Tuesday, July 10, 2007

'WAKANDAMIZAJI' WAZUA KASHEHE ZENJI!


(Tanzania - July 11, 2007)
Na Mwandishi Wetu aliyekuwa Zanzibar

Warembo wawili waliofahamika kwa jina mojamoja la Amina na Mwanaidi pichani ukurasa wa mbele, hivi karibuni walijikuta wakipigana kuwagombea wasanii wa Kundi la Sanaa la Ze Comedy, Luca Mhuvile ‘Joti au Ami J’ na Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji,’ katika kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Tukio hilo lilitokea Ijumaa ya wiki iliyopita katika eneo la Ngome Kongwe kwenye Tamasha la miaka 10 ya nchi za Majahazi ambapo wasanii hao walikuwa ni miongoni mwa vikundi vilivyotumbuiza.

Mwandishi wetu ambaye alikuwepo katika eneo hilo, aliwashuhudia wasichana hao ‘wakitiana mkononi’ kufuatia ubishi mkubwa uliojitokeza baina yao baada ya mmoja wao kufuma meseji kwenye simu ya mwenzake ‘ikiingilia anga zake’.

Ilidaiwa na rafiki wa karibu na warembo hao ambaye naye alikuwepo kwenye ukumbi huo kuwa, kila mmoja wa warembo hao alifanikiwa kupata namba ya simu ya Joti na Masanja kwa nyakati tofauti wakati walipoingia visiwani humu.

Baada ya kupata namba hizo, habari zinasema kuwa wasichana hao walikusudia kuwapigia simu ili waweze kuonana nao baada ya kumaliza maonesho yao.

Habari zilidai kuwa wasichana hao kila mmoja alipanga kumtafuta msanii wake aliyemhusudu ili awe naye kimapenzi, lakini wakiwa nyuma kabisa ya uwanja huo wakitazama vichekesho vyao huku wakipata kilevi, Amina alimuachia simu Mwanaidi na kuaga kwenda msalani.

Akiwa na simu ya mwenziwe, Mwanaidi aliipekuwa na kukuta meseji iliyodaiwa kutumwa kwa Joti ikimtaka amtafute baada ya kumalizika kwa onesho lao.

Habari zinasema kuwa Amina aliporejea kutoka msalani alikabidhiwa simu yake ambapo Mwanaidi alimuuliza sababu ya kutuma ujumbe kwa Joti ambaye alikuwa chaguo lake.

Chanzo hicho kilidai kuwa, Amina alikanusha kutuma ujumbe huo na ndipo wakaanza kurushiana maneno ya kashfa na hatimaye kuanza kurushiana makonde kama wanavyoonekana ukurasa wa mbele ambapo Amina alijeruhiwa jichoni.

Hata hivyo, wasamaria wema waliamua varangati hilo na mmoja kati yao aliyeonekana kumfafamu Amina, alikodoshiwa gari na kupelekwa hospitali ambayo haikuweza kufahamika mara moja.

Joti alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu warembo hao kutwangana makonde kwa ajili yao, alisema kuwa hafahamu. “Umesema kugombewa kwa mabaya au mazuri? Kama ni kwa mazuri basi ni mambo ya kawaida tu hayo,” alisema msanii huyo na kukata simu.

Masanja hakuweza kupatikana kuelezea, kama alikuwa akiwafahamu wasichana hao kwani simu yake haikuweza kupatikana.

Hata hivyo, Joti hakufanya kile ambacho Wazanzibar walitarajia kutoka kwake kwani hakubonyeza kizenji wala kuigiza sauti ya wazanzibar waliyoizoea kuisikia kupitia luninga. (KWA WADAU WA NJE; HAWA JAMAA HIVI SASA NDO WASANII WALIO 'MATAWI YA JUU' KULIKO WASANII WENGINE WOTE BAADA YA KIPINDI CHAO CHA VICHEKESHO CHA ze comedy KINACHORUSHWA na CHANNEL5 KUKONGA NYOYO ZA WATAZAMAJI).

No comments: