UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA ZILIZOTOLEWA KWENYE VYOMBO
VYA HABARI NA MITANDAO JUU YA KUINGIZWA NA KUWEPO KWA DAWA BANDIA ZA KUTIBU
KIFUA KIKUU
1. Hivi
karibuni baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini na mitandao ya kimataifa
imetoa taarifa juu ya kuingizwa au kuwepo kwa dawa za kutibu ugonjwa wa kifua
kikuu (Tuberculosis – TB) zinazohisiwa kuwa ni bandia katika baadhi ya nchi za
bara la Afrika ikiwemo Tanzania.
2. Taarifa
zilizotolewa zimeainisha kuwa sampuli zilichukuliwa kutoka kwenye maduka ya
dawa binafsi (private pharmacies). Ufafanuzi unatolewa kwamba, dawa za TB
huingizwa nchini kwa utaratibu maalum ambapo ni Bohari ya Dawa (MSD) pekee
ndiyo hununua na kusambaza dawa hizi katika vituo vya kutolea huduma za afya vya
Serikali na baadhi ya vituo binafsi chini ya kibali na usimamizi maalum. Dawa
zinazoruhusiwa kuingia nchini ni zile zilizosajiliwa na kuthibitishwa na TFDA.
Dawa za kutibu TB haziruhusiwi kuuzwa kwenye maduka ya dawa binafsi.
3.
TFDA
inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma kuwa taarifa hizo sio za kweli. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba mifumo ya ufuatiliaji wa ubora na usalama wa dawa ingeweza
kubaini dawa hizo katika soko. Kwa
mfano, kwa mujibu wa takwimu zilizopo, matoleo (batches) 89 ya dawa za TB yaliyochukuliwa kwenye vituo vya forodha (ports of entry) kati ya Januari 2011 na Disemba 2012 na kupimwa kwenye Maabara ya TFDA
yameonesha kukidhi vipimo vya Maabara. Aidha,
matoleo 46 ya dawa za TB
yaliyochukuliwa kutoka katika vituo vya
afya vya Serikali kati ya Juni – Disemba
2012 pia yamekidhi vipimo vya Maabara baada ya kuchunguzwa.
4.
TFDA
imeweka mifumo thabiti ya kusajili, kukagua, kuchunguza kwenye Maabara na kufuatilia
ubora wa dawa zilizoko kwenye soko. Kupitia mifumo hii, TFDA inaweza kubaini
uwepo wa dawa duni na bandia katika soko. Pamoja na mifumo iliyopo, TFDA inawaomba
wananchi kutoa taarifa pale wanapokuwa na mashaka kuhusu ubora na usalama wa dawa za TB pamoja na dawa nyingine ili hatua stahili zichukuliwe
kwa mujibu wa sheria.
5.
Mamlaka
inawashauri wagonjwa wa TB kuendelea kutumia dawa za kutibu ugonjwa huo
zinazotolewa bure kwenye vituo vya afya vilivyoruhusiwa na Serikali kwa kuwa ni
bora, salama na zenye ufanisi uliothibitishwa na TFDA.
6.
TFDA
itaendelea kufuatilia taarifa hizo na kufanya ukaguzi zaidi ili kuhakikisha
kwamba dawa za TB zinazotumika nchini ni bora na salama wakati wote.
Kwa maelezo au
ufafanuzi zaidi, tafadhali wasiliana na;
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA),
S.L.P 77150, Dar Es
Salaam
Simu: +255 22 2452108/22
2450512
Au: 0658 445222/ 0685
701735/ 0777 700002
Nukushi: +255 22 2450793
Barua pepe: info@tfda.or.tz, Tovuti: www.tfda.or.tz
No comments:
Post a Comment