Tuesday, September 18, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT!


Zijue faida za kufunga kiafya

Inajulikana kidini kwamba mtu akifunga anapata thawabu, hilo halina mjadala na pengine waumini wa dini zote, hufunga ili kupata thawabu kwa Mwenyezi Mungu. Lakini tunapaswa kujua kwamba kufunga kuna faida kubwa kiafya na pengine Mungu alituamrisha kufunga siyo tu tupate thawabu, bali pia tuboresha afya zetu.

Katika makala haya, tutazungumzia faida za kufunga kiafya kama vile ambavyo zimethibitishwa na wanafasayansi mbalimbali duniani waliofanyia utafiti suala hili. Baadhi ya watu wanaamini kufunga kuna faida kiroho zaidi kuliko kimwili, kwani kwa mtizamo wa kawaida, mwezi mtukufu wa Ramadhani unapoingia kama hivi, Waislamu dunaiani kote hufunga ili kutekeleza moja kati ya nguzo tano za Uislamu. Halikadhalika kwa Wakristu, hufunga Kwaresma kama ibada.

KUFUNGA NI NINI?

Kufunga kuko kwa aina mbili. Kuna kufunga bila kula wala kunywa kitu chochote kwa muda usiopungua saa 12 (kama wafanyaavyo waislamu) na kuna kufunga kwa kunywa maji au juisi tu kwa muda usiopungua saa 12, kwa siku 30 hadi 40. kisayansi, kufunga kunahesabika pale wanga na mafuta ya ziada yaliyohifadhiwa mwilini yanapooanza kutumika kama chanzo cha nishati. Mtu huanza kusikia njaa pale hifadhi yake ya protini mwilini inapoanza kutumika kwa nishati.

Faida za kufunga zitaanza kujitokeza wakati mwili utakapokosa nishati mpya na kulazimika kuanza kutumia vyanzo vyake vingine vya nishati vilivyomo ndani ya mwili.

Vyanzo vikuu vinakuwa ni yale mafuta ya ziada yaliyojaa mwilini ambayo huchangia mtu kuongezeka unene na kadri utakavyokula kidogo ndivyo yatakavyotumika mafuta hayo.

FUNGA NA UONDOAJI WA SUMU MWILINI

Kama kuna faida kubwa inayopatikana kutokana na kufunga, ambayo hutetewa na wanaozijua faida za kufunga kiafya, ni hii ya kuondoa sumu mwilini, kitaalamu inajulikana kama 'Detoxification'. Hii ni njia ya kawaida ya mwili kuondoa uchafu na sumu mwilini kupitia utumbo mkubwa, figo, ini, mapafu na ngozi. Njia hii inapofanya kazi yake vizuri, humuepusha binadamu na maradhi mbalimbali.

Kwa mujibu wa wanasayansi, njia hii ya mwili kuondoa sumu yenyewe, huimarika pale mwili unapokuwa na njaa, kwa sababu chakula kinapokuwa hakiingii, mwili hukumbilia kwenye akiba ya mafuta kujipatia nishati ya kujiendesha. Akiba hii ya mafuta hujitengeneza yenyewe pale wanga na sukari ya ziada inapoacha kutumika kama nishati na kushindwa kutolewa kwa njia ya kinyesi, hivyo kubadilishwa na kuwa mafuta.

Hivyo basi, wakati mafuta hayo yanapotumika kama chanzo mbadala cha nishati wakati wa funga, hutoa kemikali fulani zinazojulikana kama 'fatty acids' ambazo huingia kwenye mfumo wa damu na kutoa sumu kwa njia ya viungo tulivyovitaja hapo juu. Sumu inayotolewa mwilini wakati wa funga siyo lazima iwe iliiingia kwa njia ya chakula, bali hata kwa njia ya hewa kutokana na mazingira tunayoishi.

FAIDA NYINGINE ZA KUFUNGA

Faida nyingine za kufunga ni ule uwezo wa kuponya magonjwa mengi. Kwa kawaida, wakati wa kufunga, nishati inayopatikana mwilini huwa haitumikia kwenye mfumo wa usagaji chakula, bali huelekezwa zaidi kwenye mfumo wa kinga na uvunjajivunjaji (metabolism), hivyo magonjwa ya mwili, kama vile uvimbe, na mengine, hukosa sapoti ya nishati na kufa yenyewe.

Aidha, wakati wa funga tunaelezwa kuwa, uzalishaji wa protini mwilini huongezeka wenyewe kutokana na makosa yanayofanyika na vidhibiti vya DNA/RNA. Protini inapokuwa nyingi mwilini, seli, tishu na viungo huwa na afya bora. Ndiyo maana, mnyama kama ng'ombe, anapopata jeraha, huacha kula na binadamu hukosa njaa pale anapoumwa mafua na tonsi. Hivyo mtu anapofunga, nishati iliyopo mwilini huelekeza nguvu zake kwenye kuimarisha mfumo wa kinga badala ya mfumo wa usagaji chakula.

FUNGA HUONGEZA UMRI WA KUISHI

Mwisho, faida nyingine muhimu ya funga iliyothibitishwa kisayansi, ni kujenga afya ya mwili na kuongeza umri wa kuishi. Hali hii huchangiwa na kupungua kwa kasi ya uvunjaji kemikali (metabolism), kuongezeka kwa uzalishaji wa protini, kuimarika kwa kinga ya mwili na kuongezeka kwa uzalishaji wa homoni za ukuaji wa mwili na zinazozuia kuzeeka (anti-aging hormones).

Kwa kumalizia, inaonekana kuna sababu nyingi za kiafya za mtu kufunga, ukiacha zile za kiroho. Kwa ujumla, funga huwezesha kuondoa sumu mwilini ambazo zimerundikana kwa miaka mingi. Funga huwezesha mwili kujiponya wenyewe na kukarabati seli na tishu zilizopata majeraha na mwisho kabisa, kuna ushahidi wa kutosha funga huongeza umri wa kuishi.

Ili kupata faida hizo, unatakiwa kuzingatia kanuni za ulaji sahihi wakati wa kufungua, usile kupita kiasi, usile vyakula vingi vya mafuta, pendelea kula vyakula vya asili, matunda kwa wingi na mboga za majani. Usile ili kulipizia siku nzima ambayo umeshinda na njaa. Staili hiyo ya maisha haiwezi kukuonesha faida za funga. Tuonane tena wiki ijayo.

No comments: