Tuesday, September 29, 2009

KIHARUSI: UGONJWA HATARI WA KIMYA KIMYA


KAMA kuna jambo au tatizo la kiafya linaloweza kubadilisha maisha ya mtu au hata kupoteza uhai wake haraka, ni ugonjwa wa Kiharusi (Stroke). Ugonjwa huu, ambao huwa ni matokeo ya matatizo ya kiafya ya muda mrefu, huweza kumtokea mtu bila kutarajia.


Lakini wataalamu wa masuala ya afya, hasa wanaoufahamu vizuri ugonjwa huu, wanatuambia kwamba kabla ya mtu kupatwa na kiharusi, huonesha dalili fulani, ambazo kama zikigundulika mapema na kushughulikiwa, anaweza kunusurika na athari zake.

Hebu soma kisa hiki; Wakiwa katika pikiniki, wakila, kunywa na kufurahi, Asha anajikwaa na kuanguka chini, wenzake wanashtuka na kumuuliza; “kulikoni, unaumwa?


Asha anajibu kuwa hana tatizo, bali viatu virefu alivyovaa, ambavyo hajavizoea, ndivyo vilivyomuangusha, anawatoa wasiwasi wenzake kuwa haumwi chochote. Asha anainuka, anajifuta na kuendelea na kufurahi na wenzake kama kawaida, ingawa usoni anaonekana hayuko sawa.


Wanamaliza pikiniki yao na saa 12 jioni ilipowadia kila mmoja alikuwa nyumbani kwake. Saa 3 baadaye, ndugu yake Asha anawapigia simu rafiki zake na kuwaambia kuwa Asha amekimbizwa hospitalini, baada ya kuanguka tena na saa moja iliyofuata, Asha alifariki dunia..! Kumbe Asha alipatwa na kiharusi tangu wakati ule akiwa pikiniki na wenzake.

Laiti wangebaini kuwa kule kuanguka kwake kulikuwa ni dalili ya kupatwa na kiharusi, wangemuwahisha hospitali na angepatiwa matibabu na pengine angepona. Wanaowahishwa hospitali, baadhi hupona kabisa na baadhi hunusurika kifo lakini hubaki katika hali mbaya, kama vile kupooza baadhi ya viungo au mdomo kwenda upande.

Wataalamu wa ugonjwa huu wanasema kuwa mgonjwa anapowahishwa hospitalini ndani ya muda wa saa 3 na kupewa matibabu yanayostahili huweza kupona kabisa.


UTAMJUAJE MGONJWA?

Wakati mwingine kuzijua dalili za kiharusi ni vigumu. Madaktari wanasema kuwa unaweza kumjua mtu anayenyemelewa na kiharusi kwa kumuuliza maswali matatu rahisi yafuatayo:


-Mwambie atabasamu – mtu mwenye tatizo hilo hawezi kufanya hivyo, akifanya atafanya kwa shida

-Mwambie azungumze na kusema sentesi fupi, kama vile; “hali yangu leo siyo nzuri” – bila shaka hataweza kusema, mdomo huwa mzito.

-Mwambie anyanyue juu mikono yake miwili – hatoweza kufanya hivyo.


Inaelezwa kuwa, iwapo ndugu, jirani au jamaa yako atafanya mambo hayo matatu kwa shida au akashindwa kufanya moja wapo, muwahishe haraka hospitali!

Njia nyingine ya kumgundua mtu mwenye kiharusi, ni kumuomba atoe ulimi nje – mara nyingi wenye kiharusi hushindwa kufanya hivyo na wakiweza, huweza kutoa ukiwa upande


UNAWEZAJE KUJIZUIA?

Hakuna njia nyingine unayoweza kujiepusha na ugonjwa huu isipokuwa kuzingatia ulaji sahihi wa vyakula. Watu wote ninaowajua mimi waliopoteza maisha au kuathirika kutokana na ugonjwa huu, historia yao ya ulaji vyakula haikuwa nzuri kabisa.


Ulaji sahihi ndiyo wimbo wa kila wiki katika makala haya. Tunaposema ulaji sahihi, tuna maana kuzingatia ile kanuni inayotutaka kula vyakula kutokana na umuhimu wake mwilini na si kwa sababu ni vitamu mdomoni. Kanuni hiyo inatutaka tule vyakula kwa wingi vitokanavyo na nafaka halisi.


Tunatakiwa tule kwa wingi matunda na mboga za majani kila siku, tunatakiwa tule kwa kiasi vyakula kama vile nyama nyekundu, maziwa, vyakula vya kukaanga n.k na tunatakiwa tule kiasi kidogo sana cha sukari na bila kusahahu kunywa maji mengi kila siku, angalau lita moja.

Kushindwa kuzingatia kanuni hizo, ni kukaribisha matatizo mengi ya kiafya, ikiwemo ugonjwa huo hatari ambao unatuondoa kimya kimya tukiwa na umri mdogo.

No comments: