Monday, November 22, 2010

JUKWAA LA SANAA LAPITISHA KIAPO NA AGANO WA PARAPANDA

Mwanamitindo maarufu nchini Lisa Jensen akiwasilisha mada kuhusu ‘Fursa ya Wasanii Katika Fani ya Matangazo’ kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii.Wengine kutoka kushoto ni Mratibu wa Jukwaa Ruyembe Mulimba na Mkurugenzi wa Parapanda,Mgunga Mwamnyenyelwa.
Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa la Parapanda,Mgunga Mwamnyenyelwa akizungumzia wimbo wa Kiapo na Ahadi uliozinduliwa na kundi lake kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii.Kulia kwake ni Lisa Jensen na Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego.

Kundi zima la Parapanda likiutambulisha rasmi wimbo wa Kiapo na Agano kwenye Jukwaa la Sanaa.Wimbo huo ni mkali na uliwavutia wadau wa sanaa.

Kundi la Muziki wa asili nchini la Parapanda Jumatatu hii kupitia Jukwaa la Sanaa limezindua wimbo wake mpya wa Kiapo na Agano unaolenga kuwabana wanasiasa walioahidi ahadi mbalimbali wakati wa kampeni za uchaguzi kuzitekeleza kwa vitendo na kumaliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa wimbo huo ambao umebeba ujumbe mzito kwa wanasiasa, Mkurugenzi wa kundi hilo,Mgunga Mwamnyenyelwa alisema kwamba, wimbo huo ambao una ushairi ndani yake unalenga kuwakumbusha wanasiasa kwamba ahadi zilizoahidiwa ni agano baina yao na wanachi hivyo hawapaswi kuwahadaa na kuwalisha maneno matupu bali wanachotakiwa kufanya ni kuhimiza, kusimamia na kuwaletea maendeleo ya kweli bila kujali tofauti zao.

“Kila aliyekuwa akiomba kura alikuwa akiingia agano na wananchi hivyo, wimbo huu unasisitiza kwamba, miaka mitano ijayo kuna wananchi wametoka jasho na machozi katika kuwaingiza madarakani watataka waone wanatekelezewa ahadi zote” alisisitiza Mgunga.


Naye Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego mbali na kuwapongeza wasanii waliopata nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa mwaka huu, aliwataka wasanii kuwa mstari wa mbele kuwabana wanasiasa juu ya ahadi mbalimbali walizoahidiwa ili wasiwe ni wa kutumika tu wakati wa chaguzi kisha kubaki na shida zao.

“Wasanii tumeshiriki sana kuwaingiza wanasiasa bungeni lakini turudi nyuma na tuanze kufanya tathimini ya kina na kuwafuatilia ni kwa kiasi gani wanatekeleza yake waliyotuahidi.Tusipofanya hivyo tutakuwa tunajisaliti wenyewe,Parapanda wameanza nawapongeza kwa hili” aliongea kwa msisitizo Materego.

Awali,Mwanamitindo maarufu nchini,Lisa Jensen aliwasilisha mada yake kususu ‘Fursa ya Wasanii Katika Fani ya Matangazo’ ambapo aliwaasa wasanii kuwa na maadili bora, kuingia darasani na kusaka fursa mbalimbali ili kujenga uwanja mpana zaidi katika uelewa wa mambo na kuwa na fani zaidi ya moja katika kusaka mafanikio kisanaa.


Alisisitiza kwamba, tasnia ya mitindo inaweza kutoa ajira kubwa zaidi kwa wasanii kama wadau wataamka, wakajituma, kusaka wigo mpana wa uelewa wa mambo na kuichukulia sanaa kama kazi ya kuwapa kipato na maisha kwa ujumla.Katika hili alisema kwamba, lazima wasanii wahame kutoka kwenye dhana ya kutegemea makampuni ya watu na badala yake wajenge umoja imara na kuwa na ushirika ambao utawasaidia katika kujiendesha wenyewe badala ya kuwa tegemezi.

Jukwaa la sanaa litaendelea tena Jumatatu ijayo Tarehe 29/11/2010 ambapo muasisi wa blog nchini ambaye ni mmiliki wa blogu maarufu ya jamii Issa Michuzi atawasilisha mada kuhusu Mchango wa Blogs katika kukuza Sanaa..

No comments: