Sunday, January 13, 2008

YOU ARE WHAT YOU EAT!


ZIJUE FAIDA 20 KIAFYA ZA MAZOEZI

Ili uwe na afya njema unahitaji mambo makubwa matatu; lishe bora, kupumzika na kufanya mazoezi. Mwendo wa dakika 30 wa kutembea kwa miguu kila siku unaweza kukuletea faida kubwa za kiafya kuliko hata jitihada za madaktari dazeni moja na madawa kadhaa.

Hii ina maana kwamba mazoezi yanaweza kukuepusha na maradhi mengi ambayo yangehitaji huduma ya dawa au madaktari bingwa. Lakini siyo tu mazoezi yanaimarisha afya, lakini pia yanaweza kukukinga na maradhi hatari kama ugonjwa wa moyo, kisukari na saratani.

Aidha, mazoezi yanaweza kukufanya uonekane kijana imara na mwenye afya njema. Majarida mengi ya kitabibu yameshaelezea faida za mazoezi kiafya na zifuatazo ni faida 20 muhimu zinazopatikana kutokana na kufanya mazoezi:

1. MAZOEZI NI MAZURI KWA AFYA YA MOYO WAKO
Kwa mujibu wa makala ya Dk. William Kraus wa kituo cha tiba cha Chuo Kikuu cha Duke nchini Marekani, hata ufanyaji wa mazoezi madogo, ikiwemo kutembea kwa kukaza mwendo, husaidia afya ya moyo. Anaongeza kusema katika jarida lake kuwa kufanya aina yoyote ya mazoezi ni bora kuliko kuacha kufanya kabisa na kufanya mazoezi zaidi ni bora kuliko kuacha kufanya kabisa.

Imeelezwa zaidi kuwa mazoezi hupunguza mafuta mabaya mwilini aina ya kolestrol LDL ambayo ndiyo husababisha mishipa ya damu kuziba na mtu kupatwa na kiharusi. Mazoezi pia hurekebisha shinikizo la damu na msongo wa mawazo; huimarisha utendaji kazi wa ‘insulini’ mwilini.

Mazoezi huimarisha utendaji kazi wa misuli ya moyo na utembeaji wa damu na huondoa uwezekano wa mishipa ya damu kuziba. Ugunduzi huu umethibishwa na wataalamu wa tiba kwa utafiti wa kisayansi walioufanya kwa miaka mingi.

2. MAZOEZI HUPUNGUZA UZITO
Utafiti unaonesha kuwa ili mtu apate faida hasa za kupunguza uzito, pamoja na lishe, anahitaji kufanya mazoezia angalau dakika 30 kila siku. Kama nafasi yako inakuruhusu, unaweza pia kufanya mazoezi ya kina kwa muda wa saa moja kila baada ya siku moja. Muhimu ni kufanya mazoezi kwa ratiba na bila kukosa kwa siku ulizojipangia.

Fanya mazoezi ya saa moja mara tatu hadi nne kwa wiki, siyo wiki moja tu kwa mwezi, na utafanikiwa kupata matokeo unayoyatarajia ya kupunguza uzito na kuwa fiti kimwili na kiafya.

3. MAZOEZI HUZUIA UGONJWA WA MIFUPA
Kwa mujibu wa wataalamu, mazoezi pamoja na ulaji wa vyakula vyenye madini ya kutosha aina ya calcium, hujenga mifupa imara. Mazoezi ya kunyanyua vitu vizito, kukimbia na kutembea husaidia kupunguza uwezekanao wa kupata ugonjwa wa mifupa kadri mtu anavyozeeka.

Aidha, wataalamu wanaongeza kusema kuwa inapendeza mtu kuanza mazaoezi akiwa bado kijana, lakini hata hivyo mtu anakuwa hajachelewa akianza kujenga mazoea ya kufanya mazoezi katika umri mkubwa, kwani siku zote mazoezi yana faida kuliko kutokuwa na mazoezi.

4. MAZOEZI YANAPUNGUZA SHINIKIZO LA DAMU.
Mazoezi ni mazuri kwa shinikizo la damu; bila kujali umri wako, uzito wako, jinsia yako au kabila lako. Pia haijalishai unafanya mazoezi ya kutembea haraka, kukimbia mbio au kuogelea, faida zake zote ni sawa!

Yalikoegemea matokeo ya ufafiti huu ni mazoezi ya viuongo, ambayo huongeza mapigo ya moyo na kuimarisha uwezo wa mwili kutumia ipasavyo hewa ya oksijeni. Utafiti zaidi ulijumuisha ufanyaji wa mazoezi hayo ya viungo kwa muda wa kati ya dakika 20 – 30 kwa wiki kadhaa.

Utafiti huo unaendelea kusema kuwa kwa wastani, mazoezi yaliwasaidia washiriki kupunguza shinikizo la damu kwa tarakimu nne za juu (systolic pressure) na tarakimu 2.5 za chini (diastolic pressure). Hata hivyo wataalamu wanatahadharisha kuwa wale wenye tatizo kubwa la shinikizo la juu la damu (Hypertension), wasitegemee peke yake mazoezi katika kulidhibiti tatizo lao.

5. MAZOEZI NI ‘DAWA’ BORA YA KUONDOA MFADHAIKO
Ni elimu ya kawaida kwamba mazoezi huzuia mfadhaiko na hasira, lakini mazoezi yanafanya vipi kazi hiyo?

Mazoezi huchukua nafasi ya matatizo yote ya mfadhaiko na msongo wa mawazo kwa kuyaelekeza sehemu nyingine na kukufanya uyasahau. Halikadhalika hali yako inaweza kubadilika na kuwa mwenye tabasamu na furaha kutokana na mchakato unaofanyika wa kuboresha homoni mwilini.

6. MAZOEZI HUZUIA MAFUA
Haina uhusiano wa moja kwa moja wa mazoezi kupunguza idadi ya watu wanaopata mafua, lakini watafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Carolina, nchini Marekani, wamegundua kwamba watu wanaofanya mazoezi mara kwa mara wana uwezekano mdogo wa kupata mafua kwa silimia 23 kuliko wale ambao hawafanyi mazoezi.

Na hata watu wanaofanya mazoezi wakipata mafua, dalili za ugonjwa hutoweka haraka kuliko wale wasiofanya mazoezi. Kwa maana nyingine, mtu anayefanya mazoezi, hata akiumwa na kutumia dawa, hupata nafuu na kupona haraka kuliko mtu asiyefanya mazoezi.

Wataalamu wa afya wanaamini kuwa mazoezi huamsha na kuimarisha kinga ya mwili kwa saa kadhaa kila siku, hivyo kusaidia kuondoa mafua na homa homa. Dakika 30 tu za kutembea kwa kukaza mwendo zinatosha kabisa kukupatia faida za mazoezi.

7. MAZOEZI HUPUNGUZA MAKALI YA UGONJWA WA PUMU
Wataalamu wa tiba za michezo wanasema kwamba inawezekana kwa mtu mwenye pumu kufanya mazoezi iwapo atatumia dawa zake ipasavyo na kuepuka vitu vinavyochochoe mgonjwa kushikwa na pumu.
Kuendelea .....

No comments: