Mkurugenzi
wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akifafanua jambo kwa umakini mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani)
jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki kuhusu maandalizi ya tamasha la
kumshukuru Mungu kwa amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu litakalofanyika
Desemba 25.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki kuhusu maandalizi ya tamasha la kumshukuru Mungu kwa amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu litakalofanyika Desemba 25.
KAMPUNI ya Msama Promotions imeamua
kuandaa Tamasha la muziki wa Injili litakalofanyika katika Ukumbi wa Diamond
Jubilee, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumshukuru Mungu nchi kuvuka salama
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki,
Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, alisema wameamua kuua ndege wawili kwa jiwe moja, kwani sasa litafanyika
Desemba 25, likibeba Sikukuu ya Krismasi na shukrani hiyo ya kuvuka salama
katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema kutokana na tamasha hilo kubeba ajenda hizo mbili kwa pamoja, kamati
yake imelipa uzito mkubwa kwa upande wa suala la maandalizi ambapo wameanza kuzungumza na
waimbaji nguli wa kitaifa na kimataifa.
Msama alisema baada ya tamasha hilo
kufanyika Desemba 25 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, litahamia katika mikoa
mbalimbali itakayoteuliwa na kamati yake kwa kuzingatia kigezo cha wingi wa
maombi na uwezo wao kifedha.
“Naomba ifahamike, tamasha hili la
kumshukuru Mungu kuiwezesha nchi kuvuka salama katika mtihani mgumu wa Uchaguzi
Mkuu uliokuwa na ushindani mkubwa, litafanyika Desemba 25 katika Ukumbi wa
Diamond Jubilee,” alisema Msama na kuongeza:
“Unaweza kuona ni tamasha ambalo safari
hii litakuwa na uzito mkubwa, kwani litakuwa limebeba uzito wa Krismasi
itakayoambatana na shukrani maalumu kwa Mungu kutokana na kuijalia nchi kuvuka
salama katika Uchaguzi Mkuu,” alisisitiza Msama.
Kuhusu waimbaji, Msama alisema kamati
yake itajitahidi kuwaleta wenye uzito na mvuto kulingana na uzito wa tamasha hilo, akiamini litakuwa na
mvuto wa tofauti na yaliyotangulia na kuwasihi wapenzi na mashabiki wa muziki
wa Injili kukakaa mkao wa kupokea baraka za Mungu.
Msama kupitia Kampuni yake ya Msama
Promotions, amechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa Injili nchini
kupitia ubunifu wake wa kuratibu matukio ya muziki huo kuanzia tamasha la
Pasaka, Krismasi na uzinduzi wa kazi za waimbaji mbalimbali.
Juhudi hizo za Msama ndizo zimeufanya
muziki wa Injili kupata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kiasi cha kuwa
moja ya ajira kwa vijana wenye vipaji na karama ya kumtumikia Mungu kwa njia
hiyo ya uimbaji.