Monday, August 20, 2007

‘NIMETISHIWA KUPIGWA RISASI'

Dk. Wilbroad Slaa (katikati), ambaye ni Mbunge kwa tiketi ya Chadema na ambaye anadai kutishiwa kuuawa, akiteta na kiongozi wake Mbowe (kushoto) huku kamanda wao Zito Kabwe akiwasikiliza kwa makini kabla ya kuhutubia maelfu ya watu waliojitokeza Jangwani kumsikiliza Jumamosi iliyopita (soma habari kamili ifuatayo na angalia picha zaidi).

Na Elvan Stambuli
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa amesema ametishiwa kuuawa kwa kupigwa risasi. Dk. Slaa aliyasema hayo Jumamosi iliyopita katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi maalum ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliyesimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge mpaka mwakani kutokana na hoja yake ya kuhoji mkataba wa madini uliotiwa saini nchini Uingereza na Waziri wa Madini na Nishati, Nizar Karamagi.

Akifafanua zaidi Dk. Slaa alisema ujumbe huo wa vitisho ulimfikia kwa njia ya simu yake ya kiganjani.

"Sikwenda kuripoti polisi kwa sababu aliyenitishia kuniua simu yake ilikuwa imeandika 'private', hivyo kutomjua mtu aliyenitolea vitisho hivyo wala namba yake". alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa anaamini amepewa vitisho hivyo kutokana na kugundua kwake kuwa kuna makampuni (majina tunayahifadhi) yamepoteza fedha za serikali alizodai kufikia shilingi bilioni 131.

Aidha alidai kuna kampuni moja ilikopeshwa shilingi bilioni 31 huku kampuni nyingine ambayo hakuitaja jina lakini ya kisheria alisema ililipwa shilingi bilioni 8 kitu ambacho hakikutakiwa. Alifafanua kwamba kampuni hiyo ilitakiwa ilipwe shilingi bilioni 1.5

"Nchi hii haina wenyewe, ndege ya uchumi inayopaa aliyoisema Waziri Mkuu ni yao sio yetu," alisema Dk Slaa na kushangiliwa na wananchi waliokuwa hawajali kunyeshewa mvua iliyokuwa ikinyesha kwa nguvu.
Akifafanua sababu ya kuchomoa hoja binafsi katika kikao cha bunge lililomalizika wiki iliyopita, kiongozi huyo wa CHADEMA na Mbunge wa Karatu alisema alifanya hivyo baada ya kuona itikadi za kisiasa zinatumika zaidi hivyo kugundua kuwa hatatendewa haki.

Alisema alimuandikia barua Spika wa Bunge, Samueli Sitta na kumtaarifu kuwa anaondoa hoja yake lakini atatafuta njia mbadala wa kushughulikia ubadhirifu wa Benki Kuu ya Tanzania.

Akimgeukia Rais Jakaya Kikwete, Dk. Slaa alisema inawezekana dhamira yake haipo moyoni. "Inawezekana dhamira ya Rais Kikwete haipo moyoni, haiwezekani anapelekewa majina ya waliotumia shilingi bilioni 1.5 na mkaguzi mkuu wa serikali katika ripoti yake na asichukue hatua." alisema.

Aliongeza kuwa yupo tayari kufa kwa kushughulikia jambo hilo, hivyo alimkabidhi jalada lenye nyaraka za tuhuma hizo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe (pichani chini, kushoto) ili jambo hilo lishughulikiwe na viongozi wa kisiasa.

Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya jinai nchini, Bw. Robert Manumba amelithibitishia gazeti hili kwa kutoa tamko kuwa Dk. Slaa hajaripoti tukio la kutishiwa kuuawa katika jeshi lake, Hata hivyo aliahidi kwamba akiripoti tukio hilo polisi watalishughulikia.

1 comment:

Anonymous said...

Naupongeza sana ujasiri alionao kijana mwenzetu Zito kabwe ni dalili tosha kuwa sasa vijana tunaweza kishika madaraka na hilo ni wajibu wazee aliokuwa vilaza kipindi cha ujana wao mpaka leo ni vilaza tu tuamke vijana tutajibu nini mbele za mungu tumeutumiaje ujane wetu? tabia za starehe na ngono tuwaachie wazee walishamiliza deni lao
sisi kwa mbinu yeyote tuitoe tanzania katika umaskini uliopindukia
wabunge wetu hawana hekima sina ushahidi likini ni wangapi walifahamu swala la alilodokeza Mh. kabwe kabla?
lakini hawaoni ushupavu huo bado wakapigakura asurubiwe huo ni unafiki.

watanzania tuamke tuache ushabiki wa kijinga lazima tuongeze nguvu ya upande wa upinzani tuinyooshe serikali bila hivyo tutalia kilio cha samaki