Monday, September 17, 2007

Wakenya wamshika JK pabaya!


Na Goodluck Eliona

kufuatia mlipuko wa ujambazi unaofanywa na raia wa Kenya kwenye mikoa ya kaskazini mashariki mwa Tanzania, wananchi wamesema kuwa hali hiyo ni sawa na kumshika pabaya Rais Jakaya Kikwete ‘JK’.

Wakiongea na Ijumaa Wikienda, mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, wananchi hao walisema, kitendo cha Wakenya kuifanya Tanzania kama sehemu ya kuchota pesa za bure ni uchokozi usioweza kuvumilika. “Tumeshasikia JK amesema hawezi kuwavumilia Wakenya kwa tabia yao ya kuja kufanya uhalifu Tanzania, tunataka vitendo, kukabiliana na majambazi hao,” alisema Judith Kalolo wa Tabata.

Judith aliongeza, Wakenya wameshawaona Watanzania kama watu wasio na akili timamu, kitu ambacho kinawapa kiburi cha kufanya watakavyo. Shaban Haidu wa Mwananyamala alisema, kuwabaini Wakenya hivi karibuni, imekuja baada ya raia wa nchi hiyo jirani kufanya uhalifu kwa wingi hapa nchini. “Wameanza siku nyingi lakini walikuwa hawajagundulika, kwahiyo ni watu hatari sana, wana mbinu nyingi na endapo tusipowadhibiti watatuweka roho juu, kila siku,” alisema Haidu.

“Siku hizi wamekuja na kila mbinu ya kutupiga changa la macho, wameanzisha tabia ya kuwatumia watu sms, wanawaambia wameshinda milioni moja ya Kenya. “Wanasema bahati nasibu ilichezeshwa na Kampuni ya East Africa Breweries, ukikubali, wanakuomba uwatumie vocha ya simu ya shilingi 100,000 kwanza, halafu uende Kenya uchukue hela yako, ukiwatumia umeliwa,” alisema Yoranda John wa Mabibo.

Aidha, Yoranda alionesha sms aliyodai kutumiwa na Wakenya, waliomtapeli vocha ya simu yenye thamani ya shilingi 100,000 za Kitanzania ambayo inasomeka hivi; “You have won 1,000,000 Kshs, from our draw of east african breweries. Please call us back for more information through this number +255 763 733 964.”

Tafsiri: “Umeshinda shilingi 1,000,000 za Kenya, kupitia mchezo wa bahati nasibu ya East African Breweries. Tafadhali tupigie kwa maelezo zaidi, kupitia namba +255 763 733 964.” Wiki za hivi karibuni, Jeshi la Polisi Tanzania limekuwa kwenye mapambano na majambazi kutoka Kenya ikiwa ni sehemu ya kuwadhibiti wasifanye uhalifu. Tukio kubwa ni lile la Polisi wa Moshi, kuua Wakenya 14 ambao walikutwa na bunduki tatu aina ya AK47, makoti matano kuzuia risasi (bullet proof), bastola tatu, risasi 152 za AK47 na 55 za bastola.

Wiki iliyopita, Polisi Arusha waliwakamata Wakenya wengine watatu, wakiwa na mashine maalumu za kutengenezea kadi bandia za kuchukulia pesa kwenye ATM na zile za kufungulia milango maalumu katika Benki ya Barclays. Akiuongelea uhalifu huo, Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu alisema wiki iliyopita kuwa Jeshi la Polisi linahitaji ushirikiano na wananchi ili kukomesha ujambazi huo wa Wakenya. Mwapachu aliyasema hayo, alipokuwa akiwahutubia wananchi kwenye Kituo cha Polisi, Mererani Arusha.

No comments: