Wednesday, September 24, 2008

AINA ZA FUNGA

Wiki hii tunaendelea tena na makala yetu kuhusu funga kama tiba na kinga ya maradhi mbalimbali mwilini. Wiki iliyopita tuliona jinsi funga inavyoweza kuondoa sumu mwilini na faida nyingine nyingi kama zilivyothibitika kisayansi. Wiki hii tutaangalia aina za funga zilizopo pamoja na mambo mengine, endelea…

AINA ZA FUNGA
Kuna aina kadhaa za funga ambazo mtu anaweza kuzitumia kwa lengo fulani. Funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni funga ya ibada, ambapo mfungaji anapata thawabu kwa Muumba wake lakini pia anapata faida za kiafya za ujumla zinazotokana na funga.

Aina hii ya funga inajulikana pia kama DRY FAST, kwa maana mtu hatakiwi kula wala kunywa kitu chochote kuanzia alfajiri hadi magaharibi jua linapozama, kwa muda wa siku 30 au 29. Mfungaji wa funga aina hii, licha ya kuwa ni ibada, anapata pia faida zote za kiafya tulizozieleza hapo juu.

Bila shaka mpenzi msomaji, kama nawe uko kwenye funga ya mwezi huu, unaweza kuwa shahidi wa faida zinazopatikana kiafya kutokana na kufunga, inawezekana hivi sasa husumbuliwi sana na presha, kisukari au kuumwa na kichwa kama inavyokuwa siku za kawaida.

Aina nyingine ya funga ni ile funga ya kawaida ambayo pia inajulikana kama RUGULAR FAST. Katika funga hii, ambayo hufungwa ili kutimiza malengo ya kiafya tu, mtu hali chakula bali hunywa maji mengi ili kuyeyusha sumu mwilini na kuitoa kupitia kwenye ngozi na figo.

Funga nyingine ya malengo ya kiafya ni ile ya kufunga kula vyakula vyote ispokuwa juisi za matunda tu, funga ya aina hii, ambayo pia hujulikana kama FRUIT JUICE FASTING, mtu hunywa juisi za matunda ya aina mbalimbali kwa siku kadhaa na ni njia ya uhakika ya kuondoa sumu zote mwilini na kuuacha mwili wako ukiwa safi na wenye ngozi nyororo.

Katika funga hii, inashauriwa kwa mfungaji kutokunywa juisi bila kuichanganya kidogo na maji, kwani bila kufanya hivyo inaweza kuvuruga mchakato wa usagaji chakula mwilini. Changanya nusu ya juisi yako na nusu ya maji baridi, lakini kamwe usichanganye na barafu au maji yaliyoganda.


DALILI ZINAZOJITOKEZA WAKATI WA FUNGA
Wakati wa funga kuna dalili kadhaa hujitokeza kwa mfungaji. Dalili hizo ni pamoja na tumbo kuwa na gesi na kuunguruma, kuongezeka na kisha kushuka kwa joto la mwili, mdomo kuweka utandu mweupe, kutapika na jasho kutoa harufu kali.

Dalili zote zilizotajwa hapo juu siyo mbaya bali zinaashiria habari njema kuwa mwili uko katika mchakato wa kujisafisha na kuondoa sumu iliyokuwa imeganda na kujikita kwenye mfumo wa mwili kwa muda mrefu.

FUNGA INADHOOFISHA MWILI?
Si kweli kwamba funga hudhoofisha mwili. Imegundulika kwamba kinachomkondesha mtu wakati wa funga ni woga na mara nyingi vitu tunavyoviogopa katika maisha yetu huwa vinatuaathiri. Baadhi ya watu wanaogopa kufunga kwa dhana kwamba mtu huwezi kushinda bila kula, unaweza kufa - kitu ambacho si kweli na ndiyo kinachowakondesha baadhi ya watu.


JINSI YA KUFUNGUA

Faida kubwa inayopatikana kutokana na kufunga inaweza kupotea na kusababisha madhara kama kanuni za kufungua hazitazingatiwa. Kwa kawaida wakati wa kufungua, kwa mfano magaharibi kwa waislamu, watu hukimbilia kula vyakula vya kila aina na kwa kiasi kikubwa.


Kwa hakika, faida ya funga inapatikana kwa aina ya chakula utakachokula baada ya kufungua na jinsi gani utakavyoweza kujizuia kula vyakula visivyosahihi. Wakati wa kufungua mtu anapaswa kuanza kwa kula vyakula vya asili kama vile juisi, matunda, maji, ambavyo havina kemikali za zumu na baada ya hapo kula mlo ulio sahihi na kwa kiasi cha kawaida.

Ni makosa makubwa kufungua kwa kuingiza tena sumu mwilini, kama vile kufungua kwa kuvuta sigara, kula mishikaki au vyakula vingine vilivyopikwa na mafuta mengi. Aidha, mtu anayefungua anatakiwa, si tu kula vyakula vya asili, bali pia kula kwa kiasi na siyo kula kupita kiasi kwa lengo la kufidia mlo wa mchana kutwa!

Mwisho kabisa, inashauriwa mfungaji kuendelea kuzingatia kanuni za ulaji sahihi, funga itakuwa haina faida yoyote kiafya iwapo wakati wa kufungua unakula kila aina ya chakula unachokiona mbele yako tena kwa kiwango kikubwa, itakuwa sawa na kujaza maji kwenye gunia.

Nawatakia funga njema waislamu wote duniani na Mungu awabariki!

No comments: