Friday, September 11, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!

Piga kura kwa A.Y, Shaa
Tuzo za MAMA (MTV Africa Music Awards) zipo on air na inajulikana kwamba hapa Bongo, Ambwene Yesaya ‘AY’ na Sara Kaisi ‘Shaa’ (pichani juu) ndiyo nominees pekee waliotajwa kushiriki.

A.Y anachuana na wakali kama Jigga katika tuzo ya Msanii Bora wa Hip Hop, Shaa anaparurana na wasanii wa mataifa mengine katika tuzo ya Msanii Bora Anayekuja.

Wanaweza kushinda ikiwa tu hautobana kuwapigia kura, kumchagua AY andika neno BHH AY kwenda namba 0789 777 333 na Shaa unaandika BNA SHAA kwenda namba 0789 777 333. Unaweza kupiga kura mara nyingi uwezavyo ili kuipa heshima Tanzania katika eneo la muziki.
******

Watoto wa Michael Jackson Wapigwa stop shule
Watoto watatu wa mfalme wa Pop, Michael Jackson aliyefariki dunia hivi karibuni, Michael Jr, Paris na Prince wamepigwa stop kuhudhuria katika shule ya kitajiri iliyoko Los Angeles, Marekani waliyokuwa wakisoma wakati baba yao yuko hai.

Mtandao mmoja wa burudani ulisema kuwa familia ya Michael imeamua hivi sasa watoto hao wasomee nyumbani (Home Work) mpaka hapo

watakapowajengea shule nzuri yenye viwanja vya michezo.
“Familia ilikaa na kuamua kuwasimamisha watoto hao shule na kwamba itakuwa ikiwaletea waalimu nyumbani,” alisema rafiki wa karibu na familia hiyo.
********

Doreen Is back
Kupitia kipande hiki, ‘Mwana Mpotevu’ tutakuwa tukiwatafuta mastaa wa kitambo ambao waliwahi kufanya vyema kupitia sanaa zao kisha wakapotea. Kubwa zaidi litakuwa ni kwanini wapo kimya na huko waliko kwa wakati huo wanapiga ishu gani.

Kwa kuanza leo tunadondoka na binti aliyeingia kwenye game ya muziki wa kizazi kipya akiwa na umri mdogo na kufanya kazi kadhaa kisha kupotea, namzunguzia Doreen Mkude a.k.a Queen Doreen.

Alikuja kwa kasi na kushaini katika anga ya Bongo Flava kwa michano lakini ghafla ikawa jiiiii! Alipokutana na ShowBiz katikati ya wiki hii kabla ya yote alitamka kwamba sasa anarudi kamili kuwashika fans wote wa muziki.

Queen Doreen ambaye alikuwa memba active wa Kundi la Dar Scandal lililokuwa likiongozwa na Godfrey Tumaini ‘Dudubaya’, ameweka kweupe some issues zilizomfanya awe out of game kwa muda.

Mdada huyo alisema kuwa sababu namba moja iliyomfanya awe nje ya game ni masomo na kueleza kwamba aliona muziki Bongo si uwanja sahihi wa kuutegemea kufanya maisha ndiyo maana aliichenga Bongo Flava na kutimkia skonga.

Hata hivyo, Queen Doreen alisema kuwa kitu kingine kilichomkimbiza ni rushwa ya ngono kwa maelezo kuwa wadau wengi walikuwa wanabana kumsaidia mpaka pale atakaporidhia kuchekiwa on bed.

Mbali na hilo, aliimegea kona hii exclusive kwamba yupo anajiandaa na ujio mpya kwamba albamu yake ipo njia moja. Ni hayo tu kuhusu Doreen kwa leo. Cheki na sisi next week.
*********



Septemba 11 inakuja na mastaa kibao
Muvi ya kijanja yenye jina la Septemba 11 inatarajiwa kudondoka mtaani Oktoba Mosi mwaka huu ikiwa imesheheni mastaa wa kumwaga wakiwemo wadau wa game ya soka Bongo, Chile Kasoga anajiachia nayo.

Akipiga stori na ShowBiz mmoja wa washiriki wa filamu hiyo, Kulwa Kikumba a.k.a Dude aliyepiga mzigo ndani ya muvi hiyo kama dereva wa teksi, alisema kwamba kazi hiyo imewahusisha mastaa kama Flora Mvungi aliyecheza kama ‘Agness’ ambaye aliteswa kimapenzi na mchumba wake Benny Kinyaiya.

“Agness ni binti aliye katika maisha ya upweke baada ya wazazi wake kufariki dunia siku ya Septemba 11 kitu ambacho kinampa wakati mgumu kila anapojaribu kuiwaza siku hiyo ambayo pia ni siku yake ya kuzaliwa. Ni hadithi ya kusisimua ambayo kila mshiriki ameonesha uwezo wa hali ya juu,” alisema Dude.

Baadhi ya washiriki wengine katika muvi hiyo ni Golikipa Mzungu wa Yanga, Obren Curcovic, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo, Katibu Mkuu wa TFF Frederick Mwakalebela, Mtanga na wengine kibao.
*******

Ray, Makamua, Chid Benz njiapanda
Mastaa Ray, Makamua na Chid Benz wapo njiapanda kutokana na kujikusanyia kura chache, hivyo wanauchungulia mlango wa kutoka.

Awali, ilitakiwa leo mmoja wa washiriki aage shindano leo lakini kutokana na maboresho, wiki ijayo wawili watang’oka, hivyo kama wewe ni mpenzi wa Ray, Makamua au Chid Benz basi mpigie kura kwa wingi ili kumuokoa.

Wiki hii kila mshiriki amepewa namba maalumu ya ushiriki, hivyo badala ya kumchagua mshiriki kwa kutaja jina lake, utapaswa kutumia namba yake ya ushiriki tu. Aidha, namba za kupiga kura zimebadilika kwani sasa ipo namba maalumu, hivyo msomaji kazi kwako.

Unachotakiwa kufanya ni kuandika ujumbe mfupi wa maneno, SMS kupitia simu yako ya mkononi, unaandika neno IJUMAA unaacha nafasi, halafu unaandika namba ya mshiriki kisha unaituma kwenda namba 15551. Mfano; IJUMAA 000 halafu unaituma kwenda namba 15551.
*********

Ni bonge la impact kitaani
Staa wa muvi ya Madhila, Salum Mbwana ‘Salu’ amesema kuwa kazi yake hiyo ina bonge la impact sokoni kuliko wadau wengine wanavyoamini.

Salu aliongea na ShowBiz na kuiambia kuwa sehemu kubwa ya jamii ya Mtanzania iliyopata bahati ya kuiona nakala ya kwanza ya Madhila, imeguswa ujumbe uliopo kutokana na mtiririko wa matukio uliopangwa kitaalamu.

“Naweza kutoa picha hii, siku moja nikiwa nakatiza mitaa ya Jiji la Lukuvi, mama mmoja alinivaa na kuanza kulia, aliniambia alipoona Madhila alihuzunishwa mno kwa jinsi nilivyokuwa nateswa.
Akadai kwamba kila aiangaliapo muvi hiyo anakumbuka jinsi alivyokuwa akimnyanyasa ndugu yake ambaye alikuwa mlemavu kama mimi lakini baadaye aligundua kwamba alichokuwa anafanya ni kosa kubwa mbele ya Mungu na jamii iliyomzunguka.

“Hiyo ni sehemu ya kwanza, nakala ya pili ni kali zaidi na imeandaliwa kitaalamu na mtiririko wa matukio ni wa kiwango cha juu,” alisema Salu na kuwataka mashabiki wa filamu wasikose nakala zao kuanzia Jumatatu inayokuja.
*******
compiled by mc george

1 comment:

Anonymous said...

ni "Home Schooling" na sio "home work"!