Thursday, December 22, 2016

KATIKA KUSHEREHEKEA SIKUKUU YA KRISMAS MULTICHOICE TANZANIA YAWAKUMBUKA YATIMA WA KITUO CHA AL-MADINA JIJINI DAR ES SALAAM

 Wafanyakazi wa Kampuni ya Multichoice Tanzania na wanahabari wakiwa ndani ya gari wakienda kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Al-Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam leo.
  Wafanyakazi wa Kampuni ya Multichoice Tanzania wakiwa wamebeba zawadi kuelekea kwenye kituo hicho.
 Baadhi ya wanahabari wakisubiri kuchukua taarifa hiyo.
 Viroba vyenye chakula na zawadi mbalimbali vikipangwa vizuri tayari kwa makabidhiano.
 Wafanyakazi wa Multichoice Tanzania na watoto Yatima wa kituo hicho wakiwa mbele ya shehena  za zawadi kabla ya makabidhiano.
 Ofisa wa kampuni ya Multichoice Tanzania, Johnson Mshana (kulia), akizungumza wakati akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo kabla ya kukabidhi msaada huo.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande (kulia), akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo. Kushoto ni mama mlezi wa kituo hicho, Kuluthum Yusuf.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande (kushoto), akimkabidhi sare za shule mama mlezi wa kituo hicho, Kuluthum Yusuf.

 Bwana Chande akimkabidhi mlezi wa kituo hicho mafuta ya kula. Wengine ni wafanyakazi wa Multichoice Tanzania na watatu kushoto ni Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Alpha Joseph.
 Watoto wa kituo hicho wakishangilia baada ya kukabidhiwa msaada huo.
Mlezi wa kituo hicho, Kuluthum Yusuf (kushoto), akimuonesha nguo zinazotengenezwa na kituo hicho kupitia mradi wao wa ushonaji ambao kwa kiasi kikubwa umetokana na msaada kutoka katika kampuni hiyo ya Multichoice Tanzania.

Na Dotto Mwaibale

KAMPUNI ya Multichoice Tanzania imetoa msaada wa vyakula, nguo na sare za shule katika Kituo cha kulelea watoto Yatima cha Al-Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande alisema kampuni yao imekuwa jirani na kituo hicho katika kuwafariji watoto wanaolelewa kwenye kituo hicho kwa muda mrefu.

Alisema vifaa hivyo vyenye thamani ya sh.milioni 5 ni 
 vyombo vipya vya kulia chakula, nguo, vyakula, sare za wanafunzi wa shule za msingi, vifaa mbalimbali  kwa ajili ya mahitaji ya kila siku na fedha taslimu za kusaidia kwenye gharama za kodi.

Alisema lengo la ziara hiyo ya kutoa msaada katika kituo hicho ilikuwa ni kuwapa fursa watoto hao katika kusherehekea Sikukuu za mwishoni mwa mwaka kama krismas na mwaka mpya ili nao wajione kama walivyo watoto wengine waliopo kwenye familia zao.

Chande alisisitiza juu ya umuhimu wa kushirikiana na kituo hicho katika kuwawezesha watoto kusonga mbele kwani ndiyo taifa la kesho na akatoa mwito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia watoto hao.

Mama mlezi wa kituo hicho, Kuluthum Yusuf aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo na kueleza kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni upatikanaji wa ada kwa watoto wanaosoma shule za kulipia, nyumba ya kuishi watoto hao pamoja na chakula.  

Multichoice Tanzania imekuwa ikisaidia kituo hicho tangia mwaka 2009 mpaka sasa. 

No comments: