Saturday, January 30, 2010

IJUMAA SHOWBIZ!

Banza kupimana ubavu na Fresh Jumbe leo!
Mwanamuziki wa Kibongo ambaye anafanya shughuli zake za kimuziki nchini Japan Fresh Jumbe leo atapanda jukwaa moja na stadi wa muziki wa dansi nchini Ramadhani Masanja a.k.a Banza Stone.

Wakali hawa kwa pamoja wanatarajia kupagawisha mashabiki ndani ya Ukumbi wa Koyanga, Yombo jiji Dar.

“Namkubali sana Banza, naamini shoo itakuwa nzuri sana. Mashabiki waje kwa wingi waone mambo ya nguvu kutoka kwetu, itakuwa shoo ya aina yake,” alisema Fresh Jumbe.

Fresh Jumbe ni msanii wa muda mrefu ambaye kibao chake cha ‘Penzi Kikohozi’ bado hakijapoa huku Banza akiwa gumzo na mipini kama ‘Mtu Pesa’, ‘Mtaji wa Masikini’ na nyingine kibao. Si ya kukosa mazee!
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@

Wagosi wa Kaya: na msumari wa Uchaguzi Mkuu!
Baada ya kimya cha muda mrefu, hatimaye wasanii wakali wa Bongo Fleva kutoka Tanga, Wagosi wa Kaya wamerudi upya kwenye game, safari hii wakiteta juu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika pini hilo walilolipa jina la ‘Maumivu ya miaka 10’ wanazungumzia juu ya uchaguzi, siasa, demokrasia na mambo mbalimbali ya kijamii.
Washkaji wamezoeleka zaidi kwa jina la ‘Wazee wa Displine’ na hii inatokana na ujumbe ambao unakuwa katika nyimbo zao, bila shaka wimbo huo nao utakuwa sawa na zilizopita.

Nyimbo nyingine za wasanii hawa ambazo zilipata kutikisa ni pamoja na Wauguzi, Tanga Kunani, Trafiki, Kero na nyingine nyingi kabla ya kimya cha muda mrefu.
**************************************

Genevieve sasa ajiweka kwa Mghana!
Mkali wa Sinema anayesumbua kinoma kwenye Film Industry nchini Nigeria Genevieve Nhanji sasa amenasa kwa mcheza filamu maarufu kutoka Ghana.

Kwa mujibu wa mtandao mmoja wa burudani, Genevieve amejiweka kwa staa huyo ambaye jina lake bado ni siri, ikiwa ni baada ya kukaa single kwa muda mrefu.

Staa huyo amewahi kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari,akisema kwamba anajisikia vizuri sana kubaki msela huku akimpa mwanaye malezi bora zaidi.

Mmoja wa mashabiki wa Gene nchini Nigeria, alisema: “Safari hii kanasa, naamini kinachofuata ni ndoa, wapo karibu sana, kiasi kwamba huwezi kuamini kama Genevieve anaweza kuishi bila huyo jamaa...isitoshe ni muda mrefu sana alikuwa mpweke, nadhani wataona.”

Mastaa hao walikutana kwa mara ya kwanza nchini Ghana wakiwa location kwa ajili ya kurekodi filamu iliyowashirikisha baadhi ya nyota wa Nigeria na Ghana.
****************************************

Taraji p. Henson: aingia kwenye orodha ya wanawake 10 matajiri
Mwigizaji mahiri wa filamu kutoka Hollywood, Taraji P. Henson ameingia kwenye orodha ya wanawake kumi matajiri zaidi kufuatia filamu yake ya Date Night iliyoingia sokoni mwezi Desemba mwaka jana, kufanya vizuri na kufikia kiwango cha juu kabisa cha Double Platinum.

Taraji ambaye anashikilia tuzo ya Oscar, aliyoipata mwaka jana baada ya kuchaguliwa kuwa mmoja wa Waigizaji Bora wa Hollywood na mcheza sinema bora zaidi wa kike baada kucheza kwa mafanikio Filamu ya ‘The Curious Case of Benjamin Button’, amesema anamshukuru Mungu kwa mafanikio aliyopata na amepanga kufanya makubwa zaidi mwaka huu.

“Siku zote Mungu ndiyo wa kwanza kwa kila kitu. Nilianza kwa shida lakini sasa niko juu, nashukuru kwa hilo. Kwangu mimi huu ni wakati wa kufanya kazi zaidi ili kumuandalia maisha bora mwanangu Marcel,” alisema Taraji.

Umaarufu wa Ta raji ulianza kusambaa duniani mwaka 2001, baada ya kutoka kwa Filamu ya ‘Baby Boy’ aliyoshirikiana na nyota wa muziki Tyrese Gibson.

Sinema nyingine alizoonesha cheche ni pamoja na ‘Hustle & Flow’ (2005), ‘The Family That Preys’ (2008) na nyinginezo.

No comments: