Monday, August 20, 2007

MKE WA MTU AFUMWA AKIJIUZA, MTOTO MIKONONI, TOBA!

Makongoro Oging na Richard Bukos
Mwanamke mmoja aliyekuwa na mtoto anayedadiriwa kuwa na umri wa miezi sita, ambaye anadaiwa kuwa ni mke wa mtu, ametiwa mbaroni usiku wa manane wiki iliyopita na askari wa Manispaa ya Ilala kwa kile kinachodaiwa alikuwa akijiuza kwa wanaume, Uwazi limeshuhudia sakata zima.

Tukio hilo lilitokea maeneo ya Buguruni karibu na maeneo ya Baa ya Kimboka katika zoezi maalum lililokuwa likiendeshwa na askari hao kufuatia wimbi kubwa la wanawake, wakiwemo wanafunzi, kujiingiza katika biashara haramu ya kuuza miili.


Akiongea na waandishi wetu katika eneo la tukio lililonaswa na kamera zetu, Afisa Mtendaji wa Kata ya Buguruni, Bw. Alphonce Msenduki alisema mwanamke huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, ni miongoni mwa watu 19 waliokamatwa katika zoezi hilo na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Buguruni.

Aidha alisema kuwa kati ya hao waliokamatwa wanawake walikuwa 17 na wanaume wanaodaiwa ni wateja wa biashara hiyo haramu, walikuwa wawili.

Aidha, afisa huyo alifafanua kuwa hali ya ukahaba ni mbaya katika eneo lake, hasa maeneo ya karibu na Baa ya Kimboka, Sewa, Achimwene, Kimvulini na kituo cha daladala cha Rozana.

Aliendelea kusema, kwa kuwa kumekuwa na mchanganyiko wa wanawake wanaojiuza, wakiwemo watu wazima na watoto wenye umri kati ya miaka 11 hadi 17, ambao baadhi yao wanadaiwa kuwa ni wanafunzi, wamelazimika kuendesha oparesheni maalum kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinachangia maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Alisema kuwa watakuwa wanaendelea na utaratibu huo wa kuwakamata wanaojihusisha na biashara hiyo ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi hivyo, kwa lengo la kulinusuru taifa.

"Hawa watu wanakera sana, kwani wengi wao wamekuwa wakivamia kwenye mabaa na kusumbua wateja hali ambayo inasababisha wamiliki wa baa hizi kuona wanazivunjia heshima,” alisema afisa mtendaji huyo.

Aliendelea kusema kuwa wanawake wanaojiuza katika eneo lake wameongezeka baada ya kutimuliwa Uwanja wa Fisi huko Manzese wilaya ya kinondoni.

Alielezea zaidi kuwa wote waliokamatwa walitarajiwa kufikishwa mahakama ya jiji mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Naye mmiliki wa Baa ya Kimboka aliyejitambulisha kwa jina moja la Bw. Kimboka, alisema kuwa wanawake hao wanaojiuza wamevamia baa yake na kila wanapoondolewa na walinzi wake, hukimbilia polisi kutoa taarifa kuwa wamepigwa na kusababisha walinzi wake kukamatwa.

"Ila sasa naishukuru ofisi ya kata hii ya Buguruni, tangu zoezi la kuwakamata lifanyike, sasa wamepungua, " alisema Kimboka.

Shuhuda mwingine aliyeshuhudia kamatakamata hiyo, Bi Frida Chale, alisema kuwa anasikitishwa na kitendo kilichofanywa na mama huyo cha kwenda katika mawindo hayo haramu akiwa na mtoto mchanga.

Alisema kitendo hicho kinamuumiza mtoto kwa baridi huku akiwa hana hatia, hivyo kuweza kumsababishia maradhi kama nimonia.

Aliishauri serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, kuwa na utaratibu wa kuwahudumia watoto ambao wazazi wao huashiria kushindwa kuwalea, kama ilivyoonekana kwa mwanamke huyo aliyekamatwa kwa madai ya kujiuza.

Alisema nchi zingine duniani huwa na utaratibu wa kuokoa maisha ya watoto walio hatarini kutokana na matunzo duni wanayopewa na wazazi wao.

1 comment:

Anonymous said...

Oh my God!! Dunia imekwisha.....yaani ni hali nya uchumi kuwa mbaya au nini?? Sasa kwenda na mtoto kujiuza..