,kisha unakutana na aliyekubwaga awali akiwa kachoka kimaisha na
pengine akiwa na mwenza wa ovyo ovyo.Anashindwa kujizuia na kujikuta
anakuuliza "hey fulani uko wapi siku hizi...naona mambo si
mabaya..."Usiwe na haraka ya kujibu bali jitahidi kadri uwezavyo kuachia
kicheko cha dharau....na badala ya kujibu swali lake mkebehi kwa
kurejea swali lilelile na pigiria msumari kwa "hata wewe naona mambo si
mabaya"...na kicheko kingine..Hiyo inaitwa kushinda vita bila kwenda
vitani.
AMKA NA ENDELEA NA SAFARI
Vyovyote
utakavyofanya huwezi kumzuia mwenza aliyedhamiria kukubwaga.Pengine
amepata mtu aliye bora zaidi yako,pengine ameamua tu.Kama binti
anatamani kuwa na mtu mwenye uwezo mkubwa kifedha kuliko wewe,kuendelea
kumbembeleza mwendelee kuwa pamoja kutakuingiza kwenye vishawishi vya
ufisadi,au matendo mengine mabaya ambayo si ajabu badala ya kukusaidia
kumridhisha mwenza wako yakaishia kukupeleka jela.Naamini umeshaona au
kuskia stori kibao za watu waliolazimika kujiingiza kwenye uhalifu ili
kupata fedha za kuwaridhisha wenza wao.
Of
course,mwenza wako ana haki ya kutaka kilicho bora.Lakini hiyo sio
sababu ya kutaka uurefushe mkono wako zaidi ya uwezo wake.Mwneza wako
ana haki ya kukupa changamoto za koboresha maisha yako/yenu lakini sio
kwa namna ya kukusukuma uhatarishe maisha yako kwa ajili
yake.Kumbuka,kama maisha yake ni muhimu,yako ni muhimu pia.Kama
anakupenda kwa dhati atakubaliana na hali yako alimradi isiwe hali yako
ni matokeo ya uvivu au uzembe wako au uoga wako kijituma.
Kwa
hiyo badala ya kuendelea kuifanya hali ngumu (kubwagwa) kuwa ngumu
zaidi,futa machoz yako,amka na endelea na maisha yako.Katika saikolojia
kuna imani kwamba mengi ya tunayoyaita matatizo ni matokeo ya fikra zetu
tu.Njaa,kwa mfano,si lazima imaanishe mahitaji ya mwili (tumbo) bali ni
fikra kuwa tumbo linahitaji kitu fulani.Tamaa ni hali ya kutamani
usichokuwa nacho hata kama si cha muhimu.Badala ya kujipa moyo kuwa
mwenza wako atarudi aua atajilaumu kukubwaga,kwanini usielekeze fikra
zako kwenye masuala mengine ya muhimu katika maisha yako?Kumbuka wewe
ndiye nahodha ya maisha yako,kumkabidhi mtu mwingine jukumu hilo sio tu
kunaondoka uhuru wako wa kukufikisha unakotaka kwenda bali pia kuna
hatari ya kupotezwa.
Kwa leo inatosha!
MAKALA HII IMEANDALIWA KUTOKANA NA VYANZO MBALIMBALI MTANDAONI HUSUSAN MTANDAO WA AskMen
MAKALA
IJAYO ITAZUNGUMZIA IMANI ILIYOJENGEKA MIONGONI MWA MABINTI/WANAWAKE
WENGI WA KITANZANIA KUWA WANAUME WA KITANZANIA NI MAHIRI KWA KU-CHEAT,AU
KUNUKUU KIUSAHIHI, "OVYO KABISA", "BURE KABISA", "CHU*I MKONONI", NA
KAULI KAMA HIZO.KICHANGAMSHA UBONGO: JE TABIA YA MWANAUME (AU MWANAMKE)
INA MAHUSIANO YOYOTE NA URAIA WAKE?
HADI MUDA HUO,NAKUTAKIA SIKU NJEMA - By Chahali
No comments:
Post a Comment