Tuesday, October 14, 2008

VIJUE VYAKULA VINAVYOZUIA KUZEEKA!


Umeshawahi kukutana na rafiki yako wa siku nyingi na ukamshangaa jinsi alivyozeeka japo ki umri mko sawa? “jamaa mbona anazeeka hivi”? ni swali ambalo pia utakuwa umeshawahi kulisikia. Hali hii kilishe ina sababu ambazo leo katika makala haya tutajifunza jinsi ya kula vyakula vinavyoweza kukufanya uonekane kijana siku zote.

Katika toleo lake la hivi karibuni, jarida linalojishughulisha na uandishi wa habari mbalimbali za masuala ya lishe, Eating Well Magazine, limetoa matokeo ya utafiti mbalimbali wa vyakula vinavyochelewesha kasi ya mtu kuzeeka haraka, (anti aging foods) kama ifuatavyo:

CHOKOLETI
Katika kisiwa kimoja cha San Blas kilichopo Panama Marekani ya Kusini, kuna jamii moja ya watu wa Kuna ambao hawana matatizo ya magonjwa ya moyo ukilinganisha na wenzao wa Panama upande wa bara ambao wanasumbuliwa na maradhi ya moyo mara tisa zaidi ya wenzao!

Sababu ya jamii moja kuwa salama kiasi hicho ni kutokana na kupenda sana kunywa kwa wingi vinywaji vitokanavyo na zao la kakao (cocoa) ambalo lina kiwango kikubwa cha kirutubisho aina ‘flavanols’ ambacho kina uwezo wa kuimarisha utendaji kazi wa mishipa ya damu (blood vessels). Inaelezwa kuwa uimarishaji wa mishipa ya damu, hupunguza hatari ya mtu kupatwa na ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya figo na magonjwa ya akili.

SAMAKI
Miaka 30 iliyopita, watafiti wa masuala ya lishe na magonjwa, walianza kufanya utafiti wa kujua kwa nini jamii ya watu wa Inuits waliyoko Alaska walikuwa hawasumbuliwi na ugonjwa wa moyo kabisa. Katika utafiti wao, walikuja kugundua kuwa jamii hiyo inakula idadi kubwa sana ya samaki ambao wana kirutubisho cha ‘Omega-3’ kinachozuia kujijenga kwa kolestro mwilini na kuimarisha mapigo ya moyo kuwa sawa.

KARANGA
Utafiti uliowahi kufanywa na madhehebu ya Wasabato, ambao husisitiza ulaji unaozingatia afya na lishe ya mboga za majani (vegetarian), unasema kuwa mtu anapokula karanga, huongeza wastani wa miaka miwili na nusu katika umri wake wa kuishi. Karanga ni chanzo kikubwa cha mafuta asili, hivyo hutoa faida sawa na zile zinopatikana kwenye Olive Oil. Pia karanga ina kiwango kikubwa cha vitamini, madini na virutubisho vingine, vikiwemo vya kukinga mwili.

MVINYO (WINE)
Utafiti unaonesha kuwa unywaji wa kilevi kwa kiwango cha kawaida, hutoa kinga dhidi ya magonjwa ya moyo, kisukari na upotevu wa kumbukumbu kichwani kutokana na umri mkubwa. Kwa mujibu wa utafiti huo, aina mbalimbali za vileo (alcohol) zinaonesha kuwa na faida hizo, lakini mkazo wa utafiti umeelekezwa zaidi kwenye mvinyo mwekundu. Inaelezwa kuwa mvinyo mwekundu una kirutubisho kiitwacho ’resveratrol’ ambacho, kwa mujibu wa utafiti, huzuia kuzeeka kwa chembechembe za mwili.

MTINDI
Mwaka 1970, Georgia ya Urusi, ilidaiwa kuwa na idadi kubwa ya wazee wenye umri wa miaka 100 kuliko nchini nyingine duniani. Taarifa za wakati huo, zilidai kuwa siri ya watu wengi kuwa na umri mkubwa kama huo ni mtindi, ambao huliwa katika mlo wao wa kila siku. Wakati uwezo wa mtindi kurefusha maisha ya mtu haujathibitishwa kisayansi, lakini inaeleweka kuwa mtinmdi una kiasi kikubwa cha madini ya kashiamu na aina fulani ya ‘bacteria’ ambao hutoa kinga kwenye utumbo mdogo dhidi ya maradhi mbalimbali ya tumbo.

Mwisho, kumbuka kuwa jinsi ulivyo au utakavyokuwa baadaye, kunatokana na unavyokula, hivyo jitahidi kuwa ‘mchaguzi’ kwa kila kitu unachokula ili kulinda afya yako. Nawe kama una mchango wowote wa makala kuhusu suala la lishe ambayo ungependa kuchangia na wenzako, usisite kunitumia kwa email: amsalawi@yahoo.com.

No comments: