Tuesday, November 6, 2007

JINSI ULIVYO KUNATOKANA NA UNAVYOKULA!


Mtoto Brenna Dinkel akiwa na bonge la cabbage, ambalo hivi karibuni lilishinda tuzo katika maonesho ya Biashara ya Jimbo la Alaska. Soma umuhimu wa mboga hii..

UPUNGUFU WA KINGA MWILINI (UKIMWI):
Chanzo na jinsi ya kukabiliana nao kwa lishe

Leo tunazungumzia tatizo ya upungufu wa kinga mwilini, tatizo ambalo huufanya mwili kukosa nguvu na uwezo wake wa asili wa kupambana na maradhi. Kama tujuavyo, kinga ya mwili ndiyo inayotuepusha na maradhi mbalimbali. Mwili unapokosa kinga, huwa ni sawa na nyumba msituni isiyokuwa na milango wala madirisha.

Unapozungumzia tatizo la upungufu wa kinga mwilini, baadhi huelewa ni mtu kuishi na virusi vya HIV. Virusi vya HIV ni miongoni tu mwa vitu vinavyosababisha upungufu wa kinga miwlini, sababu kubwa ikiwa ni staili ya maisha unayoishi (lifestyle) pamoja na ukosefu wa lishe bora.

Katika makala zetu zilizopita, tuliwahi kueleza kwa kirefu kuwa mtu anaweza kuwa na upungufu wa kinga mwilini lakini akawa hana virusi vya HIV na anaweza kuwa na virusi vya HIV lakini hana upungufu wa kinga mwilini. Suala la msingi linakuwa unaishije, unakula nini na unakulaje.

DALILI ZA UPUNGUFU WA KINGA MWILINI
Baadhi ya dalili zinazoweza kuashiria kuwa mwili wako umepungukiwa kinga ya kukabiliana na matatizo ya kiafya ya mara kwa mara ni pamoja na:

Kupatwa na maambukizi sugu, kama vile kifua kikuu, n.k. Kukohoa na kuumwa mafua mara kwa mara. Kutokwa na vidonda mdomoni au malengelenge sehemu za siri mara kwa mara. Kuvimba tezi na kupatwa na saratani.

CHANZO CHA KUPATWA NA UPUNGUFU WA KINGA
Kuna uhusiano mkubwa kati ya upungufu wa kinga mwilini na hali ya mtu kuwa na jazba kila wakati, msongo wa mawazo, staili ya maisha anayoishi, chakula anachokula na jinsi alavyo. Sababu zingine zinazochangia kushuka kwa kinga ni pamoja na matumizi ya dawa kali za tiba na umri mkubwa.

Ifuatayo ni orodha kamili inayoweza kusababisha upungufu wa kinga mwilini:
Mwili kukosa lishe
Saratani
Virusi vya HIV
Uvimbe tumboni
Upungufu wa seli nyeupe za damu (Neutropenia)
Upasuaji wa kubadili viungo (Transplant)
Upungufu wa uasidi tumboni.

Aidha, upungufu wa kinga mwilini unaweza kusababishwa pia na umri mkubwa, kwani kadri umri wa mtu uanvyoongezeka, ndivyo kinga ya mwili nayo inavyoshuka. Baadhi ya watoto wadogo na wanawake waja wazito, nao hukabiliwa na tatizo la upungufu wa kinga mwilini.

NINI DAWA YA UPUNGUFU WA KINGA MWILINI?
Ni ukweli unaojulikana kwamba ili kuwa na kinga imara mwilini - uwe mtu unayeishi na virusi vya Ukimwi au mtu usiye na virusi - lishe bora ndiyo suluhisho pekee. Ili kuwa na kinga ya mwili imara, huna budi kuzingatia ulaji wa vyakula vifutavyo kwa wingi:

Kula kwa wingi matunda, mboga za majani, maharage, vyakula vitokanavyo na mbegu (ufuta, uwele, mtama), vyakula vitokanavyo na nafaka zisizokobolewa (whole grains) na mbegu jamii ya karanga.

Usipende kula kwa wingi vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi. Kula kwa wingi vyakula vyenye virutubisho vingi aina ya carotenes kama vile: maji ya matunda ya machungwa na mengine yenye rangi ya njano. Mboga za kijani cheusi, karoti, magimbi, viazi vitamu, pilipili hoho na nyanya.

Mboga ya kabichi na nyingine jamii ya kabichi, kama vile koliflawa, bokoli, figili na nyingine, zinasaidia sana kuzuia upungufu wa kinga mwilini. Mboga jamii ya kabichi sio za kupuuza kama baadhi ya watu wanavyodhani kuwa ni mboza za kimaskini.

USHAURI MWINGINE WA KUIMARISHA KINGA YA MWILI
Ili kufikia lengo la kuwa na kinga ya mwili iliyo imara, mazoezi na kunywa maji ya kutosha kila siku pamoja na kula lishe bora ni jambo la lazima. Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia katika kupambana na upungufu wa kinga mwilini;

UNYWAJI MAJI: Kunywa angalau lita mbili za maji kila siku (glasi 10 - 12) ili kuimarisha kinga ya mwili na kuondoa sumu mwilini.

MAZOEZI: Ufanyaji wa mazoezi kila siku, angalau ya kutembea kwa dakika 30 au ya viungo, ni njia bora ya kuimarisha mwili na kuuongezea uwezo wa kupambana na magonjwa. Vile vile inashauriwa kufanya mazoezi ya kuvuta na kushusha pumzi na kupumzika.

KUONDOA MSONGO WA MAWAZO: Inashauriwa mtu ajiepushe na msongo wa mawazo kwa kufanya vitu vya kuburudisha akili anavyopenda, kama kwenda kwenye burudani, michezo, kufanya 'shopping' n.k.

BADILI STAILI YA MAISHA: Kuwa na staili mbaya ya kuishi na ulaji usio sahihi, huathiri kwa kiasi kikubwa kinga ya mwili. Hivyo unashauriwa kuulinda mwili wako na kinga yako, kwa kufuata staili bora ya maisha na kula lishe bora kama ilivyoelekezwa hapo juu.

MWISHO: Kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, suala la kula lishe bora na kuishi staili ya maisha inayokubalika, kama ilivyoshauriwa hapo juu, ni jambo la lazima, wasipozingatia hayo wanakuwa wamejiweka hatarini zaidi kuliko mtu asiye na virusi.

Na kwa mtu ambaye hana virusi vya Ukimwi, ni vizuri kuzingatia suala la lishe na staili bora ya maisha ili kujiepusha na maradhi ya mara kwa mara na magonjwa mengine hatari. Adui mkubwa wa watu wote (wenye virusi na wasiokuwa navyo) ni maradhi. Maradhi hayachagui, yanaweza kumpata mtu yeyote na wakati wowote iwapo kinga yake ni dhaifu.

No comments: