Tuesday, August 14, 2007

MWONGOZO BORA WA ULAJI - 2


Wiki iliyopita tulianza sehemu ya kwanza ya makala haya na tuliangalia miongozo mitano kati ya kumi inayofaa kufuatwa katika kufuata kanuni za ulaji sahihi wa kila siku.

Wiki hii tunaendelea na miongozo ya mwisho mitano kama ifuatavyo:

6. kula milo mitano ya matunda kwa siku (5-A-DAY)
Hakikisha unafikia lengo la kula milo mitano ya matunda kwa siku, kiasi hicho ndicho kinachopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), lakini kiasi hicho ni cha kuanzia tu, unaweza kula zaidi ya hapo. Mlo mmoja ni sawa na kisahani kimoja cha chai, hivyo mwili unahitaji angalau visahani vitano vya matunda kila siku.

Aidha, unashauriwa kula mboga za majani katika kila mlo na kula matunda yenye rangi tofauti tofauti ili kupata virutubisho mbalimbali na muhimu kwa ustawi wa afya yako.

7. Epuka kukaanga vyakula (Skip Fry-up)
Epuka kula vyakula vya kukaanga, na kama ukilazimika kukaanga, basi usitumie mafuta yaliyobandikwa lebo ya 'vegetable oil', mafuta aina hii huharibika kirahisi yanapopata joto na hivyo kuwa si salama kiafya na huongeza kasi ya mtu kuzeeka!
Badala yake pendelea kuoka, kuchoma au kuchemsha vyakula. Ukilazimika kukaanga, basi tumia mafuta yaliyandikwa 'Olive Oil', 'Corn Oil' au 'sunflower oil' ambayo hayana madhara kiafya.

8. Kula mafuta mazuri (Eat 'good' fats)
Katika milo yako, tumia mafuta yaliyo bora, usiache kabisa kutumia mafuta, kwani mafuta nayo yana umuhimu wake katika mwili wa binadamu, ili mradi ni yale yaliyo katika kundi zuri.

Mafuta hayo mazuri utayapata kwa kula karanga, korosho, maparachichi, samaki, mafuta ya alizeti na nafaka, yote haya yameonesha kuwa na faida nyingi za kiafya, ikiwa ni pamoja na kuongeza kinga ya mwili, kulinda ubongo pamoja na moyo.

9. Punguza sukari (Kill the sugar).
Punguza kiwango cha sukari katika milo yako kwa kuepuka kula vyakula vilivyohifadhiwa kwenye makopo au paketi. Usipende sana kula keki, biskuti na vyakula vingine vya aina hiyo ambavyo huwa na kiasi kikubwa cha sukari. Badala yake pendelea zaidi kula matunda ya aina mbalimbali ambayo huwa na sukari nzuri itakayokusaidia kiafya mwilini.

10. Kula maharage (switch to beans)
Katika mlo wako, usikwepe kula maharage, njegele, njugu mawe na jamii nyingine za maharage kwani yana faida na umuhimu mkubwa katika mwili wa binadamu.

Maharage siyo tu yana kiasi kikubwa cha ufumwele (fibre), bali pia hayana kiasi kikubwa cha protein ambayo unaweza kuipata hata usipokula nyama, ambazo mara nyingi huwa zina kiasi kikubwa cha 'mafuta mabaya'.

Kwa ujumla ukizingatia mwongozo huu wa chakula, bila shaka unaweza kuishi maisha ambayo hutasumbuliwa na maradhi ya mara kwa mara.

2 comments:

Anonymous said...

Jamani tunasubiri majibu ya picha zilizozua mgogoro.Mlidai tu-stay tuned mngejibu jana hiyohiyo,sasa kutwa nzima mlikuwa na kikao nini?

Anonymous said...

Mrisho tunasubiri maelezo uliyoahidi kuyatoa kufuatia majibu ya Chahali. Usikwepe, maana kwa kufanya hivyo ndio utakuwa unatudhihirishia kiwango cha ukweli wa habari unazozichapa