Thursday, May 24, 2018

Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza kuendelea kuboresha uhusiano wa kibiashara

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto) akizungumza na baadhi ya maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, juu ya kuangalia njia bora za kudumisha uhusiano baina ya Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza nchini, katika Makao Makuu wa Magereza, jijini Dar es salaam, Mei 23, 2018. Kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dokta Charles Kimei leo amekutana na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Dokta Juma Malewa ili kuangalia njia bora zaidi za kudumisha na kuboresha uhusiano baina ya pande zote mbili. Akizungumza katika mkutano huo ambao pia ulijumuisha maafisa waandamizi kutoka Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza, Dokta Kimei alilishukuru Jeshi hilo kwa kuwa mdau mkubwa wa Benki kupitia mikopo, akaunti za mishahara za askari na SACCOSS ya Magereza ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitoa huduma kwa askari Magereza.

“Nichukue fursa hii kulishukuru Jeshi la Magereza kwa biashara ambayo limekuwa likitupatia, niipongeze SACCOSS ya Magereza kwa uamuzi wa kuwa Wakala wa FahariHuduma, hii si tu itawaongezea kipato kupitia kamisheni za uwakala, pia itasogeza huduma za kibenki karibu na Maaskari Magereza”, alisema Dokta Kimei.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa akizungumza katika kikao na uongozi wa Benki ya CRDB, uliomtembelea ofinisi kwake, Makao Makuu ya Magereza jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei. 


Akielezea juu ya fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB kwa wafanyakazi Dokta Kimei alisema hivi karibuni Benki imeshusha riba inayo toza katika mikopo binafsi toka 20% mpaka 17%, muda wa marejesho umeongezwa toka miezi 72 hadi miezi 84, wakati kiwango cha kukopa kimeongezwa kutoka shilingi milioni 50 mpaka kufikia Shilingi Milioni 100 hivyo kuwapa wateja wigo mpana zaidi wa kukopa ili kufikia malengo.
Dokta Kimei pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha askari wa Jeshi la Magereza kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo huku akibainisha ya kuwa Benki ya CRDB imeanzisha utaratibu maalum wa kununua madeni na mikopo ya askari kutoka katika Taasisi zingine za Kifedha. Hivyo kutoa fursa kwa askari wenye mikopo Benki nyingine, kukopa toka Benki yao pendwa ya CRDB. Mpaka kufikia mwisho wa mwezi Aprili 2018 tayari Benki ya CRDB ilikuwa imeshakopesha zaidi ya maofisa 5,415 wa Jeshi la Magereza ambapo jumla ya shilingi 29.4 bilioni zilikuwa zimekopeshwa kwao.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto) akimkabidhi zawadi maalum, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa, wakati alipomtembelea ofisini kwake, Makao Makuu wa Magereza, jijini Dar es salaam, Mei 23, 2018. Mkutano huo ulikuwa na lengo kudumisha uhusiano wa kibiashara baina ya Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza nchini. 


Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Dokta Juma Malewa alimshukuru Dokta Kimei kwa kutembelea Jeshi hilo na kuipongeza Benki ya CRDB kwa maboresho hayo katika huduma zake, huku akiisifu zaidi huduma ya Salary Advance ambayo alisema kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha maisha ya askari. Dokta Malewa alisema katika maboresho hayo yanayoendelea Jeshi la Magereza lingependa kutumia mfumo wa kibenki katika kukusanya mapato yake katika miradi na huduma mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“Nikuombe Dokta Kimei na uongozi mzima wa Benki ya CRDB kuona uwezekano wa kuweka huduma za kibenki kama ATM na Matawi kwenye maeneo ya Magereza yenye uhitaji mkubwa wa huduma hiyo”, aliongezea Dokta Malewa. Dokta Malewa pia aliiomba Benki ya CRDB kushiriki katika miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa na Jeshi hilo ikiwamo ujenzi wa hospitali ya Jeshi la Magereza Ukonga, miradi ya Kilimo cha kisasa na chenye tija, mradi wa kokoto Msalato pamoja na uwekezaji katika miradi ya viwanda vidogo vidogo.
Baadhi ya Maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, wakiongozwa na Naibu Kamishna wa Jeshi hilo, Kamishna Festo Sanga (wa kwanza kulia) wakati wa kikao maalum na uongozi wa Benki ya CRDB, uliotembelea Makao Makuu ya Magereza, jijini Dar es salaam leo.
“Ningependa kuona pia Benki ya CRDB kuwa mteja wa bidhaa na huduma zinazotolewa na Jeshi la Magereza mfano Benki kutumia samani za ofisi na Magereza kupewa Kandarasi za ujenzi wa miradi ya Benki inayodhaminiwa au kumilikiwa na Benki”, aliongezea Dokta Malewa akionyesha fursa ya kibiashara iliyopo baina ya Benki na Jeshi la Magereza.

Dokta Kimei alimhakikishia Mkuu wa Jeshi la Magereza kuwa Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana na Jeshi hilo katika miradi mbalimbali ambayo wamepanga kuitekeleza, huku akihaahidi kutuma timu ya wataalam kutoka Benki ya CRDB kufanya upembuzi yakinifu juu ya kuweka ATM na kufungua vito vya kutolea huduma katika maeneo ya Jeshi la Magereza ilikufikisha huduma kwa akari kwa urahisi.
Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa akieleza jambo kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Juma Malewa (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Magereza, jijini Dar es salaam leo.

“Matarajio yangu ni kuona uhusiano baina yetu ukikua zaidi, naihidi kuwa kupitia Wakurugenzi na Mameneja wetu wa matawi tutaweka utaratibu wa kutembelea ofisi za Magereza nchi nzima ili kuhakikisha haya tuliyokubaliana hapa yanatekelezwa”, alisema Dokta Kimei.

Mkutano huo ulimalizika kwa Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza kutengeneza kikosi kazi cha kufuatilia utekelezaji wa maazimio ambapo Kamishna Gaston Sanga Mkurugenzi wa Utawala, fedha na Rasimali watu wa Jeshi la Magereza alichaguliwa kuwa Mwenyekiti akisaidiwa na Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wakati wa Benki ya CRDB Bi. Jesica Nyachiro. Dokta Kimei pia alimuomba Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB Bi. Tully Mwambapa kuona namna ambavyo Benki ya CRDB itaweza kuunganisha shughuli zake za misaada kwa jamii na Jeshi la Magereza.


Katika mkutano huo Benki ya CRDB iliahidi kutoa msaada wa kompyuta na vitendea kazi vingine kwa Jeshi la Magereza ili kuongeza ufanisi wa Jeshi hilo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi April 2018, Benki ilikuwa pia imeshafungua zaidi ya Akaunti elfu tatu (3,000) za mishahara kwa askari wa Jeshi la Magereza.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei akizungumza.
Baadhi ya Maafisa wa Benki ya CRDB, wakiwa kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto) akimkabidhi zawadi maalum, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa, wakati alipomtembelea ofisini kwake, Makao Makuu wa Magereza, jijini Dar es salaam, Mei 23, 2018. Mkutano huo ulikuwa na lengo kudumisha uhusiano wa kibiashara baina ya Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza nchini.
Picha ya pamoja.

No comments: