Monday, June 30, 2008

WIKIENDA SHOWBIZ!

King of Hip Hop:
Wasipoangalia sura, mfalme wa kweli atapatikiana - Kalapina

Mkali wa Hip Hop Bongo, Karama Masoud a.k.a Kalapina kutoka Kikosi cha Mizinga, ameweka wazi msimamo wake kuhusu Shindano la Ijumaa King of Hip Hop, kwamba anayestahili kushinda ni yule aliye mwana Hip Hop halisi, Eunice Macha na Chausiku Omar, walicheki naye.

Akisema na safu hii hivi karibuni, Kalapina ambaye ni mmoja kati ya wasanii waliotajwa kuingia kunako mpambano huo alitamka kwamba iwapo usipofuatwa ushabiki na kutazama vigezo halisi ana kila sababu ya kushinda.

“Mimi naamini kabisa iwapo ikifuatwa misingi halisi ya nani ni mwana Hip Hop atapatikana mfalme wa kweli, ila mashabiki wakitazama sura hapo kutakuwa na tatizo.
“Ni vema pia kila msanii aliyechaguliwa kushiriki katika shindano hilo, angeandikiwa maelezo ya kutosha, ili mashabiki wajue amefanya nini na nini anachojua kuhusu muziki huo,” alisema .

Mratibu wa Shindano hilo, Charles Mateso amewataka wasomaji wa gazeti la Ijumaa kuendelea kuwapigia kura wana Hip Hop waliopendekezwa ili hatimaye siku ya mwisho apatikane mfalme halisi.

“Unachotakiwa kufanya ni kumpigia kura unayedhani anastahili kuwa mshindi, andika neno HP (acha nafasi) jina la msanii kisha tuma kwenda namba 15551.

Wana Hip Hop wanaowania taji hilo litakalokuwa na zawadi kubwa ni Kalapina, Fid Q, Rado, Chid Benz, Profesa Jay, Langa, Black Rhino, Joe Makini, Kala Jeremiah na Lord Eyez kutoka kundi la Nako2Nako.

Muvi ya Mama Devi kudondoshwa na Tollywood Filamu yenye jina la ‘Mama Devi’ ambayo inatarajiwa kufanya maajabu sokoni, itadondoka hivi karibuni kupitia kampuni mpya ya usambazaji wa muvi za Kibongo, Tollywood Movies iliyopo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa msemaji wa kampuni hiyo, Chris Magori, Tolywood sasa imekuja kufanya kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu na wadau wengi wa tasnia hiyo, yaani kuzalisha filamu na kuziingiza sokoni zikiwa katika VHS, DVD na VCD.
“Filamu ya Mama Devi inafundisha, inasisimua na kuburudisha ndiyo maana tumeamua kuanza nayo. Ndani yake wapenzi wa filamu nchini watashuhudia kisa cha mke wa mtu mmoja ambaye alipigwa risasi baada ya kufumwa na mume wa mtu, mbali na hilo yapo mengi ya kushangaza, kwa kifupi siyo picha ya kuikosa,” alisema Magori.
Kawa wasanii watakaohitaji kufanya kazi na Tollywood amewataka wafike ofisini kwao, Sinza Bamaga, Dar es Salaam ili waweze kupata maelezo kamili
************************************************.

Street Version:
Luteni Yusuf MakambaAlipofika, alipokelewa na maswali kutoka kwa wana habari
...alitaka kujua mengi zaidi kuhusu ajali hiyo na kutoa ushauri wake
...alipata maelezo kamili jinsi jengo lilivyodondoka..... Mkuu wa mkoa wa sasa, Abbas Kandoro alimpa maelezo zaidi kuhusu ajali hiyo ...unaona pale mzee.....eh!
Siku chache zilizopita kamera za ‘Street Version’ zilimbamba laivu Katibu Mkuu wa Chama Tawala (CCM), Luten Yusuf Makamba kunako mtaa wa Mtendeni na Zanaki, Dar es Salaam.
Kiongozi huyo ambaye aliwahi kuliongoza Jiji la Dar es Salaam (mkuu wa mkoa) alikutana na kamera hii alipokuwa katika ziara ya kushuhudia jengo la ghorofa kumi lililodondoka hivi karibuni na kusababisha mtu mmoja kufariki na wengine kujeruhiwa.

No comments: