Friday, June 27, 2008

IJUMAA SHOWBIZ!

Lile shindano kabambe la Ijumaa King of Hip Hop linalooendeshwa na gazeti hili, linaendelea kushika kasi huku washiriki wakianza kutambiana kuchukua ushindi.

ShowBiz ilipozungumza na baadhi ya wasanii wanaochuana katika kinyang'anyiro hicho, wengi walionyesha kujiamini na kuwa na usongo wa kuibuka kidedea.

"Najua hili ni shindano, na katika shindano kuna kushinda na kushindwa lakini kwa upande wangu najiamini lazima nichukue ushindi,"alisema mmoja wa washiriki hao aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

Msanii mwingine anayewania ushindi katika mtanange huo (jina tunalihifadhi) alipoulizwa na ShowBiz kuhusu shindano hilo alisema: "Kwakuwa mshindi anapatikana kwa njia ya kura, basi nafikiri tuwaachie wasomaji wenyewe ndiyo waamuzi, lakini nipo tayari kukubaliana na matokeo ya aina yoyote kwasababu najua ni maamuzi ya wapenzi wetu."

Akichonga na safu hii juzi, ofisini kwake, Sinza jijini Dar es Salaam, Mratibu wa shindano hilo, Charles Mateso alisema shindano hilo linaanza kushika kasi na amewataka wasomaji wetu waendelee kupiga kura nyingi kadri wawezavyo.

"Mambo ndiyo kwanza yanaanza kuchanganya, wasomaji wanapaswa kukumbuka kuwa, washindi ni wale watakaowachagua wenyewe, hivyo basi waendelee kupiga kura kwa wingi kumpigia mshiriki wanayedhani kuwa anastahili kuwa Ijumaa King of Hip Hop.

"Kwa mfano unataka kumpigia kura msanii ambaye unadhani anastahili kushinda. Andika neno HP (acha nafasi) kisha andika jina la msanii kwenda namba 15551 na hapo utakuwa umemuwezesha msanii unayependa kuwa Ijumaa King of Hip Hop," alisema Mateso.

Wakali wa Hip Hop wanaoshindanishwa katika shindano hilo ni Fid Q, Langa, Kala, Kalapina, Rado, Chid Benz, Joh Makini, Prof. Jay, Lord Eyes na Balck Rhyino.

Aidha, wasomaji watakaopiga kura nyingi zaidi watajiweka katika nafasi ya kujipatia zawadi kibao.

***********************************************

Mbasha kuwasha moto Dodoma!
Mkali wa Muziki wa Injili nchini anayekwenda kwa jina la Flora Mbasha, anatarajia kuzindua albamu yake mpya ya Furaha Yako keshokutwa (Jumapili) mjini Dodoma katika Uwanja wa Dodoma Stadium, mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Hamida Hassan anakuhabarisha.

Msanii huyo ambaye amejizolea umaarufu kutokana na albamu zake mbili za Unifiche na Jipe Moyo, alisema kwamba wakazi wa Dodoma watakuwa wa kwanza kushuhudia uzinduzi huo kabla ya mikoa mingine hivyo amewataka mashabiki wake wasikose bahati hiyo ya pekee.

"Hii ni zawadi ya pekee kwa mashabiki wangu wa Dodoma, ninawasihi wote waje wakutane na upako wa Bwana. Ni burudani inayoambatana na ujumbe utakaoimarisha imani za Wakristo, kwakweli ni shoo nzuri kuliko maelezo," alisema.
Amesema kuwa, mbali na ujio wa albamu hiyo pia anatarajia kutambulisha mtandao (website) wake ambao ni www.florambasha.com.
***********************************************

Juma Nature, Mheshimiwa Temba pamoja tena?
Kuna habari zinasema kwamba wasanii mahasimu wawili kutoka Makundi ya Muziki ya TMK Wanaume Family na TMK Wanaume Halisi, Juma Kassim 'Nature' na Amani Temba 'Mheshimiwa Temba' wapo mbioni kuungana pamoja na kuendeleza makamuzi kama zamani.

Mwana ShowBiz wetu, Shaban Rajabu amenyaka nyepesi hizo street ambapo washkaji wa karibu wa masela hao, wanadai kuwa wakali hao wa Bongo Fleva hivi sasa wapo karibu na mazungumzo ya chini chini kuhusu kufanya kazi pamoja tena yanaendelea.

Wanyetishaji walidai kwamba, hatua hiyo imekuja kufuatia jitihada kubwa za kuwapatanisha alizofanya Prodyuza maarufu nchini, Khalfan Peter a.k.a P-Funky a.k.a Majani au Kinywele Kimoja kutoka Studio za Bongo Records.

"P Funky anapaswa kupewa pongezi sana kwa kazi nzito aliyoifanya, lakini pamoja na Majani, Shindano la Nani Mkali limesaidia kwa kiasi kikubwa sana kuwaweka washkaji karibu," alipasha msela huyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake 'pepani'.

Katika hatua nyingine, kona hii iliwanasa masela hao wakipiga stori huku wakicheka na wakati mwingine kugongeana mikono, nje ya Studio za Bongo Records zilizopo Sinza-Bamaga jijini Dar es Salaam.

"Hawana bifu tena hawa jamaa, hata Temba alipokuwa katika mahojiano na Channel Ten, alisema anamzimia Nature kuliko msanii mwingine yeyote wa Bongo Fleva," aliongeza mpashaji wetu.

Prodyuza P-Funky anayedaiwa kuwa ndiye mpatanishaji mkuu wa wasanii hao, alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema: Wanakuja hapa na wanaongea vizuri tu, kifupi ni kwamba hawana bifu ila kuhusu kufanya kazi pamoja siwezi kulizungumzia, nadhani wenyewe ndiyo wenye majibu mazuri zaidi."

ShowBiz bado inaendelea kuwasaka wakali hao ili waweze kuzungumzia kuhusu ishu hiyo.
***********************************************
Kaole Kufunika A Town leo!
Kutoka Kundi la Sanaa la Kaole la jijini Dar es Salaam, Simon Simalenga a.k.a Dimera ambaye ndiye Katibu Mkuu anatudakisha kwamba, leo watafanya shoo ya nguvu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ikiwa ni onesho lao la kwanza kufanyika nje ya Dar es Salaam, baada ya kundi lao kuanzishwa.

"Watu waje waone mambo yetu, Kaole ya sasa siyo ile ya zamani, wasanii wamepikwa na wameiva vya kutosha. Sina mengi ya kuongea zaidi ya kuwataka wakazi wa A Town na vitongoji vyake waje waone mambo yetu ," alisema Dimera.

Aliongeza kusema kwamba kabla hawajaanza shoo, watacheza mechi ya mpira wa miguu kati yao na wasanii wa maigizo wa A Town, lengo likiwa ni kukuza vipaji vya wasanii wachanga wa Arusha na kuboresha uhusiano wa kisanii kati yao na Wadau wa Tasnia hiyo waliopo mikoani.

Haya kazi kwenu mashabiki wa A Town kutoka pande zote za Ngaramtoni, Majengo, Sakina, Mianzini, Soweto, USA River, Ngulelo na kwingineko nendeni mkawaone Kaole wakifanya mambo yao.

No comments: