Tuesday, October 28, 2008

Dondoo muhimu kwa afya yako

Katika suala la zima la kuwa na afya bora, hiyari iko mikononi mwa mtu mwenyewe. Unaweza kuamua kuishi na afya bora na unaweza pia kuamua kuishi na afya mbaya, uamuzi ni wako. Kama ilivyo kwa jambo lolote, nia, uelewa na kujituma ndiyo huwa siri ya mafanikio, hivyo hata katika suala la afya ni hivyo hivyo.

Mtu kuwa na afya njema siyo jambo linaloweza kuja lenyewe bila wewe mwenyewe kufanya jitihada za kupata maarifa ya kutambua mahitaji ya mwili wako, halikadhalika, kuwa na afya mbaya hakuji kwenyewe, bali huwa ni matokeo ya kutokuzingatia au kutokujua mahitaji ya mwili wako jana, hasa katika suala zima la chakula na mtindo wa maisha unayoishi.

Katika makala ya leo, tutakupa baadhi ya dondoo muhimu zitakazokusaidia kukupa mwanga wa njia bora ya kuishi maisha yenye afya njema kwa kujua hulka ya mwili wako na kufanya kile mwili unataka;

MWILI IMARA
Mwili umetengenezwa ili kufanyakazi na kujishughulisha nyakati za mchana na kupumzika usiku giza linapoingia, ndivyo mwili ulivyoumbwa na ulivyozoea. Ingawa kuna mwanga wa bandia unaoweza kubadilisha usiku ukaonekana kama mchana, lakini viungo ndani ya mwili vinafuata asili yake na huwezi kuvidanya.

Hivyo huna haja ya kushindana na mwili wako, kama una uhuru wa kupanga muda wako, ni vyema kufanyakazi zako mchana na kisha ukalala mapema na kuamka mapema. Hii itaupa mwili nafasi ya kutosha ya kupumzika wakati nishati yake inapokuwa katika kiwango chake cha chini. Utashangaa kiwango cha kazi au michezo utakayoweza kuifanya kwa kuamka asubuhi mapema.

Hapa inasisitizwa kwamba kulala na kuamka mapema ndiyo mwili unavyotaka na ndivyo ambavyo utakavyoweza kufanya kazi au shughuli yako yoyote kwa ufanisi zaidi na bila kuuchokesha mwili.

TIBA MBADALA
Vyakula kama vile matunda, mboga na baadhi ya vyakula vingine vilivyopo jikoni kwako, vina uwezo mkubwa wa kutumika kama tiba mbadala. Ni vizuri kujua uwezo wa kila tunda, mboga au mmea wowote katika kutibu magonjwa madogo madogo kama kichwa, tumbo, mafua, n.k, badala ya kukimbilia matumizi ya dawa kali kali (Anti Biotic).

Kwa matatizo ya mafua na kusikia baridi mwilini, vitunguu swaumu ni dawa nzuri sana. Tengeneza supu ya kuku yenye mchangayiko wa vitunguu swaumu visivyopungua punje sita na yai bila kiini chake, kisha kunywa - mafua na baridi vitatoweka.

Kwa matatizo ya kuchafuka kwa tumbo au kujaa gesi, chukua kijiko kimoja na nusu cha mdalasini, weka kwenye kikombe kimoja cha maji yenye uvuguvugu, changanya kisha acha kwa muda wa dakika kumi na tano. Baada ya muda huo, kunywa mchangayanyiko huo, mchafuko wa tumbo utaondoka mara moja.

DONDO ZA AFYA BORA
Unene ni tatizo kubwa miongoni mwa vijana na watu wazima. Watu wengi wanakula kupita mahitaji yao halisi. Utafiti unaonesha kuwepo uhusiano mkubwa wa ulaji kupita kiasi na hatari ya kuatwa na magonjwa.

Ulaji wa chakula kiasi na chenye manufaa kiafya, kutakuhakikishia wewe na familia yako afya imara kwa miaka mingi ijayo. Ni bora kula kila siku mlo wenye faida kwa mwili wako badala ya kufanya hivyo pale unapoambiwa na daktari tu.

Ulaji wa mboga pekee (vegetarianism) unaendelea kupata umaarufu duniani kwa sababu unamuwezesha mtu kupata faida zote sawa na mtu anayekula nyama, lakini bila kuwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wowote.

Jizuie kula kupita kiasi na hakikisha unakunywa maji mengi kila siku. Wakati mwingine watu hutafsiri kiu kama njaa na kuishia kufakamia chakula wakati kilichokuwa kikihitajika mwilini kilikuwa maji tu. Hivyo tunashauriwa kutii miili yetu kwa kuhakikisha tunakunywa maji ya kutosha, hata kama hatusikii kiu, kwa sababu pale tunaposikia kiu, tayari mwili unakuwa umepungukiwa maji.

No comments: