Friday, June 25, 2010

IJUMAA SHOWBIZ!

Nakaaya
Wasanii na vyama vya upinzani: Sugu aandaliwa makubwa CHADEMA, Nakaaya ndani, Kalapina, Madee pia wamo

Ni exclusive lakini pia ni heavy weight scoop! Ijumaa Showbiz inakupa news kwamba The Bongo Hip Hop legend, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ muda si mrefu ataanza kutambulishwa kama mheshimiwa kwa sababu ameandaliwa mambo makubwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Sugu a.k.a Mr. II, jana alitarajiwa kuchukua kadi ya CHADEMA, hivyo kuwa mwanachama rasmi wa chama hicho ambacho kina dhamira ya dhati ya kumsimamisha kwenye jimbo moja (hatulitaji kwa sasa) katika Uchaguzi Mkuu ambao ratiba inaonesha utachukua nafasi yake Oktoba 31, 2010.

Ijumaa Showbiz linakupa ‘data’ zisizo na shaka kuwa CHADEMA kimefikia hatua hiyo ya kumsimamisha Sugu kugombea ubunge, baada ya kutembelea jimbo husika na kufanya utafiti ambao ulionesha kwamba galacha huyo mwenye rekodi ya kupigania haki bila woga, anakubalika kwa wapigakura ile mbaya.

Mmoja kati ya maofisa wa juu wa CHADEMA (jina tunaliminya), alisema nasi kwamba kila kitu kinawekwa sawa hatua kwa hatua.

“Tumekwishazungumza naye, tumemshawishi ajiunge na chama chetu, tumemueleza ni kwa kiasi gani anavyokubalika kwa wapigakura, pia tukamueleza umuhimu wa yeye kuwepo bungeni hasa katika kipindi hiki ambacho anatetea haki za wanamuziki,” alisema ofisa huyo wa CHADEMA na kuongeza:

“Tumempa katiba ya chama chetu apitie ili aone sera za CHADEMA za kumkomboa Mtanzania, baada ya hapo tumeandaa hafla ya kumkabidhi kadi kitakachofuata ni kutangaza nia na kuchukua fomu ambayo itarejeshwa kwa kishindo bungeni.”

Mmoja wa wabunge wa chama hicho (jina tunalo) alisema amefurahishwa mno na hatua ambayo wamefikia na Sugu na kuongeza kwamba mambo yakienda vizuri, watawasha moto wa nguvu kwenye jimbo ambalo ‘mchizi’ ameonekana anakubalika.
“Sugu! Nimefurahi sana, wewe subiri uone moto tutakaouasha. Ni patamu sana,” alisema mbunge huyo ambaye muda bado kumtaja waziwazi.

Mambo yakienda sawa kwa CHADEMA na Sugu, basi mwaka huu itaonekana kwamba wasanii wa muziki wa kizazi kipya watakuwa wameamua kuvamia upinzani.

Prezidaa wa Block 41, Kino, Karama Masoud ‘Kalapina’ tayari amekwishatangaza kwamba mwaka huu atagombea udiwani wa Kata ya Kinondoni kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) na staa wa Mr. Politician, Nakaaya Sumari yeye amedhamiria kuwania ubunge Viti Maalum (CHADEMA).

Msanii mwingine wa muziki wa kizazi kipya mwenye ndoto za kuwania Udiwani pande za kwao Manzese ni Hamad Ally a.k.a Madee lakini bado hajaweka wazi atasimama kwa tiketi ya chama gani.

Ukitaka kujua jimbo ambalo CHADEMA wanataka kumsimamisha Sugu na kauli yake mwenyewe, funua gazeti ndugu na hili, Ijumaa Wikienda Jumatatu.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Twanga: Kuendeleza sherehe Dom
Zikiwa zimesalia siku mbili Bendi ya African Stars a.k.a Twanga Pepeta idondokee kwenye sherehe kubwa za kutimiza miaka kumi tangu kuanzishwa kwake, ShowBiz imetupiwa ishu kwamba furaha hiyo itaendelea pia pande za Dodoma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka sherehe hizo zitakazoanzia ofisini kwao Kinondoni Studio na kumalizikia katika Viwanja vya Leaders, Dar es Salaam zitachukua nafasi Jumapili ya keshokutwa.

“Siku hiyo kutakuwa na burudani kibao na michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, mpira wa wavu na mingine, kabla vijana wa Twanga hawajapanda stejini. Baada ya Dar es Salaam tutaelekea Dodoma Julai 2, mwaka huu na kuendeleza sherehe hizo ndani ya Ukumbi wa Kilimani,” alisema Asha Baraka.
##############################
Afande aigonga bajeti ya nchi, awaokoa wabunge
Mfalme wa Mashairi ya Hip Hop, Suleiman Msindi ‘Afande Sele’ ameamua kutoa neno lake kuhusu wakati huu ambao bajeti ya nchi kwa mwaka wa fedha 2010/2011 imesomwa na vikao vya bunge vinaendelea.

Amewagonga nyundo wananchi kufuatilia vikao vya bunge ili kuelewa bajeti za wizara mbalimbali, pia akawakoa konzi la mbali wabunge wachache ambao wanakacha vikao vya bajeti na kuketi kuangalia mashindano ya Kombe la Dunia.

Katika SMS yake aliyoituma kwetu, Afande Sele alisema: “Kaka, pamoja na wa TZ wengi kuwa bize wakati huu wa mambo ya World Cup, ni vyema pia kama wakiwa bize katika kujua na kufuatilia Bunge wakati huu pia kwakuwa ndiyo wakati ambao Bunge limepitisha bajeti ya nchi.

“Na bila shaka bajeti ndiyo muhimu zaidi kwetu kwakuwa ndiyo mwamuzi wa maisha na hatma ya taifa letu masikini. Wale wenzetu wanaocheza World Cup wanatambua hilo katika nchi zao na ndiyo maana wamefanikiwa kufika pale na kushiriki mashindano yale.

“Michezo na burudani ni mambo ambayo yanamaanisha furaha na starehe katika maisha ya mtu. Na ili mtu afurahi na kustarehe anatakiwa awe ameshapata vitu vyote muhimu na vya msingi katika maisha kama kula kupata elimu, matibabu, kufanya kazi na hata kuvaa na kulala.

“Baada ya kufanikiwa katika vitu hivyo vya msingi ndipo mtu anapoweza kuburudika na kucheza, hivyo ndivyo maisha yalivyo na ndivyo wafanyavyo wenzetu wenye kujielewa. Ni aibu kusikia eti wabunge wetu wanakacha vikao muhimu vya bajeti ya nchi kwa ajili ya kuangalia World Cup.”
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
compiled by mc george/ijumaa newspaper

3 comments:

Unknown said...

hiyo bajeti kaka yangu vyovyote itakavyopangwa ndiyo hivyo hivyo hakuna atakayebadilisha, ndiyo maana watu wako busy na mambo yao usikilize usisikilize haibadiliki

Anonymous said...

Ndugu yangu Mrisho uliipata msg niliyokujibu kuhusu mtandao wenu wa Global kutokupatikana hewani huku ughaibuni.

Mrisho's Photography said...

nilipata lakini nashindwa kuelewa kama tatizo liko kwako ama kwetu..je umejaribu kuwauliza na wenzako mnaokaaa eneo moja kama nao hawapati? Tunavyoamini huku na watu wengine matandao wetu hauna tatizo na unaonekana sehemu zote...nitumie email: uwazi@hotmail.com