Saturday, January 18, 2014

MAPENDEKEZO 9 YA JINSI YA KUCHAGUA JINA LA KUTUMIA KAMA MSANII

Kama mwandishi na mmiliki wa blog kama hii ya BC [mahali ambapo vipaji huibuliwa na majina kutambulishwa] mojawapo ya majukumu yangu ya kawaida kila siku au kila wiki ni pamoja na kupokea kazi mbalimbali za wasanii. Mara nyingi,kazi hizo zinakuwa bado hazijasikika katika masikio ya wapenzi na mashabiki wa muziki. Hivyo basi,ni jukumu langu pia kuzisikiliza nyimbo hizo, kuzifafanua na kuzielewa ili kupata maudhui yanayofaa katika kuitambulisha nyimbo na msanii mwenyewe.

Kuna wanaochipukia na kuna wanaoanza safari ndefu ya kuelekea kwenye umaarufu au kujikimu na maisha. Kuna wanaokuwa wanarejea baada ya mapumziko na tafakuri na kuna ambao wanakuwa wameogopa kwamba wanaanza kusahauliwa na hivyo wanajifaragua kurejea kilingeni.

Hivi sasa, kila jua linapozama,maelfu ya vijana wanajisogeza vitandani mwao kupumzisha mwili na akili huku ndoto zao zikilenga kwenye “kutoka” kwa maana ya kuwa msanii superstar ajaye. Kazi ya kuwaza ni kazi.Kazi ya kufanya kinachotakiwa kufanyika ili kutimiza lengo au malengo ni kazi zaidi.

Sanaa inalipa. Sanaa ni kazi. Sina takwimu halisi lakini bila shaka tunakubaliana kwamba sanaa inatoa ajira kwa maelfu [kama sio mamilioni] ya vijana nchini mwetu.Na ni kweli kwamba ingelipa zaidi endapo taratibu na sheria mbalimbali [ambazo zipo] zingetumika vyema. Kuna wanaofaidi Jasho la hawa vijana na ndio maana kuna “mgando” katika utekelezaji wa sheria hizo. Hii ni mada ambayo natumaini kuifanyia kazi zaidi katika siku za usoni.


Leo ninachotaka kuzungumzia ni jinsi ya kuchagua jina la kutumia kama msanii[ stage name]. Kwa mzaha unaweza usione umuhimu wa kupasua kichwa kwamba utoke na jina gani au jinsi gani jina unalotumia hivi sasa linaathiri soko au masoko ya kazi zako na maendeleo yako kwa ujumla kama msanii. Lakini endapo utatumia muda kidogo na kutizama majina japo 10 tu ya wasanii unaowajua au unaovutiwa na kazi zao ndani na nje ya Tanzania,utagundua kwamba, umakini unaohitajika katika kazi nzima ya sanaa[ ubunifu,umaridadi,hadhira, ujumbe nk] inahitajika pia katika zoezi la kuchagua jina.

Kabla hata ya watu kusikia kazi yako,watasikia jina kwanza. Mtangazaji wa redio, televisheni au hata mwandishi wa makala ya burudani gazetini au kwenye blog nk atasema leo tunamtambulisha fulani bin fulani ambaye ni msanii mpya. Jina la wimbo wake ni … Tayari utaona kwamba jina linaanza na hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuzingatia unatumia jina gani.

Bila shaka wewe msomaji,shabiki wa muziki,mtangazaji wa radio au televisheni utakubaliana nami kwamba jina la msanii linahusika [the name matters]. Yapo majina ambayo ukiyasikia unashikwa na tamaa ya kuisikia kazi yake. Kama kazi yake itakuwa sio nzuri kwa kiwango ulichotarajia, hilo ni suala jingine ila amini usiamini,jina unalojipa lina nafasi kubwa sana katika aina ya kazi za sanaa utakazokuwa unazitoa. Wanasaikolojia wanakubaliana katika hili pia.

Ninapopokea kazi za wasanii[ hususani wale wapya kabisa ambao ndio kwanza wanataka “kutoka”] huwa natizama kwa makini kazi yake nikianza na jina analotumia yeye kama msanii na hata jina la wimbo. Ninapoona msanii amechagua kujiita “Bullet Hunter au Idiot Sucker au Mtambo wa Gongo” nk huwa naanza kushikwa na simanzi. Kwa bahati mbaya mara nyingi imekuwa ikitokea kwamba Bullet Hunter na kazi yake huwa imekaa kama bullet[risasi] zina mlio lakini zinaweza kuelekezwa kokote na kuua yeyote aliyepo mbele. Mifano ya majina ya kisanii yenye kuleta au kujenga taswira “fulani” kabla hata ya kusikia kazi ya msanii ni mingi. Sitaki kupoteza muda wako msomaji wangu kwa kukupa mifano laki zaidi.

Jina unalolichagua ndilo litakalotumika kukutambulisha wewe kama msanii na kazi zako. Wenzetu wanasema ndio “brand” yako. Mtu akitaka kuelewa kazi zako kwa kutizama na kutafsiri jina lako tu atapata majibu gani?

Hizi hapa ni mbinu zinazoweza kumsaidia msanii kuchagua jina la kisanii [stage name]

  • Unaweza kutumia jina lako…Lakini: Bahati nzuri kabisa ni kwamba baadhi ya wasanii hawahitaji kuongeza wala kupunguza kitu kutoka kwenye majina yao. Wanaweza au unaweza kutumia jina lako kamili na likakubalika. Mifano ya wasanii wa namna hiyo wapo wengi. Lakini kama utakavyoona katika dondoo zinazofuatia hapa chini, ni muhimu kuhahakisha kwamba vigezo hivi umevizingatia au kuviangalia kwa makini zaidi.

  • Chagua Jina Unalolipenda: Mifano ya watu ambao walipozaliwa wazazi wao waliwapa majina fulani na baadae kidogo tu walipojielewa wakagundua kwamba hawayapendi  kabisa majina yao na kuamua kuyabadili ipo mingi sana.Katika karne hii hutaki kupitia hayo. Chagua jina ambalo unalipenda na hutolionea soni kuliitikia. Hii ni pamoja na jina lako kama msanii [stage name]. Hutaki kujipa jina ambalo baada ya muda mfupi ukisikia MC analitaja unataka kujificha badala ya kuwa na shauku ya kulivamia jukwaa.

  • Liwe Rahisi Kutamkika: Unapochagua jina hakikisha  kwamba linakuwa rahisi kutamkika. Hapa ni muhimu kuzingatia kwamba ndoto yako [ na ya kila msanii] ni kuuza kazi zake kwa mataifa mbalimbali na watu wa asili mbalimbali. Je,mchina ataweza kutamka jina lako kirahisi? Mzungu wa Amerika je? Vipi Mhindi kutoka Mumbai? Kwa bahati mbaya, watu wengi wanaposhindwa kulitamka jina lako wanakata tamaa pia kuwaambia marafiki zao kuhusu “yule msanii ambaye jina lake siwezi kulitamka”. Unakosa masoko.Unapoteza fursa ya kuongeza mashabiki.

  • Liwe Rahisi Kukariri au Kukumbukwa: Unapochagua jina hakikisha kwamba ni rahisi kukumbukwa. Mara nyingi hili huenda sambamba na kuchagua jina fupi[mara nyingi moja]. Japokuwa wapo wasanii au wanamuziki mbalimbali maarufu ambao walitumia majina yote mawili na yakakamata [mfano Michael Jackson] lakini kumbuka kwamba majina yote [Michael na Jackson] ni mepesi kukumbuka na pia marahisi kutamkika. Unapokuwa na jina rahisi kukumbukwa na mashabiki na wapenzi wa muziki inavutia zaidi na inapanua kirahisi zaidi wigo wako wa biashara.

  • Linauzika?: Ushawahi kusikia jina la msanii fulani ambalo hapo kwenu linamaanisha tusi baya kabisa? Eeenh, nadhani umenielewa. Siku hizi ni rahisi kutizama maana ya jina lako katika lugha mbalimbali ulimwenguni. Google inatoa msaada huo kupitia ukurasa wake wa masuala ya ukalimani.


  • Tumia jina moja tu badala ya mawili: Hii inaendana na hiyo hapo juu. Badala ya kutumia majina yako yote mawili jaribu kutumia au kuchukua jina moja. Jina hilo moja linaweza kuwa jina lako la mwanzo, kati au mwisho[mara nyingi la baba]. Mfano wa wasanii maarufu ambao waliamua kutumia majina yao ya mwanzo tu na kuachana na mengine ni Rihanna[ alipozaliwa alipewa jina  Robyn Rihanna Fenty], Beyonce [jina lake ni Beyoncé Giselle Knowles] au Madonna [ aliitwa Madonna Louise Ciccone]


  • Unaweza kutumia Namba au Alama: Ingawa unahitaji kuwa makini zaidi unapoamua kutumia namba kwenye jina lako la kisanii, unapoamua kutumia jina lenye namba hakikisha kwamba linakuwa na maana au linaendana kwa karibu na kitu au vitu vinavyohusiana na maisha yako. Hivyo vinaweza kuwa jina la mtaa[maarufu ulipokulia] au hata nchi kwa mfano [#255 ambayo ni code ya miito ya simu ya kimataifa kwa Tanzania]. Baadhi ya wasanii maarufu ambao waliongeza au kuweka namba kwenye majina yao ni kama vile marehemu 2Pac[ jina lake ni Tupac Amaru Shakur] E-40 [ jina lake Earl Stevens) au Ke$ha ( alipozaliwa wazazi walimpa jina Kesha Rose Sebert)

  • Unaweza kutumia jina la utani: Wengi wetu tulipokuwa watoto au mashuleni tulipachikwa majina ya utani. Nakumbuka mimi wenzangu shuleni waliniita CheGu. Nilikuja kuelewa baadae kwamba jina hilo lilitokana na misimamo yangu.Wakaona wanifananishe na Che Guevara[ mpigania haki za binadamu na uhuru aliyezaliwa Argentina na baada kupigana bega kwa bega na Fidel Castro kusaka utawala wa watu nchini Cuba na baadae Congo nk]. Nilichukia kuitwa CheGu. Leo hii nikiangalia nyuma na baada ya kuelewa maisha ya Che Guevara, nisingechukia na si ajabu ningekuwa msanii ningejiita jina hilo.Kwa upande wako unaweza pia kutumia jina ambalo ulikuwa unaitwa mtaani au shuleni kama utani. Lakini hakikisha masuala hayo hapo juu yanahusika.

  • Lipo Au Lishachukuliwa Kwenye Mitandao Ya Kijamii?: Mwisho dunia ya leo imebadilika. Hata kusema imekuwa kama kijiji nahisi kuna mapungufu. Unapojiandaa kujipa jina ni vizuri kuhakikisha pia kwamba jina unalojipa unaweza pia kulitumia katika mitandao ya kijamii kwani mitandao hii [upende au usipende] ipo nasi sasa na muda mrefu ujao.

Kumbuka kwamba jina [ambayo itabeba brand yako nzima] ndio itatumika katika masuala yote ya kujitangaza au kutafuta masoko ya kazi zako. Ni vigumu kufanya branding awareness bila kushirikisha mitandao ya kijamii. Kwa hiyo basi, ni vyema kuchunguza kwanza kama jina unalotaka kutumia bado linapatikana au limeshachukuliwa. Kama limeshachukuliwa achana nalo.Pia labda niongeze kwamba wakati huu huu wa kutafuta jina ni muhimu pia kuangalia upatikanaji wa vitu kama anuani ya tovuti yako nk.

Jeff Msangi ni mwandishi,mwendeshaji mkuu wa mtandao wa BongoCelebrity.com na mdau wa karibu wa masuala ya burudani na muziki. Unaweza kuwasiliana naye kupitia jeffmsangi at gmail dot com.

No comments: