Wednesday, March 3, 2010

LISHE YA KUKUEPUSHA NA UGONJWA WA MOYO


Ingawa inawezekana ukawa unajua vyakula ambavyo siyo vizuri kwa afya yako, lakini ikakuwia vigumu kuachana navyo kutokana na mazoea, utamu na wakati mwingine umaskini ulionao. Hata hivyo, unahitaji kuchagua kati ya maisha yako na kula.

Kuna msemo maarufu usemao kuwa hatuishi ili tule, bali tunakula ili tuishi, hivyo basi kama kweli unahitaji kuendelea kuishi kwa muda mrefu, ni vyema ukazingatia kanuni za ulaji sahihi.

Halikadhalika, ili ujiepushe na ugonjwa wa moyo, ambao ni miongoni mwa magonjwa sugu yanayoua mamilioni ya watu kila mwaka duniani, huna budi kujua vyakula unavyopaswa kula na unavyopaswa kuviepuka au kula kwa kiasi kidogo sana. Zifuatazo ni hatua saba ambazo ukizifuata utajiepusha na ugonjwa wa moyo, na kama tayari unao, utapata nafuu:

1. Punguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi
Hatua ya kwanza kuchukua ni kujiepusha na ulaji wa mafuta mabaya yanayosababisha kolestrol mwilini ambayo hutokana na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi mabaya. Kuwepo kwa kiasi kikubwa cha kuwepo kwa Kolestrol nyingi mwilini, husababisha kuziba kwa mishipa ya damu (arteries) ambayo humuweka mtu katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo au kupatwa na kiharusi.

Kwa kifupi, njia bora ya kujiepusha na matatizo ya moyo, ni kujiepusha na ulaji au matumizi makubwa ya siagi na jibini, pamoja na vyakula vingine vyenye kiwango kikubwa cha mafuta yanayosababisha kolestrol mwilini.

Pale unapolazimika kutumia mafuta, chagua mafuta yatokanayo na mimea kama vile alizeti, olive Oil au Conala oil, ambayo hayana kolestrol, hata hivyo mafuta hayo nayo yanatakiwa kutumiwa kwa kiasi cha wastani. Vile vile mafuta ya nazi si mazuri sana kwa afya ya moyo, nayo ni ya kuepukwa au kutumiwa kwa kiwango kidogo.

2. Kula vyakula vya protini vyenye mafuta kidogo
Vyakula kama vile nyama, mayai, kuku, samaki na maziwa, ndiyo vinavyoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha protini. Hata hivyo, wakati wa kula vyakaula hivi tahadhari na uchaguzi mkubwa lazima ufanyike ili kuepuka ulaji wa mafuta yasiyofaa kupitia vyakula hivyo.

Unapotaka kula nyama, chagua steki ambayo haina mafuta kabisa (Lean Meat). Unapotaka kula nyama ya kuku pia, epuka kula pamoja na ngozi ambayo huhifadhi mafuta mengi. Pia chagua samaki wasio na mafuta mengi, kama vile sangara, na badala yake kula aina nyingine ya samaki, hasa wale wa maji baridi. Pia unapotaka kunywa maziwa, kunywa maziwa yaliyoandikwa ‘Low Fat’ au ‘Fat Free’ na usinywe ‘Full Cream’.

Aina zote hizo za maziwa, zinapatikana kwenye maduka mbalimbali ya bidhaa za vyakula, hivyo ni vyema ukajua kilicho bora kwa afya yako. Kwa wale wanaotumia ‘fresh milk’ ni bora kuyachemsha na yanapopowa uengue ule utandu wake wa juu (malai) ambao huwa ni ‘cream’ ambayo si nzuri kwa afya ya moyo wako.

Vile vile, unaweza kujiepusha moja kwa moja na ulaji wa nyama na badala yake ukala vyakula vingine ambavyo ni salama zaidi na vina kiwango kikubwa tu cha protini, kama vile maharage na soya.

3. Kula kwa wingi matunda na mboga za majani
Mboga na matunda zina kiwango kikubwa sana cha vitamini na madini aina mbalimbli ambayo ni muhimu kwa afya ya binadamu, zina kiwango kidogo cha calories lakini kiwango kikubwa cha kamba lishe inayomuepusha mtumiaji na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo.

Jiwekee mazoea ya kula mara kwa mara matunda kwa kuweka kwenye friji yako ama jikoni, katika sehemu ambayo utayaona kirahisi na kutamani kula mara kwa mara.

Kwa mfano, unaweza kukatakata vipande vya karoti, zabibu, ‘apples’, ndizi au ‘peas’ kwa ajili ya kutafuna - tafuna mara kwa mara na kuondoa hamu ya kutafuna vyakula vingine vyenye mafuta.

Itaendelea wiki ijayo...

No comments: