Ndugu zangu,
Imekuwa ni utamaduni wangu kutuma salamu za Mwaka Mpya kwa wajumbe wangu wa Mjengwablog, marafiki zangu kwenye FB na wengine walio ndani na nje ya mitandao ya kijamii.
Nimefanya hivyo tangu mwaka 2006 ilipoanzishwa Mjengwablog. Na mwaka huu naendeleza utamaduni huo.
Ndugu zangu,
Naandika salamu hizi nikiwa hapa Iringa, na nikiwa na mambo mawili ya kuwaeleza;
Mosi, napenda kuwahakikishia kuwa Mjengwablog/KwanzaJamii itaingia mwaka mpya wa 2016 na kasi zaidi ya mwaka jana. Tutazidisha ubunifu katika kuwaletea huduma mpya na bora zaidi.
Mosi, napenda kuwahakikishia kuwa Mjengwablog/KwanzaJamii itaingia mwaka mpya wa 2016 na kasi zaidi ya mwaka jana. Tutazidisha ubunifu katika kuwaletea huduma mpya na bora zaidi.
Ikumbukwe, Mjengwablog ilikuwa blogu ya kwanza hapa Tanzania kuja na ubunifu wa kuweka kurasa za mbele za magazeti mwaka 2007. Mwaka huu tumekuwa blogu ya kwanza Tanzania kwa kuwa wa kwanza kila alfajiri kuwaletea habari za magazetini zikiwa na uchambuzi wa habari ku 3 ikiwamo uchambuzi wa katuni bora ya siku.
Mwakani tumedhamiria kuunganisha huduma hizo na radio blogging ikiwa na maana ya kufanya chambuzi kwa njia ya radio ya mtandaoni na kuposti ( KwanzaJamii Radio). Mengine mapya ya kiubunifu yako jikoni, yatakuja kwa mwaka ujao, 2016.
Jambo la pili nililotaka kulisema linahusu hali ya mtanziko wa kisiasa Zanzibar. Ni majuzi tu nilikuwa Zanzibar kwa takribani juma moja. Nilitembea Zanzibar mjini na vijijini.
Hakika, sijawahi kupanda boti na kuviacha visiwa vya Zanzibar nikiwa na shaka ya kitakachotokea nyuma baadae. Safari hii niliondoka Zanzibar nikijisikia hivyo. Zanzibar sikuikuta hali njema ya upepo wa kisiasa. Nakumbuka nikiwa kitongoji kimoja pale Jambiani nilioongea na wenyeji walioonyesha shaka kwenye mazungumzo. yao wakati wakiongea nami.
Pale Jambiani niliiona chuki baina ya wenyeji iliyotokana na tofauti za kiitikadi. Chuki iliyoonyeshwa hata kwenye maandishi ya kutani na kwenye milango ya nyumba. Ni chuki iliyoonyeshwa hata kwenye mijadala ya mitandaoni ambayo binafsi niliianzisha kwa madhumuni ya kuamsha fikra na kubadilishana maarifa na uzoefu.
Niliyoiona si Zanzibar niliyoifahamu. Bado naamini, Zanzibar imejaa watu wakarimu na wenye upendo. Suluhu ya Zanzibar itapatikana na Wazanzibar wenyewe na kwa njia ya mazungumzo hadi kufikia muafaka.
Na walio kwenye meza ya mazungumzo wasitangulize maslahi binafsi. Kwenye kujadiliana ili kutatua mgogoro pande husika ziwe tayari kupata na kupoteza. Si vema pia kwenda kwenye meza ya mazungumzo ukihitaji jambo moja tu, kwamba kama ukilikosa ndio mwisho wa dunia.
Na duniani hapa mengine yaliyofutwa, na kama ni kisheria na yakachapwa hata kwenye gazeti la serikali, basi, si rahisi yakarejeshwa kwa wino ule ule. Ni vema ikatangulizwa hekima na busara. Ni vema na ni busara yakawekwa mazingira ya, hatma ya yote, kuwa pande zinazokinzana zote zikaibuka washindi.
Na hakuna namna yeyote ile ya kuvifanya visiwa vikawa tulivu bila ya uwepo wa makubaliano ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo viongozi wakuu wa pande zote mbili wafanye kazi ya ziada ya kuwahimiza wananchi wao kuchimba makuburi marefu ya kuzizika chuki zao baina ya wao kwa wao. Chuki zilizojengeka kwenye misingi ya ubaguzi. Na sote tunajua dhambi ya ubaguzi, ni kama dhambi ya mwanadamu kuonja nyama ya mwanadamu mwenzake, hawezi kuacha.
Ni iwekwe wazi, kuwa suala la Muungano wetu halipaswi kuwa mjadala tena kama uwepo au usiwepo, bali ni kwa namna gani tutauimarisha.
Maana, daima utabaki kuwa ukweli, kuwa jambo la Zanzibar ni letu Bara, na kinyume chake.
Maana, daima utabaki kuwa ukweli, kuwa jambo la Zanzibar ni letu Bara, na kinyume chake.
Na tuwe tayari kupambana hadi risasi ya mwisho, na nguvu zote hasi, za ndani na nje ya mipaka yetu, zinazotaka kututenganisha kwa misingi ya Uzanzibar, Upemba, Ubara na hata udini.
Ni imani yangu, kama ilivyotokea huko nyuma, kuwa Zanzibar imeweza kuvuka mitihani migumu na ikasimama tena.
Naziona ishara za tumaini jipya la Zanzibar linalokuja. Kwamba viongozi wakuu wa CCM na CUF Zanzibar watazishinda nguvu hasi na zinazochagizwa na wahafidhina wa pande zote mbili, hivyo, kupata formula mpya ya kuvivusha visiwa vya Zanzibar na Pemba kutoka kwenye mtanzuko wa kisiasa uliopo sasa.
Mungu Ibariki Tanzania na Heri Ya Mwaka Mpya.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
No comments:
Post a Comment