Monday, August 20, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT!

MAJI YANAWEZA KUWEPO PASIPOKUWA NA BINADAMU, LAKINI BINADAMU HAWEZI KUWEPO PASIPOKUWA NA MAJI!

Kuonesha umuhimu wa maji katika maisha ya binadamu, unaweza kusema maji yanaweza kuwepo hata mahali ambako hakuna binadamu, kwani hayahitaji msaada wowote kutoka kwetu, lakini sisi kamwe hatuwezi kuishi mahali ambako hakuna maji, kwa sababu uhai wetu unategemea maji, hasa ya kunywa, kwani bila hayo hatuwezi kuishi hata kwa wiki moja tu!

Maji ni moja kati ya virutubisho vya mwili muhimu sana. Tofauti na aina nyingine za virutubisho, maji hayana akiba mwilini hivyo tunalazimika kuyanywa kila siku na kila wakati ili kuufanya mwili kuwa na akiba ya kutosha.

Mwili wa wastani wa binadamu wenye uzito wa kilo 72 una kiasi cha asilimia 60 za maji, ambazo ni karibu lita 42. Mtoto mchanga, asilimia 75 ya mwili wake ni maji tu na kwa wazee asilimia hushuka hadi kufikia 50.

Kwa mujibu wa wanasayansi wetu, kiasi cha maji kilichomo mwilini huonekana kwenye nyama za misuli alizonazo mtu. Unaweza kujiuliza lita 42 za maji zinakaa wapi kwenye mwili wa binadamu? Kiasi cha 2/3 ya maji hukaa kwenye seli za mwili (Intra Cellular fluid) na kiasi kingine kilichobaki ni majimaji ya ziada yanayopatikana kwenye damu na mkojo.

Miili yetu hutokwa na jasho kila wakati bila ya sisi kujua, hata wakati wa baridi. Utokaji jasho ni njia mojawapo ya mwili kurekebesha joto lake ambalo zaidi hutokana na maji. Mwili hutokwa na jasho pale unapokuwa unafanyakazi au hali ya hewa inapokuwa ni ya joto.
Mwili unapokuwa na joto jingi ndivyo unavyotokwa jasho, bila kunywa maji ya kutosha kila wakati, hatuwezi kutokwa jasho na iwapo kiwango cha maji kinachohitaji mwilini kitapungua zaidi ya asilimia 10, lazima mtu atapatwa na matatizo ya kiafya yatakayohitaji msaada wa daktari.

JE, TUNAHITAJI KIASI GANI CHA MAJI KWA SIKU?
Mahitaji ya maji mwilini kwa mtu mzima ni kiasi cha mililita 2800. Kiasi kingine cha maji hupotea mwilini kupitia hewa tunayopumua na tunavyoenda kujisaidia haja kubwa, karibu nusu ya maji tunayokunywa hutoka kupitia njia ya mkojo.

Kiasi cha maji kinachotoka mwilini kwa njia ya jasho, kinatofautiana kati ya mtu na mtu, lakini kinatofautiana kati ya nusu lita hadi lita mbili kwa siku, kutegemeana na kazi anazozifanya na hali ya hewa.

Kiwango cha maji kinachoingia mwilini kila siku, karibu nusu lita tunaipata kupitia vyakula vya majimaji tunavyokula, hivyo basi kiwango cha maji anachotakiwa mtu kukinywa kila siku ni lita 2 ambazo ni sawa na glasi nane kubwa na hiki ni kiwango kinachoshauriwa kwa watu wazima ambao shughuli zao ni za kawaida katika hali ya hewa yenye joto.

TUNYWE KINYWAJI GANI?
Kwa kifupi, kinywaji bora zaidi ni maji yaliyo safi na salama. Watu wengi wanaamini kwamba kiwango hicho cha maji kilichotajwa anachotakiwa mtu kunwa kwa siku(lita mbili) ni lazima kiwe cha maji tu. Lakini kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, vinywaji vingine kama chai, juisi na vingine baridi, vikitumika kwa wastani, vinachangia kwa kiasi fulani kuongeza kiwango cha maji mwilini.

Aidha, matunda nayo huchangia kiasi kikubwa cha maji mwilini, hasa matunda yenye asili ya maji maji, kama vile machungwa, mapapai, n.k. Kwa maana nyingine ukiwa mlaji mzuri wa matunda na vinywaji vingine baridi una uhakika wa kuwa na maji mwilini yatakayosaidiwa na maji mengine utakayoyanywa kawaida. Vinywaji baridi vizuri ni vile ambavyo havijaongezewa sukari.

Ni vizuri mtu kupenda kunywa vitu vya majimaji kila wakati pamoja na chakula au katikati ya chakula. Kwenye nchi zenye joto kali, kiwango kilichotajwa hupaswa kuongezwa zaidi ili kufidia upungufu unaoweza kujitokeza kutokana na mwili kutokwa na jasho jingi.

Kumbuka maji ni uhai, bila maji hakuna kitu kinaweza kufanyika ndani ya mwili wa binadamu, ndiyo maana hata mgonjwa mahututi, huduma ya kwanza ya haraka anayopewa huwa ni kuongezewa maji mwilini kwanza! Unywaji maji hakukugharimu sana, lakini kutokunywa kunaweza kukugharimu sana!



No comments: