Thursday, October 11, 2007

VITUKO USWAHILINI!

Binti mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Bilaila, hivi karibuni alijikuta akipata kipigo kikali kutoka kwa mama mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja kwa madai kwamba, amekuwa na tabia ya kupora mabwana wa watu.

Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni katika maeneo ya Manzese Uwanja wa fisi jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na umati wa watu.

Awali wawili hao walisikika wakirushiana maneno makali huku Bilaila akituhumiwa kupora waume za watu.

"Hatukujua hata walikotokea na walivyoanzana lakini kwa jinsi walivyokuwa wanaongea inaonesha Bilaila kamchukulia yule mwanamke bwana wake.

"Baada ya kutukanana kwa muda mrefu ndipo wawili hao walipopandishana hasira na kuanza kutwangana makonde ambapo yule binti alionekana kuzidiwa nguvu, aliumizwa vibaya hadi kupoteza fahamu," alisema shuhuda huyo.

Aidha mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Mama Uledi alidai kumfahamu vilivyo binti huyo na kueleza kuwa, amekuwa na tabia ya kuwaganda waume za watu na kuwafanya wasahau wake na familia zao.

"Mimi namjua fika yule msichana, ni kiwembe kupita maelezo yaani akimzoea tu mumeo jua atamchukua ndiyo maana nimefurahi alivyoshikishwa adabu,” alisema mama huyo.

Hata hivyo ilielezwa kuwa, wawili hao walikuwa mashoga walioshibana lakini ugomvi huo umeufanya umati uliokuwa katika tukio hilo kubaini kuwa, kikulacho kinguoni mwako.

No comments: