Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa uzinduzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45, Leo Jumamosi 10 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akikata utepe ishara ya uzindua wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45,
Leo Jumamosi 10 Machi 2018.
Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akimshuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule na vituo vya afya Wilayani bukombe wakati wa dhifa ya uzinduzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45, Leo Jumamosi 10 Machi 2018.
Mamia ya wananchi Wilayani Bukombe Mkoa wa Geita wakimlaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli mara baada ya kuzindua barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45, Leo Jumamosi 10 Machi 2018.
Na Mathias Canal, Ushirombo-Geita
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe
Magufuli Leo Jumamosi 10 Machi 2018 amezindua rasmi barabara ya Uyovu-Bwanga
yenye urefu wa kilomita 45 ambayo imekamilika kwa kujengwa kwa kiwango cha
lami.
Katika dhifa hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Runzewe Kata ya
Uyovu Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ni
nchi ya tano kwa ukuaji wa uchumi barani Afrika hivyo wananchi wanapaswa
kuwapuuza wanasiasa wanaohubiri kuporomoka kwa uchumi kwa matakwa ya kujiimarisha
kisiasa.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili serikali imefanya kazi
kubwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta mbalimbali kwa usimamizi nzuri katika
rasiliamali Madini, kuboresha sekta ya elimu ambapo wanafunzi wanasoma bure
kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.
Alisema kuwa, bajeti ya mwaka 2015 katika sekta ya afya ilikuwa
ni Bilioni 31 lakini serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha afya za
watanzania ambapo sasa bajeti imefikia shilingi Bilioni 239 na hayo ni matokeo
ya umoja na amani iliyopo nchini.
Rais Magufuli amesema amani iliyopo nchini Tanzania imejengwa
chini ya uasisi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikasimamiwa vyema
na marais wastaafu Mhe Ally Hassan Mwinyi, Mhe Benjamin Mkapa pamoja na Mhe
Jakaya Mrisho Kikwete.
"Mambo yanayofanywa na serikali hayawezi kuyafurahisha
mataifa mengine hivyo mataifa hayo yanawatumia watanzania wenyewe kutengeneza
chuki dhidi ya serikali yao" Alikaririwa Rais Magufuli
Aliongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo imekuwa sehemu ya Kuchochea
shughuli za maendeleo ya kijamii katika usafirishaji wa mazao, kurahisisha
usafirishaji wa watu na bidhaa, sambamba na kuongeza pato la Mkoa wa Geita
na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Rais Magufulu amewasihi wananchi Kutovamia
hifadhi za Taifa badala yake kuwa wavumilivu na kuiacha serikali ifanye, kwani
watatumwa wataalamu wa Wizara ya ardhi na maliasili ili kuratibu na kuona namna
ya kuyagawa maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe Elius John Kuandikwa
na Mtendaji Mkuu wa Tanroads nchini Mhandisi Patrick Mfugale walisema
kuwa usanifu wa barabara hiyo ulifanywa mwaka 2006 na kampuni mbili za
kitanzania kwa jumla ya Shilingi Milioni 207.6 ambapo barabara hiyo imesanifiwa
kubeba na kutumika kwa miaka 20 kwa upana wa mita 9.5
Walisema Ujenzi wa barabara hiyo uliokamilika Octoba mwaka jana
umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 45.454, ambapo msimamizi amelipwa shilingi
Bilioni 2.3 huku akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi mwezi
Octoba mwaka huu.
Dhifa ya uzinduzi wa barabara hiyo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa
wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, Naibu Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na
mawasiliano, Mhe Elius John Kuandikwa, Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini
Mhe Doto Mashaka Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Tanroads
Mhandisi Patrick Mfugale.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment