Tuesday, August 31, 2010

JIKINGE NA KIHARUSI (STROKE) KWA FUNGA


Katika siku za hivi karibuni, ugonjwa wa kupooza sehemu ya mwili au kiharusi, umeongezeka kwa kasi ya ajabu ambapo tumeshuhudia watu mbalimbali, wakubwa kwa wadogo, wakipatwa na tatizo hili na wengine kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa wataalamu wetu, tatizo hili la kiharusi, hutokana na kuganda kwa damu mwilini kunakosababishwa na kuganda kwa mafuta kwenye mifupa ya damu. Hali hiyo husababisha damu kushindwa kuzunguruka katika mfumo wake kama inavyotakiwa na hivyo kusababisha mtu kupatwa na kiharusi.

Aidha, imeelezwa kwamba makampuni ya kimataifa yanayotengeneza vidonge vya kujikinga na tatizo la kuganda kwa damu mwilini, hufanya biashara kati ya dola za kimarekani Bilioni 10 hadi 20 kwa mwaka, kitu ambacho kwa wao ni biashara kubwa ambayo wangependa iendelee daima na wasingependa kuwepo tiba mbadala.

Kwa upande mwingine, tatizo la kuganda kwa damu mwilini linaweza kuepukwa kwa kuzingatia kanuni za lishe na ulaji sahihi tu. Lakini pia imegundulika kuwa hata funga, kama inayofungwa na Waislamu hivi sasa duniani, ni kinga kubwa dhidi ya maradhi hayo.

Kama ilivyoelezwa hapo juu kuwa tatizo la kiharusi linatokana na kuganda kwa damu mwilini, funga husafisha damu kwa kuondoa sumu na mgando wowote unaoweza kuwepo kwenye mishipa ya damu na hivyo kukuepusha na ugonjwa huo.

Kwa kawaida mwili umeumbwa ili ujilinde wenyewe, hasa pale unapopokea vitu sahihi na hasa chakula. Kitendo cha kutokula masaa kadhaa, akiba ya mafuta mwilini hutumika kama nishati, hivyo sumu sumu zilizopo mwilini nazo hutafuta njia ya kutoka.

Kwa mtu anayefunga mara kwa mara, hujitengenezea kinga kubwa katika mwili wake dhidi ya maradhi ya kiharusi (stroke) na kwa maana nyingine maradhi ya shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa moyo nayo hayawezi kumsumbua.

Ili mtu uwe na afya njema, viungo vifuatavyo na mifumo yake ni lazima viwe safi na vifanye kazi yake vizuri:

1. Utumbo mpana sharti uwe safi wakati wote. Ili kuwa na utumbo safi ni lazima uwe unapata choo cha kawaida kila siku bila matatizo kutokana na unavyokula. Moja ya kazi za funga ni kusafisha utumbo mpana kwa njia zake za asili na kuondoa sumu zote.

2. Mfumo wa usagaji chakula (digestive system) na njia ya kutolea uchafu na sumu, nayo lazima iwe safi na inayofanya kazi vizuri. Kwa kufunga, utaimarisha mfumo wako wa usagaji chakula pamoja na njia ya kutolea uchafu.

3. Mfumo wa damu mwilini, nao unatakiwa kuwa safi na uwe na uwezo wake wa asili wa kupitisha damu kwenye mishipa bila vikwazo vyovyote, kazi ambayo huweza kufanywa na funga pia na kuondoa chanzo cha kiharusi ambacho ni kuganda kwa damu (blood clotting).

4. Metaboli ya mwili wako (metabolism) au utendaji kazi wa mwili wako kwa ujumla katika kupondaponda na kusambaza vyakula mwilini, lazima uwe katika hali nzuri na funga ndiyo inayoweza kuboresha metaboli ya mwili wako.

5. Mfumo wa nyongo unaofanyakazi yake ya uzalishaji vizuri ambao ni muhimu kwa ufanisi wa usambazaji wa damu mwilini, mfumo ambao huweza kuimarishwa vizuri na funga.

Mtu anayeweza kuimarisha vitu vitano vilivyotajwa hapo juu, ndiye anayefanikiwa kuwa na afya njema na uchangamfu kila siku na kwake yeye funga ndiyo tegemeo lake.


1 comment:

Disminder orig baby said...

kaka siachi kufunga Monday and Thursday, hii ni dawa tosha naamini