Wiki iliyopita tuliendelea na makala haya yenye lengo la kujua sababu za watu kuugua mara kwa mara. Tumeanza kwa kuona kuwa mwili una kanuni zake ambazo ni lazima zifuatwe na zisipofuatwa huleta maradhi. Vile vile tumeona kuwa maradhi hayaji ghafla, bali huanza kwa kutoa ishara ambazo watu wengi, ama hawazijui au huzipuuzia…Sasa endelea.
Wapo wanaodai kuwa kula matunda mwishoni hakuna ubaya wowote, lakani watafiti wamegundua ulaji wa matunda baada ya mlo unapunguza kiwango cha virutubisho vinavyoingia mwilini. Tunashauriwa kula matunda kwanza na baada ya nusu saa au zaidi ndiyo tule chakula ili kupata faida hasa ya matunda.
Maziwa, jibini, mtindi
Kundi la tatu la vyakula ni vile vitokanavyo na bidhaa za maziwa, ikiwemo maziwa fresh, mtindi, jibini, n.k. Kiwango tunachotakiwa kula kutoka katika kundi hili ni kidogo ukilinganisha na kile cha matunda na mboga. Kwa watu wazima tunatakiwa tunywe maziwa kiasi, isipokuwa watoto wadogo ambao kinywaji chao kikubwa ni maziwa.
Aidha, elimu ya kutosha inahitajika katika suala la unywaji maziwa. Inaeleweka kuwa maziwa ni kinywaji salama na chenye virutubisho vingi vyenye faida mwilini, lakini tahadhari inatakiwa kuchukuliwa unapokunywa maziwa, kwani yanaweza pia kuwa chanzo cha tatizo lingine.
Usipende kunywa maziwa yenye mafuta (Full Cream) na badala yake pendelea maziwa yaliyoondolewa mafuta (Fat Free Milk) au yenye kiwango kidogo sana cha mafuta. Maziwa yenye mafuta mengi siyo mazuri. Kama unavyojua, mafuta yakizidi mwilini huwa chanzo cha magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
Ulaji nyama, samaki, mayai, maharage
Hili ni kundi la vyakula vinavyotoa protini mwilini na ni kundi la tatu kati ya makundi matano ya vyakula. Vyakula vya kundi hili ni muhimu kama vilivyo vyakula katika makundi mengine, lakini vyakula vyake vinatakiwa kuliwa bila kuzidisha kiasi.
Tunajua umuhimu wa protini mwilini, lakini pia yatupasa kujua madhara anayoweza kuyapata mtu anayekula kiasi kingi cha vyakula hivi, hasa nyama na mayai.
Nyama
Linapokuja suala la kula nyama, hasa ya ngo’mbe, mbuzi, nguruwe na zingine za wanyama wa porini, tahadhari kubwa inatakiwa kuchukuliwa, kwani aina hii siyo yote ni nzuri kwa afya yako.
Tunaelezwa kuwa, miongoni mwa madhara anayoweza kuyapata mtu anayependa sana kula nyama nyekundu kwa wingi, ni pamoja na kusababisha shinikizo la damu, ugonjwa wa kuvimba miguu au magoti. Chanzo cha matatizo hayo, pamoja na mambo mengine, huwa ni ulaji wa nyama kwa kiasi kingi. Mtu mwenye matatizo hayo haruhusiwi kugusa nyama tena.
Kama nilivyogusia hapo juu kuwa kuna sehemu ya nyama ni bora kuliko nyingine linapokuja suala la kula kwa ajili ya kupata protini mwilini. Katika nyama, kuna sehemu zina mafuta mengi na sehemu zingine hazina, epuka kula nyama zenye mafuta na badala yake kula nyama isiyokuwa na chembe ya mafuta (Lean Meat).
Mtu anayechagua aina hiyo ya nyama, ambayo huwa ni steki isiyokuwa na mafuta na kupikwa bila kuwekwa mafuta yoyote, hupata faida ya protini na hivyo kujiweka mbali na hatari ya kupatwa na magonjwa yaliyoelezwa hapo juu.
Maziwa
Aidha, linapokuja suala la kunywa maziwa, tahadhari pia yapaswa kuchukuliwa kama ilivyo kwenye nyama.
Itaendelea wiki ijayo...
1 comment:
Tafadhali mada hii nzuri sana, endelea kutupa zaidi.
Asante sana kazi nzuri kaka.
Post a Comment