WMU AKIULIZA SWALI KWA MMOJA WA WAONYESHAJI TOKA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
WAJUMBE
DT AKISISITIZA JAMBO
WADAU WAKUBWA WA UTALII NCHINI WAKITETA NA WMU
WANAMUZIKI WA MSONDO OMARIO9KULIA) GURUMO NA WMU
..KIKUNDI CHA NGOMA CHA ASILI
HOTUBA YA MHE. EZEKIEL M. MAIGE (MB) WAZIRI WA
MALIASILI NA UTALII ALIYOITOA WAKATI WA KUADHIMISHA SIKU YA UTALII DUNIANI ILIYOFANYIKA KITAIFA TAREHE 21/10/2011 - DAR ES SALAAM
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Katibu Mkuu- Wizara ya Maliasili na Utalii,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Kwa niaba ya Serikali napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wageni
wote waalikwa kwa kuacha shughuli na ratiba zenu muhimu mno na kuitikia mwito
wetu na kujumuika pamoja nasi katika
Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani. Pia shukrani zangu za kipekee ziende kwa Kamati ya Maandalizi yenye wajumbe
kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na
Taasisi zake, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar
es Salaam, Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Bodi ya Utalii Dar es Salaam (DTEB),
Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT) na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Nchi yetu ni mwanachama hai wa Shirika la Utalii Duniani kuanzia 1975.
Shirika la utalii Duniani limetenga siku ya tarehe 27 Septemba kila
mwaka kuwa siku maalum duniani kwa jamii
ya kimataifa katika kutafakari,
kudumisha na kuchochea maendeleo ya utalii kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Kila nchi hupanga namna itakavyoadhimisha siku hiyo chini ya Kauli Mbiu
itolewayo na Shirika la Utalii Duniani kila mwaka.
Mwaka 2011 kimataifa Siku ya Utalii Duniani ilisherekewa Mjini Aswan
nchini Misri chini ya Kauli Mbiu isemayo ”Tourism Linking Cultures” ikiwa na maana Utalii huunganisha
Tamaduni.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Mabibi na Mabwana,
Kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani chini ya Kauli mbiu isemayo Utalii
huunganisha Tamaduni (Tourism- Linking Cultures) ni kutambua uwezo mkubwa wa
utalii katika kuunganisha tamaduni mbali mbali. Kupitia utalii watu wenye tamaduni
mbali mbali husafiri kutoka
maeneo mbali mbali na kukutana na watu wenye tamaduni tofauti katika maeneo
waliyoyatembelea, hivyo kujenga mahusiano baina yao, hali ambayo hupelekea
kuvumiliana, kuheshimiana, kuelewana na kuleta amani duniani.
Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani kwa siku hii maalum ni mwito kwa wote wanaojihusisha na biashara
ya utalii kuheshimu tamaduni na kuendeleza shughuli za utalii zitoazo fursa na
faida kwa wanajamii.
Katika kuadhimisha siku hii nimefahamishwa kuwa yameandaliwa maonesho
ya wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ambapo
bidhaa na huduma mbalimbali za utalii zitaoneshwa. Pia
mdahalo maalum baina ya wadau wa
sekta ya utalii umeandaliwa.
Ni imani yangu kuwa
mtatumia muda huu vizuri na mtaweza kutushauri nini kifanyike, na nani, wakati
gani katika kuifanya Dar es Salaam kuwa kituo cha utalii, kuendeleza utamaduni
kuwa zao la utalii, kuunganisha wazalishaji wa bidhaa za utalii na walaji ili
kuhakikisha kuwa utalii Tanzaina unakua na kuweza kutoa mchango mkubwa zaidi
katika Pato la Taifa na kuwapatia wananchi kipato hivyo kujiondolea umaskini.
Mabibi na Mabwana,
Utalii ni miongoni
mwa sekta zinazokua kwa kasi duniani kiuchumi, ambapo takwimu zinaonesha mwaka
2010 Idadi ya watalii duniani ilifikia 940 milioni sawa na ongezeko la asilimia
6.6 kutoka mwaka 2009. Mapato
yatokanayo na utalii duniani yalifikia Dola za Kimarekani 919 milioni mwaka
2010 wakati mwaka 2009 mapato yalikuwa Dola za Kimarekani 851 milioni sawa na
ongezeko la asilimia 4.7
Takwimu zinaonesha idadi ya watalii Barani Afrika iliongezeka hasa kutokana na kuwa
wenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia
2010 yaliofanyika Afrika Kusini. Idadi
ya watalii ilifikiai 49 milioni mwaka 2010 ambayo ni ongezeko la asilimia 7 kutoka
mwaka 2009 na mapato yatokanayo na utalii yalifikia Dola za Kimarekani 31
milioni sawa na ongezeko la asilimia 4 sawia .
Sekta ya utalii Tanzania ni ya
pili kwa ukubwa katika kuchangia pato la Taifa ambapo utalii unachangia
asilimia 17. Takwimu zinaonesha mwaka 2010 Idadi ya watalii waliotembelea
Tanzania iliongezeka kufikia watalii 782,679
wakati mapato yatokanayo na utalii yalifikia Dola za Kimarekani 1.25 Bilioni. Mwaka 2009 watalii
waliotembelea Tanzania walikuwa 714,367 na waliliingizia taifa Dola za
Kimarekani 1.15 Bilioni.
Utalii huchangia zaidi ya asilimia 25 kwa fedha za kigeni.
Serikali imekusudia kuongeza mchango wa utalii katika pato la taifa na
katika kutoa fursa za ajira. Mkakati
mmojawapo unaotumika kama ulivyoainishwa katika Sera ya Utalii ya mwaka 1999 ni kupanua wigo wa utalii ikiwa ni pamoja na
kufungua maeneo mapya ya utalii na kuendeleza mazao mapya ya utalii hivyo
kuongeza muda wa mtalii kukaa nchini na kufanya matumizi zaidi. Hii ni pamoja
na kutumia fursa nyingi tulizo nazo
zikiwemo tamaduni zetu, sanaa zetu nk.
Mkoa wa Dar es salaam ndio mwenyeji wetu Mwaka huu. Ni vyema tuongeze
jinsi ya kulifanya Jiji liwe kivutio cha utalii. Hivi sasa Dar es salaam ni
jabali lililolala.
Kwa mfano Jiji la London ni moja kati ya Jiji la Kimataifa kati ya
Majiji 150 ambayo yanapokea Watalii mbalimbali wa Kimataifa. Hivi sasa Jiji la London linapokea Watalii
takriban m. 20 kwa mwaka. Mji mingine ambayo hupokea watalii kwa wingi ni pamoja na Bankok, Paris, New York na Singapore.
Majiji 150 ulimweguni huchangia theluthi
ya watalii wote wanaotembea sehemu mbalimbali ulimweguni. Mji ni kichocheo cha uchumi kwa kukuwa kwa
Sekta ya Utalii ambapo fursa za uwekezaji, miundo mbinu, majengo, na usafiri wa
anga ni moja ya changamoto zinazosukumwa na ukuaji wa Sekta ya Utalii Katiaa mijini.
Miji yetu ikiwemo jiji la Dar es salaam inawezekana kuwa vivutio vikuu
vya utalii na kuchangia katika kuongeza kipato na kutoa ajira kwa wakazi wake.
Ili kufikia lengo hilo lazima yawekwe mazingira yatakayochochea maendeleo ya
vivutio na huduma kwa watalii.
Ili watalii wakae na kutumia fedha
zao lazima tuwe na sehemu mbalimbali takazowafanya wafanye hivyo. Kwa mfano
tunahitaji kuwa na hoteli zenye huduma za ziada kukidhi matakwa ya watalii wa
kileo. Kwa mfano tuwe na maduka bora ya zawadi na souvenir. Tunahitaji kuwa na
maeneo ya wazi yenye kuwa na huduma za viwango na kwa mpangilio. Watalii
wanahitaji kutembea wakiwa huru na ndani ya maeneo yaliyo safi na yenye usalama
Katika majiji mengine watalii wa
ndani na wa nje hufanya burudani na kutumia fedha nyakati za jioni na usiku.
Hawawezi kufanya hivyo katika mitaa iliyo na giza kwa kutokuwa na taa za
barabarani. Hawataweza kufanya hivyo kama barabara zetu haziwi na maeneo ya
watembea kwa miguu. Hawawezi kufanya hivyo huku wakinyemelewa na wachuuzi na
vibaka.
Haya maendeleo ya huduma katika
nchi za wenzetu hufanya na Halmashauri za majiji yao na huchagizwa na madiwani
na mameya wao. Kwa nini Manispaa za jiji la Dar es salaam haziweki maaskari wao
na mgambo kuimarisha usalama kwenye maeneo muhimu ya kitalii. Kwa nini huduma
bora za vinywaji hazitolewi maeneo ya Mnazi mmoja saa za jioni huku kukiwa na
ulinzi wa kutosha. Kwa nini eneo la coco beach haliendelezwi kama walivyofanya
wenzetu wa Mji Mkongwe Zanzibar. Water
front za wenzetu ni maeneo makuu ya burudani na huduma za kuvinjari. Kwetu ni
eneo la kutupa takataka, kuegesha magari na maficho ya vibaka. Kwa nini eneo la
kuanzia fukwe iliyo mbele ya hoteli ya Kilimanjaro Hyatt hadi mbele ya posta
mpya halisafishwi, kuendelezwa na kuruhusu huduma kwa watalii ili jioni watu
wavinjari eneo hilo. Nafahamu Mamlaka ya Bandari wanahodhi eneo hilo na mipango
ya kuliendeleza ipo kwenye michoro na makabrasha yana vumbi la zaidi ya miaka
20 bila kutekelezwa kwa sababu ya kigugumizi na maamuzi ingawa Wakurugenzi
wamefanya study tour mabara yote ya ulimwengu kuona wenzetu wanafanya nini.
Kuwekeza mijini ni rahisi
ikilinganishwa na mbugani. Kwa mfano ujenzi na uendeshaji wa hoteli na migahawa
mijini ni rahisi ikilinganishwa na mbugani, ambapo huduma na mahitaji
mbalimbali yanapatikana mbali na kusafirishwa kwa gharama. Ni changamoto kwa
jiji na watu wa mipango-miji kuweka mazingira yatakayowezesha uwekezaji katika
huduma za malazi na burudani. Tukifanikisha hili tutaongeza ushindani na
kupunguza ughali wa huduma kwa wageni wetu. Tukifanya hivi tutapanua wigo na
kupunguza utegemezi wetu kwa aina moja au mbili tu za utalii wa mbugani na
kupanda mlima.
Huu ni muda wa kujirekebisha, na
kujipanga ili kulifanya Jiji la Dar es salaam livutie watalii. Natoa wito kwa
wadau wote wakiwemo viongozi na wanasiasa tuwe na msukumo wa kuelekea huko.
Nafahamu wadau wetu wa maendeleo wapo tayari kutuunga mkono, wafanyabiashara
wapo tayari kuwekeza lakini lazima tuondokane na umangimeza na tuongeze uwazi
na uwajibikaji.
Kazi ya kuendeleza utalii inahitaji ushirikiano wa wadau mbali mbali
kuanzia Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa ambao ndiyo wenye maeneo yenye
vivutio vingi, Serikali kuu, Sekta
binafsi, jamii na watalii wenyewe. Pia vyuo na taasisi zitoazo mafunzo ya
utalii na taasisi za utafiti vina mchango mkubwa katika uendelezaji utalii.
Bila kusahau mchango mkubwa wa vyombo vya habari
katika kutangaza fursa na kuelimisha umma juu ya umuhimu wa utalii na
namna wanavyoweza kunufaika na shughuli mbalimbali za utalii. Rai yangu kwenu leo ni kuwa mje na maazimiao yatakayopeleka mbele utalii wetu.
Tunapoadhimisha Siku
ya Utalii Duniani sambamba na miaka 50 ya uhuru, tuendelee kuitunza, kuipenda
na kuijenga nchi yetu na watu wake kwa kutunza na kudumisha hazina ya utamaduni
ambao ni pigo la roho ya taifa letu.
Baada ya kusema hayo
nawatakia siku njema na majadiliano yenye kuzaa matunda.
Asanteni kwa
kunisikiliza
No comments:
Post a Comment