Tuesday, September 4, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT!

NANASI: Mdhibiti wa
saratani na ukosefu wa choo

Awali ya yote, nachukua fursa hii kuwapongeza wasomaji wangu wa wiki iliyopita wa makala ya tunda aina ya Epo. Kulikuwa na makosa ya tafsiri ya tunda hilo kwa lugha ya kiswahili, ambapo mimi nililiita tunda hilo kama Shufaa badala ya Tufaha. Napenda kuomba radhi kwa kosa hilo na nashukuru kwa wale walioliona na kuamua kunisahihisha.

Leo tunazungumzia faida za kiafya za tunda lingine maarufu, Nanasi au kwa lugha ya kiingereza Pineapple. Tunda hili ambalo hapa nchini linapatikana kwa wingi maeneo ya ukanda wa pwani ya Bagamoyo, ni tunda lenye faida nyingi mwilini na upatikanaji wake ni rahisi, bei yake inaanzia shilingi 100 kwa kipande hadi shilingi 1,000 kwa nanasi zima.

Kwa maana nyingine hakuna sababu ya msingi inayoweza kumfanya mtu ashindwe kula tunda hili kwa kipindi chote cha msimu au mwaka mzima. Tunda hili linaweza kuliwa kwa kutengeneza Juice au kwa kula zima na ladha yake ni tamu hata bila kuweka sukari ya ziada, kwani sukari ya asili iliyomo inatosha.

FAIDA ZA KIAFYA ZA NANASI
Awali ya yote, nanasi lina faida kubwa za kiafya katika kupambana na matatizo ya maumivu mwilini na ukosefu wa choo. Lina kirutubisho kimoja muhimu sana kinachojulikana kama Bromelain ambacho hupatikana kutoka katika shina na nyama za nanasi. Miongoni mwa dazeni kadhaa za protini zinazopatikana kwenye nanasi, ni pamoja na vimeng'enyo (Enzymes) vinavyosaidia usagaji chakula tumboni.

Hapo awali, watafiti waliamini kwamba vimeng'enyo hivyo vina faida kubwa za kiafya katika mwili wa binadamu na kwamba dawa nyingi za kuongeza lishe mwilini zilitengenezwa kutokana na nanasi, halikadhalika iliaminika kwamba nanasi husaidia tu matatizo ya utumbo kushindwa kusaga chakula, lakini hivi sasa wamegundua faida zake ni nyingi.

Katika hali ya kawaida mtu mwenye matatizo ya kufunga choo kwa muda mrefu, akila nanasi hupata choo kirahisi, ingawa kisayansi haijaweza kuthibitishwa. Ili kupata faida na matokeo yanayotarajiwa ya nanasi, kula kiasi kikubwa cha nanasi asubuhi kabla ya kula kitu kingine.

NANASI NI KINGA YA MAGONJWA NA HUONGEZA KINGA MWILINI
Nanasi ni chanzo kizuri cha Vitamini C ambayo nayo ni muhimu sana katika kupambana na maadui nyemelezi ambao hufanya uharibifu katika seli za mwili pale panapokuwa hakuna kinga. Wavamizi hao, au kitaalamu wanajulikana kama Free Radicals, ndiyo huwa chanzo cha magonjwa mengi mwilini.

Ukweli huo utaelezea kwa nini Vitamin C imekuwa muhimu sana katika kuzuia na kupunguza kabisa magonjwa kama maumivu ya mwili na matatizo mengine. Vile vile Vitamin C ni muhimu sana katika kusaidia uendeshaji wa mfumo wa kinga mwilini, hivyo kwa wale wanaosumbuliwa mara kwa mara na mafua pamoja na homa, wanashauriwa kuzingatia ulaji wa matunda yenye Vitamin C kwa wingi kama nanasi.
Aidha nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini adimu yajulikanayo kama Manganese, ambayo ni muhimu katika uimarishaji wa vimeng'enyo vinavyosaidia uzalishaji wa nishati ya mwili na kuimarisha kinga yake.

Unywapo glasi moja tu ya juisi ya nanasi, utapata kiasi cha asilimia 128 ya kiwango cha Manganese kinachotakiwa. Mbali ya madini hayo, pia nanasi ni chanzo kizuri cha vitamini mbalimbali jamii ya Vitamini B.

Mbali ya faida zilizoelezwa hapo juu, nanasi lina virutubisho muhimu vya kuzuia au kupambana na uvimbe tumboni na aina za saratani, kwani lina uwezo wa kupambana na adui wanaosababisha kansa mwilini kwa asilimia 30. Hii ina maana kwamba ukiwa mlaji mzuri wa tunda hili, basi unajiwekea kinga ambayo itakulinda na matatizo ya kutokewa na uvimbe tumboni, hasa kina mama.

Kwa mujibu wa daktari aliyeongoza utafiti kuhusu saratani, Dk. Tracey Mynott waTaasisi ya Tiba ya Queensland, virutubisho vilivyomo kwenye nanasi, vina uwezo wa kuzuia kansa ya titi, mapafu, utumbo na kinena.

Aidha, Taasisi ya Saratani ya Marekani inasema kuwa, saratani ni ugonjwa unaoathiri watu wengi hivi sasa nchini humo kuliko magonjwa ya moyo. Matatizo ya saratani huongezeka kadri umri wa mtu unavyoongezeka.

Wiki ijayo tutaendelea na uchambuzi mwingine wa matunda muhimu na yanayopatikana kwenye mazingira tunayoishi na kuendelea kujua faida zake na umuhimu wake katika ustawi wa jamii, tofauti na mazoea yaliyojengeka akilini mwetu kuwa matunda ni anasa tu.

2 comments:

James said...

tufaha sio kiswahili ni kiarabu tafadhari ebu tutafutie jina kiswahili.

Anonymous said...

Habari za kazi kaka Mrisho. Nashukuru sana kwa kutuelimisha. Mimi naomba kuuliza niwahi kusikia kuwa mbegu papai ni dawa kubwa ya minyoo na amiba. Je ni kweli? na ni kweli zinatumiwaje naomba maelekezo.

Dada Izzy.