Monday, December 29, 2008

WIKIENDA SHOWBIZ!

Lady Jaydee
Mwana FA
Prof Jizzle aka Red Carpet
Kanal Top & Dully Sykes
JI

TMK Family
Nyoshi

Waliofunika...2008
Hatimaye lile swali, ‘Nani alipoteza 2008?’ tulilouliza wiki iliyopita kupitia safu hii limepata majibu. Zikiwa zimesalia siku 2 tu, kabla ya kuufikia mwaka mpya 2009, tunachukua fursa hii kuwadondoshea majina ya baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya, bendi za muziki wa dansi, wasani wa maigizo, nyimbo na makundi yaliyofanya vyema 2008, hiyo ni kwa mujibu wa wasomaji na wapenzi wa burudani nchini.

Wasanii muziki wa kizazi kipya:
Mastaa wa muziki wa kizazi kipya waliotajwa ‘kupoteza’ 2008 ni pamoja na Chid Benz ambaye hivi karibuni alitangaza kuachana na muziki, Prof. Jay, A.Y, Marlaw, Lady Jaydee, Dully Sykes, Ali Kibba, Johmakini bila kuwasahau Mwana FA na Mr. Blue ambao wanafunga mwaka huku kazi zao, ‘Bado Nipo Nipo’ na ‘Tabasamu’ zikifunga mwaka kwa mafanikio ya kutosha.


Makundi muziki wa kizazi kipya:
Kwa upande wa makundi yaliyotajwa na wasomaji kupoteza mwaka 2008 ni TMK Wanaume Family ambalo kazi zake kama Dar Mpaka Moro, Umri na nyingine ambazo zilibamba kwa sana, bila kulisahau kundi la Nako 2 Nako Soldiers ambalo lilikimbiza na ngoma kama Hawatuwezi, Hip Hop kabla ya kusambaratika mwishoni mwa mwaka huu. Kundi lingine ni Kikosi cha Mizinga ambalo limefanikiwa kuwabadili tabia baadhi ya vijana kupitia kazi yao, ‘Hip Hop bila madawa’.

Chipukizi wa kizazi kipya:
Wasomaji na wapenzi wa muziki wa Bongo Flava pia waliwataja wasanii chipukizi waliojituma na hatimaye kufanya vizuri 2008 kupitia kazi zao ambao ni J.I aliyetoka na ngoma yenye jina la Kidato Kimoja, Tunda Man, Dulayo na Kala Jeremiah.

Dansi:
Bendi za muziki wa dansi, FM Academia na Akudo Impact ndizo zilizotajwa kupoteza zaidi 2008 kutokana na kazi zilizofanya ikiwemo kupiga shoo za nguvu zinapokuwa kunako majukwaa mbalimbali.

wasanii wa maigizo:
Kwa upande wa msanii aliyeng’ara kunako sanaa ya uigizaji, hususani filamu majina ya Ray na Kanumba ndio yametajwa na wasomaji wengi zaidi yakifuatiwa na mrembo Irene Uwoya ambaye siku chache baada ya kudondokea kunako tasnia hiyo ameonesha uwezo mkubwa.

Nyimbo zilizobamba:
Nyimbo kama ‘Habari Ndiyo Hiyo (A.Y na Mwana FA), Bado Umenuna (Marlaw), Awena (Kassim), Natamani (MB Dog), Mama Neema (20%), Hapo Vipi? (Prof. Jay), Nzela (Banana & B-Band), Kidato Kimoja (J.I), Uvumilivu (K-Sher), Bado Nipo Nipo (Mwana FA), Tabasamu (Blue) zimetajwa kufanya vizuri 2008 kupitia game ya muziki wa kizazi kipya. Kwa upande wa muziki wa dansi Diamond Musica wamelamba dume kupitia kazi yao, ‘Mapenzi Kitu Gani’ huku Dar Modern Taarab wakipoteza na wimbo wao, Gharika la Moyo.

Taarabu:
Tukija kunako sanaa ya muziki wa taarabu kundi la Jahazi limetajwa kupoteza 2008, likifuatiwa na Dar Modern (Watoto wa Kandoro).

Abby Cool & MC George Over The Weekend inawapongeza wasanii wote waliotajwa kufanya vyema 2008, tunawatakia mwaka mpya wa 2009 wenye mafanikio, waendelee kukaza ili wafike mbali zaidi. Na kwa wale ambao hawakutajwa hii ni changamoto kwao ya kujituma zaidi 2009. Tuko pamoja katika kuisongesha sanaa ya Bongo.
compiled by mc George

No comments: