Tuesday, December 4, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT!


UNASUMBULIWA NA UGONJWA WA MOYO?
SOMA HAPA!

Mwezi uliopita tuliandika kuhusu ugonjwa wa shinikizo la chini la damu (Low Blood Pressure) na shinikizo la juu la damu (High Blood Pressure au Hypertension) na tulielezea jinsi ya kuzuia au kukabiliana na magonjwa hayo sugu kwa kutumia vyakula vya aina mbalimbali, hasa matunda na mboga.

Leo tunaangalia kuhusu ungonjwa wa moyo (Coronary Heart Disease) ambao una uhusiano wa karibu sana na matatizo ya shinikizo la damu. Kama tutakavyoona katika makala haya, tatizo la ugonjwa wa moyo nalo linaweza kuepukwa au kudhibitiwa kwa kutumia chakula na kuisha staili sahihi ya maisha.

Kwa mujibu wa wataalamu wetu, ugonjwa wa moyo unajumuisha dalili nyingi za kitabibu ambazo hujitokeza pale mishipa inaposhindwa kupeleka damu ya kutosha kwenye moyo na hatimaye kusababisha kiharusi, msituko wa moyo na kifo cha ghafla.
DALILI MBAYA
Watu wanaousumbuliwa na ugonjwa wa moyo, upumuaji wao huwa wa shida, hali inayosababishwa na damu kukosa hewa ya oksijeni ya kutosha, husikia maumivu kifuani au mikononi.

Aidha dalili nyingine kwamba moyo wako hauko sawa ni kusikia uchovu mara kwa mara, kuzimia, miguu na mikono kuwa ya baridi, moyo kwenda mbio na kutokwa jasho mara kwa mara.

KITU GANI KINASABABISHA UGONJWA WA MOYO?
Inawezekana kukawa na sababu nyingine, lakini sababu za msingi zinazosababisha ugonjwa wa moyo ni tabia ya ulaji usiosahihi, kuishi staili ya maisha ya kujibweteka na msongo wa mawazo.
Katika kufafanua kwa kina sababu hizo, utafiti wa kina uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Moyo na Mapafu ya Massachusetts, nchini Marekani, umeorodhesha mambo saba yafuatayo kuwa ndiyo visababishi vikubwa vya Ugonjwa wa Moyo:

1. Kuongezeka mwilini kwa kiwango kikubwa cha kolestro na vitu vingine vya mafuta mafuta.
2. Kupanda juu kwa shinikizo la damu
3. Kuongezeka kwa asidi kunakosababishwa na kukithiri kwa protini mwilini.
4. Kuwepo kwa ugonjwa wa kisukari
5. Unene wa kupindukia (utipwatipwa)
6. Uvutaji sigara na
7. Kutokufanya mazoezi ya mwili

Kimoja au mchanganyiko wa visababishi vilivyotajwa hapo juu, huweza kumsababishia mtu ugonnjwa wa moyo, visababishi ambavyo vingi vinachangiwa na ukosefu wa lishe sahihi mwilini. Aidha, mawazo ya mara kwa mara husababisha mwili kuzalisha homoni ambazo hatimaye huziba mishipa ya damu na hivyo kuuchosha moyo.

Baada ya kuona chanzo cha ugonjwa wa moyo na maelezo yake kwa ufupi, tuangalie sasa ni jinsi gani unaweza ukaudhibiti au kujiepusha nao kwa kutumia matunda na mboga au chakula kwa ujumla;

ZABIBU KAMA TIBA YA MOYO
Kama tunavyosema siku zote, matunda halisi yana faida kubwa katika mwili wa binadamu katika kutibu magonjwa mbalimbali, ukiwemo moyo. Zabibu zina uwezo wa kutoa ahueni kubwa kwa maumivu ya moyo na moyo kwenda mbio. Ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa haraka kwa kutumia lishe ya matunda ya zabibu pekee kwa siku kadhaa mfululizo. Juisi ya zabibu ndiyo hasa inapaswa kutumiwa na mgonjwa aliyepata mshituko wa moyo.

TUFAHA (APPLE) KAMA TIBA YA MOYO
Inaelezwa kuwa tunda hili, japo ni ghali hapa nchini, lina virutubisho venye uwezo mkubwa wa kuuamsha moyo. Wagonjwa wenye moyo dhaifu watapata ahueni haraka sana kwa kutumia kwa wingi tunda hili ambalo linapatikana kwa wingi mijini.
KITUNGUU KAMA TIBA YA MOYO
Vitunguu maji vimeonekana kuwa na thamani sana katika kupambana na ugonjwa wa moyo. Vitunguu vinasaidia sana katika kushusha kolestro kwenye damu. Kijiko kimoja cha chai cha juisi ya kitunguu, ikitumiwa asubuhi kabla ya kula kitu chochote, huwasaidia sana.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments: