KONGAMANO kubwa la aina yake limefanyika mjini Dar es salaam ambapo washiriki walizungumzia namna ya kuendeleza rasilimali watu katika eneo la utaalamu na taaluma katika shughuli mbalimbali za uendelezaji wa makampuni na viwanda.
Kongamano hilo ambalo lilihudhuria na watu wenye kariba kubwa katika masuala ya viwanda na biashara akiwemo Dkt. Reginald Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa makampuni ya IPP na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF);na Balozi wa Ufaransa nchini Malika Berak liliangalia uhaba wa wataalamu na namna ya kuuondoa uhaba huo wakati taifa linaelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
Wengine waliokuwepo katika kongamano hilo Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero na maofisa wa serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akikaribisha washiriki na wadau wengine alisema kwamba mafunzo hayo yaliyoratibiwa kwa pamoja katika wataalamu wa Ufaransa, ESRF na Benki ya Maendeleo ya Afrika yamelenga kudadavua tatizo lililopo na kulipatia ufumbuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (katikati) akisalimiana na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kulia) alipowasili katika ofisi za ESRF jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa
Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak.(Picha na Modewjiblog)
Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak.(Picha na Modewjiblog)
Taasisi ya utoaji mafunzo ya Ufaransa ya AFPA ndiyo ilikuwa inaendesha mafunzo hayo wakibadilishana uzoefu na wadau wa Tanzania kutoka sekta binafsi.
Akifafanua zaidi Dkt. Kida alisema kwamba kongamano hilo limelenga zaidi katika kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto zinazojitokeza na fursa zilizopo katika mafunzo, ukuzaji na uendelezaji taaluma.
Dkt. Kida alifurahishwa na mchanganyiko wa watu kutoka sekta binafsi waliofika katika kongamano hilo ambao aliamini kwamba wataelezea uzoefu wao katika kukabiliana na changamoto za taaluma katika makampuni yao.
Aidha alisema kwamba wadau hao wa Tanzania watapata uzoefu wa timu ya wataalamu wanne kutoka kwa wakala wa mafunzo ya taaluma nchini Ufaransa (AFPA) ambao wataeleza miaka 60 ya uzoefu katika masuala ya mafunzo ya taaluma na uendelezaji wa utaalamu.
Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak (kushoto) akibadilishana mawazo na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida katika ofisi za ESRF jijini Dar es Salaam.
Alisema anaamini kwamba mchanganyiko huo wa wadau utasaidia katika kukabiliana na tatizo la taaluma katika soko la ajira la Tanzania.
Alisema mazungumzo hayo ni muhimu sana katika kuibua fursa hasa wakati taifa hili linajipanga kuelekea katika uchumi wa kati wa viwanda na bila wataalamu wenye taaluma zao makamapuni na viwanda vingi vitakuwa na shida kubwa.
Alisema changamoto kubwa inayokabili taifa la Tanzania kuelekea nchi ya viwanda kama ilivyo katika nchi nyingine zinazoendelea ni ukosefu wa taaluma na utaalamu.
“Ukosefu wa wafanyakazi wenye taaluma katika ngazi zote ni tatizo kubwa linalokabili harakati za kuelekea uchumi wa viwanda” alisema Dkt. Kida.
Anasema pamoja na matatizo hayo taasisi yake tayari imeshaanza kushughulikia shida hiyo ya taaluma nchini Tanzania kwa kuwa na makongamano mbalimbali makubwa yanayokutanisha wadau kuzungumzia hali hiyo.
Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak (kulia) akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero (kushoto) alipowasili ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (katikati) kabla ya kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano.
Alisema kwa mfano mwaka 2015 iliendesha jukwaa la mafunzo ya ufundi (VTEC) Africa. Katika jukwaa hilo lililofanyika Machi 10 -12 mwaka huo walizungumzia mafunzo ya utaalamu wa gesi na mafuta kwa mataifa ya Afrika. Jukwaa hilo liliendeshwa kwa kushirikiana na kampuni ya Uingereza ya Getenergy.
Aidha Oktoba 9, 2015 iliendesha semina kuhusu uumbaji wa programu za mafunzo kwa aili ya kupata wataalamu wa gesi na mafuta.
Lakini, alisema, kuanzia Julai 2014, ESRF imekuwa ikishirikiana na shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kutekeleza mpango wa miaka mitano wa mafunzo ya kinadharia na utaalamu yenye mfumo wa Ushiriki ambapo ESRF yenyewe hutoa msaada wa kitawala na lojistiki kwa wanafunzi ili waweze kwenda kuhudhuria mafunzo nje ya nchi.
Aidha ESRF imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali na uchambuzi kuhusiana na uendelezaji wa taaluma nchini Tanzania na moja ya ya tafiti hiyo ni kudorora kwa ubora wa elimu Tanzania na namna ya kuzuia anguko hilo na kulibadili.
Mwaka 2014 na mwaka huu kuna mada inayozungumzia uendelezaji wa mafunzo ya taaluma na uwezo wa uzalishaji Tanzania.Mada hii ni sehemu ya taarifa ambazo zitapatikaa katika ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2017.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kulia) akiongozana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano wa ESRF. Nyuma ni Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak akibadilishana mawazo na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi pamoja na Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ally Msaki.
Naye Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berack amesema kwamba kuwapo kwa taasisi hiyo ya Ufaransa kushea elimu na watanzania kutasaidia kuinua na kuboresha fursa za maendeleo hasa rasilimali watu katika utaalamu.
Alisema AFPA yenye uwezo wa miaka mingi katika kuendesha mafunzo ana tumaini itasaidia kuamsha ushindani na kuziba mapengo ya wafanyakazi wataalamu katika nafasi mbalimbali.
Aidha alitoa wito wa kuwapo kwa sera ambapo Tanzania na Ufaransa zitashirikiana kuhakikisha kwamba kunakuwapo na mwendelezo katika suala la utaalamu na taaluma kwani hiyo ndiyo inayoweza kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya viwanda.
Alisema AFPA yenye wataalamu zaidi ya elfu 80 wakiwa wamebobea katika uandazi wa watu wanaotafuta kazi, kufundisha utaalamu na pia kuwezesha ushindani katika masuala ya biashara wataweza kusaidia watanzania kudadavua matatizo yao na kujiweka mbele katika kufanya mabadiliko ya kiuchumi na kitamaduni ili kusonga mbele.
Naye Dkt. Reginald Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa makampuni ya IPP na Mwenyekiti wa TPSF alisema kwamba mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo serikali imetoa mpango wake wa maendeleo wa miaka mitano ambao utekelezaji wake unategemea sana utaalamu na taaluma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki na wadau wengine katika kongamano hilo.
Alisema kwamba wakati serikali inajipanga taifa kuwa na uchumi wa kati mwaka 2025 taifa linatakiwa kujipanga katika kutengeneza rasilimali watu wenye taaluma ambao wanaweza kulifikisha taifa katika eneo hilo.
Alisema kwamba katika hali hiyo inafaa kuendelea kuratibu na kutengeneza mitaala inayofaa kwa ajili ya kuendeleza watu na hivyo kuendeleza taaluma kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Inafaa, alisema Dk Mengi, utengenezaji wa watu wenye taaluma lazima uende sambamba na haja ya taifa katika mipango yake ya maendeleo kwa kutoa wataalamu walio bora ambao watatengeneza bidhaa bora na huduma bora zitakazoinua uchumi wa mtu mmoja na taifa.
Alisema ipo haja ya kuwapo kwa ushirikiano wa sekta binafsi na serikali katika kuhakikisha mazingira yanawezesha uzalishaji zaidi wa wataalamu ambao watakuwa na uhakika na ubunifu wa kuendeleza teknolojia na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo.
Alisema awali uchumi ulitengenezwa kwa kuzingatia ujamaa ambapo serikali ilikuwa inafanyabiashara na kuzalisha lakini baada ya mabadiliko inatakiwa vile vile kubadilika ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa ambayo ni ya soko huria.
Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak akizungumza kwenye kongamano hilo.
Aliwataka watanzania kubadilika katika fikira zao na kuona namna ya kuwezesha maendeleo ya rasilimali watu kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ambayo yanahitaji utaalamu wa sasa hasa katika sekta binafsi.
Alisema ni lazima watu pia katika taaluma lazima kuwepo na uwajibikaji, uadilifu na uwezo katika kufanikisha maendeleo ya taaluma.
Akitolea mfano wa mtu aliye mlemavu nchini Japan alitaka watanzania watumie kile kilichopo tunachoweza ili kutengeneza maisha bora kabisa.
Alisema mlemavu huyo wa Japan ambaye alikuwa amepooza kuanzia shingoni ambaye kwa sasa ni milionea alimwambia kwamba alikuwa halilii ambavyo hana bali kile alichonacho alihakikisha anakitumia vyema.
Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi akifungua kongamano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ofisi za ESRF jijini Dar es Salaam.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi na Ajira, Eric Shitindi katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ally Msaki alisema ipo haja ya wadau wote kuwa pamoja katika kuhakikisha elimu inaboreshwa na pia wataalamu wanasukwa kwa kuzingatia soko la ajira.
Alisema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imechukua hatua kadha kuongeza utaalamu katika soko la ajira kwa kuanzisha mpango wa miaka mitano ambamo ndani yake yamezungumzwa masuala ya mafunzo ya ufundi na utaalamu .
Alisema hakuna maendeleo yanayokusudiwa bila kuwa na wataalamu na hivyo serikali itaendelea kushirikiana na wadua mbalimbali kuendeleza mafunzo kwa lengo la kusaidia soko la ajira.
Alisema bila kuwa na ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na waajiri hapatakuwapo na wataalamu na hivyo itakuwa shida katika maendeleo ya taifa.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (wa pili kushoto) na washiriki wengine wakifuatilia kwa umakini risala ya mgeni rasmi, Dk. Mengi.
Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ally Msaki akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi na Ajira, Eric Shitindi katika kongamano hilo.
Pichani juu na chini ni sehemu ya washiriki kutoka sekta binafsi, serikalini pamoja na taasisi mbalimbali walioshiriki kwenye kongamano hilo.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Tonia Kandiero akichangia maoni kwenye kongamano hilo.
Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kulia), akibadilishana mawazo na Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kushoto) pamoja na kurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ally Msaki wakati wakielekea kwenye eneo maalum kwa ajili ya zoezi la picha ya pamoja.
Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi katika picha ya pamoja na wakala wa mafunzo ya taaluma nchini Ufaransa (AFPA) na wadau waliowezesha kongamano hilo kufanyika.
Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa kongamano hilo.
Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kushoto) akifurahi jambo na Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak (wa pili kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (katikati) pamoja na Prof. Prosper Ngowi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kulia) akiagana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Tonia Kandiero mara baada ya kumalika kwa kongamano hilo.
No comments:
Post a Comment