Saturday, August 4, 2012

MJENGWABLOG INASHUTUMU KUFUNGIWA KWA MWANAHALISI

 
Ndugu zangu,
Mjengwablog, kama mtandao wa kijamii, unaungana na watetezi wa uhuru wa habari kushutumu hatua ya Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na masuala ya Habari, Utamaduni na Michezo kulifungia gazeti la kila wiki la  Mwanahalisi.

Tunaamini, kama ilivyo Serikali, kuwa vyombo vya habari navyo vinaongozwa na wanadamu. Yumkini yanaweza kutokea mapungufu ya hapa na pale na hata hali ya kutofautiana. Hivyo, tofauti hizo zitatuliwe kwa njia ya majadiliano, na pale inaposhindikana, vipewe nafasi, vyombo vyenye dhamana ya kutoa hukumu baada ya kusikiliza pande mbili zinazotofautiana.

Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kulifungia Mwanahalisi kwa kutuhumiwa na Serikali na kuhukumiwa na Serikali hiyo hiyo kuwa limeandika makala za uchochezi ni sheria iliyopitwa na wakati na inayopaswa kufanyiwa marekebisho ya haraka. Ni sheria kandamizi yenye kuongeza mashaka na hofu kwa umma juu ya watawala badala ya kuyapunguza na kuondoa hofu hizo katika dunia hii ya sasa iliyo tofauti na ile ya mwaka 1976.

Hakika, kufungiwa kwa Mwanahalisi kuna maana ya kuwanyima Watanzania haki yao ya kupata habari kwa kupitia gazeti hilo ambalo, kwa siku ya Jumatano, kwa wengine, kulinunua gazeti hilo kwao imekuwa ni kama ada.

Na kwa ukweli, wasomaji wa Mwanahalisi ni Watanzania wa kada mbali mbali ikiwamo watendaji walio Serikalini na hata ndani ya Wizara iliyohusika na kulifungia Mwanahalisi. Ndio, bila shaka nao pia wanasikitika kimya kimya kwa kunyimwa haki yao ya kulisoma gazeti hilo.

Ni matumaini yetu, kuwa Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na masuala ya habari itafikiria upya uamuzi wake huo wa kulifungia gazeti la Mwanahalisi. Kwamba, Mwanahalisi lifunguliwe bila masharti yeyote. Na kama kuna makosa yamefanywa na Mwanahalisi, basi, Serikali ilifikishe gazeti hilo Mahakamani.

Maana, mahakama ndio kimbilio la wenye kudai haki, iwe ni kwa wanyonge wanapoona hawakutendewa haki, na hata wenye nguvu wanapoona hawakutendewa haki, ikiwamo Serikali.

Na juu ya yote, Tanzania ya sasa kama nchi, tofauti na huko nyuma, inaruhusu watu wake kuwa na uhuru mpana wa kujieleza. Tanzania , kama nchi, bado haijawa na sifa mbaya ya kuminya uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari. Serikali ina wajibu wa kufanya iwezayo kuepuka kuwa na sifa hiyo mbaya. Maana, ni sifa mbaya isiyo na  maslahi kwa taifa katika dunia ya sasa.

Pamoja Tuijenge Nchi Yetu.
Maggid Mjengwa
Mwenyekiti Mtendaji
0788 111 765, 0754 678 252

No comments: