Saturday, October 21, 2017

Watoto wafanyakazi wa nyumbani Jijini Mwanza wachagua wawakilishi

Binagi Media Group
Watoto wafanyakazi wa nyumbani kutoka Kata za Jiji la Mwanza ambao wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya utambuzi na Shirika la WOTESAWA, jana wameunda uongozi kwa ajili ya kutetea haki na maslahi ya watoto wenzao.

Viongozi hao kutoka kila Kata watakuwa na jukumu la kutoa elimu ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto wafanyakazi wa nyumbani ikiwemo wa ukatili wa kingono, kipigo na utumikishwaji pamoja na kutoa taarifa katika ngazi husika pindi wanapobaini mwenzao kakumbana na ukatili.

“Hakikisheni mnakuwa sauti ya wenzenu, mnakuwa sauti za watoto wenzenu ambao wamefungiwa kwenye mageti na hawana sauti. Mkiona mtoto mdogo ananyanyaswa hakikisheni mnatoa taarifa ngazi mbalimbali ikiwemo shirika la WoteSawa ama kwa viongozi wa serikali za Mitaa”. Alisisitiza Angel Benedicto ambaye ni Mkurugenzi wa WOTESAWA, Shirika la Kutetea Haki za Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani.

Viongozi waliochaguliwa waliahidi kufichua vitendo vya ukatili katika jamii na kwamba watatumia vyema fursa waliyoipata kusambaza elimu waliyoipata kwa waajiri wao pamoja na watoto wafanyakazi wenzao katika mitaa yao ili kutokomeza ukatili katika jamii.

Viongozi hao walitoka Kata mbalimbali Jijini Mwanza ikiwemo Mkuyuni, Isamilo, Capripoint, Kirumba, Pasiansi, Butimba, Igogo, Buhongwa na Mkolani ambapo pia watakuwa ni wawakilishi wa watoto wafanyakazi wa nyumbani katika shughuli mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa WOTESAWA, Angel Benedicto akizungumza kwenye semina hiyo jana
Mkurugenzi wa WOTESAWA, Angel Benedicto
Viongozi wawakilishi wa watoto wafanyakazi wa nyumbani kutoka Kata mbalimbali Jijini Mwanza wakimsikiliza Mkurugenzi wa WOTESAWA, Angel Benedicto
Viongozi wa serikali za mitaa Jijini Mwanza ambao ni marafiki wa watoto wafanyakazi wa nyumbani Jijini Mwanza wakiwa kwenye semina hiyo
Bonyeza HAPA kusoma zaidi

No comments: