Monday, October 18, 2010

WIKIENDA SHOWBIZ!

Justin Bieber Umri mdogo, pesa nyingi, mambo makubwa
Kuna madogo wengi waliamka na kufanya kweli kisha kutengeneza pesa nyingi. Wakapewa heshima kwa ‘wandaz’ walizofanya. Wakawekwa kwenye kumbukumbu ya kudumu na ikaaminika hakuna anayeweza kufikia rekodi zao.

Bow Wow alipiga mzigo wa kufuru akiwa na miaka 14, Lil Romeo alitikisa, Jerome alipotoka na Your not too old for me alisumbua lakini Justin Bieber ni mwisho wa ubishi.

Mama yake, Pattie Mallette alibeba mimba yake akiwa na umri wa miaka 18. Akasimangwa, akaishi kwa manyanyaso kwa kipato duni, akatengwa na baba wa mtoto, kwahiyo hata alipomzaa Bieber alimlea katika mazingira magumu.

Unadhani mpaka leo kuna watu wanamcheka? Thubutu, mama anakula goodtime, anatumia gari analotaka, anakula anachotaka, anavaa anavyopenda, hajiulizi pesa ila kinachomfanya awaze ni jinsi ya kuzitumia. Hayo ni matunda ya kuzaa tunda jema, Bieber.

Ni dogo ‘flani’ ambaye hajipendi wala hajui kama yeye ni maarufu, hatambui kama anapesa zinazomfanya aitwe tajiri. Kutokana na hayo mara kwa mara huingia kwenye ‘kashkash’ ya kuwatoroka walinzi wake na kuzama ‘kitaa’.

“Anahitaji uhuru zaidi lakini sisi tumeajiriwa kumlinda yeye, tunakuwa makini muda wote kuhakikisha mambo hayaharibiki,” alinukuliwa mkuu wa walinzi wa Bieber, alipohojiwa na mapaparazi ni kwanini wanambana dogo huyo.

Bieber ndiye mwanamuziki anayetajwa kuwa na mashabiki wengi kuliko mwingine yeyote mtandaoni. Ukurasa wake wa Twiter unatajwa kuwa bize mno kutokana na jinsi mashabiki mbalimbali duniani wanavyochungulia.

Kutokana na hilo, menejimenti ya Twiter imekuwa ikifikiria jinsi ya kutoa huduma maalum kwa ajili ya ukurasa wa Bieber ili kuondoa usumbufu uliopo kwa sababu idadi ya watu wanaomtembelea ni kubwa kuliko uwezo uliopo.

Idadi ya mashabiki aliyonayo mtandaoni, imewatisha mpaka mastaa wakubwa Marekani kama 50 Cent na Kanye West ambao kwa nyakati tofauti wamemtembelea Twiter na kujionea jinsi dogo huyo alivyo lulu ya wana wa ulimwengu wa sasa.

MAFANIKIO SAWA ILA HAJITAMBUI
Tatizo kubwa ambalo linamsumbua Bieber ni utoto. Anapenda kuishi kama watoto wengine. Umaarufu na pesa anazoingiza kila siku kupitia muziki, havimfanyi ajione yupo ‘levo’ nyingine.

Moja ya matukio ya kuchekesha lilitokea hivi karibuni nchini Canada. Baada ya kufanya shoo jukwaani, Bieber aliwachenga walinzi wake na kuingia mtaani ambako alinunua ice cream na kuilamba kwa fujo.

Alipotaka kugeuza arudi, kuna mijibaba ilimuona na kugundua ni Bieber, kwahiyo ‘wakamtait’ na kumueleza kwamba kisingeeleweka endapo angetaka kuondoka bila kuwaimbia.

Dogo akawauliza kumbe mnataka hilo tu? Akawaambia ‘waskonde’, akaanza kutoa burudani na kujaza umati mkubwa. Kule ukumbini walinzi baada ya kumtafuta sana, wakaamua kuingia mtaani ambapo walimkuta akiwa bize anatoa shoo nyingine tena ya bure mtaani.

Walinzi walipotaka kumchukua, akawajibu wamuache kwanza kwa sababu wale ni mashabiki wake, waliohitaji huduma yake.

ALIPOTOKA
Alizaliwa Machi Mosi, 1994, London, Ontario, Canada na kukulia Stratford, Ontario. Pamoja na kwamba baba yake, Jeremy Bieber alimtosa mama yake, hivyo kumfanya akue kwa tabu lakini anawasiliana naye na kumpa heshima kama mzazi.

Bieber alionesha dalili za kuwa mwanamuziki alipojifunza kucheza piano, drums, guitar na trumpet. Alipokuwa na miaka 12, aliimba wimbo wa Ne-Yo ‘So Sick’ katika mashindano ya kuimba mjini Stratford na kushika nafasi ya pili.

Mama yake, Mallette ‘alipost’ YouTube video ya Bieber akiwa anaimba kwenye shindano hilo kwa ajili ya kuwaonesha ndugu na marafiki. Aliendelea kutumbukiza video za Bieber akiwa anaimba nyimbo mbalimbali za R&B.

KIPAJI CHAKE KILIVYOGUNDULIWA
Scooter Braun, aliye Afisa Masoko Mtendaji wa zamani wa Studio ya So So Def, akiwa mtandaoni anatafuta video za wanamuziki mbalimbali, kama ajali alikutana na moja ya video za Bieber za mwaka 2007.

Braun alivutiwa na video hiyo ambayo pia ilitoa maelekezo ya mahali anaposoma Bieber. Alimfuatilia na mwisho kabisa alikutana na mama wa mtoto huyo.

Mallette (mama wa Bieber) hakuwa na imani ya moja kwa moja kwamba mwanaye atachukuliwa na Braun kisha kubaki salama, kwahiyo kwa sababu na mafanikio ya mtoto wake kimuziki aliyataka, alimruhusu lakini hakuacha kumuomba Mungu.

“Mungu, namuweka kwako. Uniletee Mkristo safi na afanye kazi kwenye lebo ya Kikristo,” aliomba Mallette.


Bieber akiwa na miaka 13, alipaa na Braun hadi Atlanta, Georgia na kurekodi demo tapes kadhaa. Wiki moja baadaye, aliimba mbele ya Usher Rymond na alipovutiwa, walimsainisha mkataba katika Kampuni ya Raymond Braun Media Group (RBMG) ambayo ni muungano wa Braun na Usher.

Justin Timberlake anatajwa pia kumfukuzia Bieber lakini alikuta Usher amemuwahi. Mwaka 2008 alipelekwa Studio ya Island Records ambako alianza kufyatua mawe. Hapo ikabidi na mama mtu ahamie Atlanta kuanza kufaidi matunda ya kipaji cha mwanaye.

AMEVUNJA REKODI YA STEVIE WONDER
Mafanikio ya albamu yake ya kwanza yamemfanya avunje rekodi ya Stevie Wonder ya kuwa msanii mdogo wa kiume kuliko wote kushika nafasi ya kwanza katika chati za US Billboard 200.

Stevie Wonder aliweka rekodi hiyo mwaka 1963 na mwaka 2009, yaani miaka 46 baadaye, Bieber amemjibu mkongwe huyo.

Mafanikio mengine ya albamu yake ya kwanza ni kutoa nyimbo saba ambazo zote ziliingia chati mbalimbali, hivyo kuweka rekoki ya aina yake.
Albamu yake iliuza platinum kwenye nchi mbalimbali, ingawa kuna maeneo alifikia mauzo ya dhahabu mpaka fedha.

Nyimbo kama One Time, My World, One Less Lonely Girl, Love Me, Favorite Girl na nyinginezo ni kati ya mawe ambayo yanampaisha dogo huyo kwa sasa.

Moja ya matukio makubwa na yenye heshima kwa Bieber ni kuimba wimbo wa Stevie Wonder Someday at Christmas kwa ajili ya Rais wa Marekani, Barack Obama na mkewe Michelle Obama kwenye Ikulu ya nchi hiyo, iliyopo Washington.


ANAJIANDAA NA MRADI MPYA
Dogo akiwa amebalehe sasa na sauti yake ikiwa imekomaa kiasi, ameanza kurekodi albamu yake ya pili. Dr. Dre anatajwa kuwemo kwenye timu ya watayarishaji wa nyimbo mpya za Bieber.


Ana umri wa miaka 16 lakini katika mapenzi yupo sawa, kwani tayari imethibitika kwamba ametoka kimapenzi na wanawake wawili.

Alianza mapenzi akiwa na miaka 13, kwani inaonesha kwamba mwaka 2007, alianza kutoka na Caitlin Beadles ingawa mwaka 2008 waliachana.
Mwaka huu, aliangukia kwa Jasmine Villegas ambaye yupo naye mpaka sasa.
**************************************

Msanii Kanumba (kulia) akibadilishana mawazo na mwongozaji wa filamu ya Ping Pong Matthias (kushoto) wakati wa uzinduzi wa European Festival 2010 katika New World Cinema wikiendi iliyopita
Msanii Sajuki na mkewe Wastara nao walikuwepo
Tayana akiongea na Director wa movie ya Ping Pond kutoka Ujerumani.
****************************************
Tayanaa alewa chakari, aporwa simuPrizenta Tayana Amri aliona chungu ya kuutwika na kuwa chakari, pale alipoibiwa simu yake ya mkononi Alhamisi iliyopita, New World Cinema, Mwenge, Dar es Salaam.
Mchongo mzima unasomeka kuwa Tayana akiwa mmoja wa wahusika wakuu wa ishu ya Filamu za Bara la Ulaya, baadaye aliamua kujitwika maji makali a.k.a tingas mpaka akawa ziii!

Kipindi ‘flani’ akaonekana akiwa anapiga misele ukumbini akiwa peku, wakati uso wake na jinsi alivyotembea haikuwa kazi kugundua kwamba kichwani alishajitwika glasi za kutosha.

Akiwa anatangatanga ukumbini, ‘Vuvuzela’ wa safu hii akamuuliza kulikoni? Mdada akajibu: “Jamani nimeibiwa simu yangu, Nokia Xpress Radio.”

Vuvuzela likarusha swali la pili, mbona peku? Akajibu: “Viatu vinanizingua, nimeviacha kwenye gari.” Imeandikwa na Richard Bukos,Hemed Kisanda.
*************************

Barnaba agonganisha mademu, watwangana
Fundi wa mashairi ya mapenzi aliye zao la Taasisi ya Tanzania House of Talent (THT), Barnaba Jumatano iliyopita jioni, aligonganisha mademu ambao walitwangana.

Mtiti huo ulitokea eneo la Sayansi, Kijitonyama, Dar baada ya demu wa zamani wa Barnaba anayetajwa kwa jina moja la Lulu, kukivaa chombo kipya cha staa huyo wa kibao cha Njiapanda.

Sosi wetu wa awali alipasha kuwa Barnaba alipita mitaa ya Sayansi na kitu chake kipya, hivyo kile cha zamani kikashuhudia, kwahiyo kikanyanyuka na kumkwida mwanamuziki huyo, haijatosha mademu watupu wakaanzishiana kubwa.

‘Vuvuzela’ wa safu hii alipofika eneo la tukio, alikuta ugomvi unamalizika na Lulu amekwishatimua lakini haina maana tulikosa kauli ya mwanamuziki huyo.


“Tumeachana na Lulu long time lakini amekuwa akinifuatafuata sifahamu ananitafuta nini? Nilikuwa katika moja ya mishemishe zangu hivyo nashangaa aliamua kumuanzishia demu wangu mambo ambayo sijayapenda kiukweli,” alisema Barnaba huku akiingia kwenye gari na kutoweka na kitu chake kipya.

compiled by mc george/ijumaa wikienda

No comments: