Tuesday, August 18, 2009

Chumvi na sukari: Vinaongoza kwa kuliwa, lakini ni hatari

Kama kauli mbiu ya makala haya inavyosema kila siku, Jinsi Ulivyo kunatokana na unavyokula, ndivyo ambavyo vyakula tajwa hapo juu, vinaweza kuwa mwilini mwako. Ukivila kama inavyotakiwa vina faida na ukila tofauti vina madhara kwako. Jinsi utakavyovitumia ndivyo utakavyokuwa kiafya. CHUMVI Chumvi ni miongoni mwa bidhaa muhimu ya kila siku kwa binadamu kwa upande wa chakula.

Kwa namna moja ama nyingine kila siku mtu analazimika kula chumvi, iwe kupitia mboga au vitafunwa vingine vilivyotayarishwa kabisa. Kwa bahati mbaya watu wengi wanakula kiasi kikubwa sana cha chumvi kuliko inavyohitajika na katika ulaji huo hula aina ya chumvi isiyo sahihi pia. Matokeo yake, chumvi hugeuka mwilini kuwa chanzo cha magonjwa sugu, kama ya presha.

Aina ya chumvi inayopendekezwa na wataalamu wetu kutumiwa na isiyo na madhara katika afya zetu ni chumvi asilia, kama vile chumvi bahari na kadhalika. Vile vile ni kiwango kidogo sana ambacho tunatakiwa kutumia kwa siku, ni makosa makubwa kuweka kiasi kingi cha chumvi kwenye chakula unachokula, kwa sababu tu unapenda ladha yake.

Wako watu ambao hupenda kuweka kiasi kingi cha chumvi katika milo yao ili kupata ladha aitakayo, bila kujua kiwango kinachohitajika mwilini ni kidogo, matokeo yake huwa ni kupata madhara mengine mwilini. SUKARI Kuna aina mbili kuu za sukari. Sukari Nyeupe na Sukari Nyekundu. Sukari nyeupe inaelezwa kuwa sukari mbaya na hatari kiafya kuliko kitu kingine. Lakini kinyume chake, sukari nyeupe ndiyo imekuwa chaguo la watu wengi wanapofanya ununuzi wa sukari dukani.

Inaelezwa kuwa ubaya wa sukari nyeupe unatokana na hatua inayopitia kiwandani ambayo mwisho wa siku inaondolewa virutubisho vyake vya asili na kubaki ‘makapi’ ambayo hayana faida yoyote mwilini zaidi ya kuletea ladha tamu na ya kupendeza mdomoni. Badala yake inashauriwa tutumie sukari ‘nyeusi’ (brown sugar)ambayo yenyewe inakuwa bado haijaoendolewa virutubisho vyake vya asili vinavyohitajika mwilini.

Rangi ya nje inaweza isikupendeze machoni, lakini iingiapo mwilini inaweza kuwa na faida sana. Kama itawezekana, ni bora ukaacha kabisa kutumia sukari na badala yake upendelee asali halisi. Uzuri wa asali, ambayo ina kiwango kikibwa cha sukari kisicho na madhara, unaweza kuitumia katika vinywaji na vyakula mbalimbali na kupata ladha nzuri.

Kwa kuwa bidhaa hizi mbili ni muhimu katika mahitaji yetu ya kila siku, na kwa kuwa ndiyo bidhaa tunayoitumia kwa wingi, ni vyema basi tukahakikisha tunajua kiwango na aina tunayotakiwa kuitumia kwa siku, ili tupate faida badala ya madhara kiafya.

1 comment:

DUNDA GALDEN said...

Duh kama mungu kupita hapa na sito wacha kupita au kula chabo,juzi tuu nilitoka kumwambia rafiki yangu mmoja juu ya kupunguza kula vitu vya sukari akawa mbogo sasa sina cha kuongea zaidi ya kumwambia asome hapa